Nyuki wavamia shule wajeruhi wanafunzi 11, walimu watatu

Morogoro. Wanafunzi 11 na walimu watatu wa Shule ya Msingi Kambi Tano iliyopo Mtaa wa Kambi Tano, Kata ya Lukobe katika Manispaa ya Morogoro, wamejeruhiwa baada ya kushambuliwa na kundi la nyuki waliovamia eneo la shule hiyo leo Jumatano Februari 11, 2026.

Majeruhi wote walipelekwa katika Kituo cha Afya Lukobe, walikopatiwa matibabu na baadaye kuruhusiwa kurejea nyumbani baada ya hali zao kuimarika.

Tukio hilo limetokea asubuhi wakati wanafunzi hao wakiwa darasani wakiendelea na masomo.

Mbali na kusababisha majeruhi, pia liliibua taharuki kwa wananchi wanaoishi jirani na shule hiyo, hasa ikizingatiwa kuwa ni tukio la pili la aina hiyo kutokea katika mtaa huo.

Akizungumza baada ya kukamilika kazi ya uokoaji, Kamanda wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Morogoro, Shabani Marugujo amesema walipokea taarifa ya tukio hilo kutoka kwa Polisi Kata, Mkaguzi wa Polisi Zuwena Mwita, mara moja kikosi cha uokoaji kilifika shuleni hapo.

Hali ilivyokuwa kwenye shule ya msingi kambitano iliyopo kata ya Lukobe baada ya wanafunzi na walimu kukimbia kufuatia nyuki kuvamia shuleni hapo na kung’ata wanafunzi 11 na walimu watatu, vipindi vya masomo shuleni hapo leo vimesitishwa Hadi kesho Februari 12 vitakapoendelea kama kawaida. Picha Hamida Shariff



Amesema timu ya waokoaji iliyoongozwa na Stafu Sajenti, Alexander Makuluni ilikuta kundi kubwa la nyuki likiwa limetanda angani na wengine wakiwa wamejikusanya kwenye mnara uliobeba tanki la maji ndani ya shule hiyo.

“Baadhi ya nyuki walikuwa wametanda angani, huku wengine wakiwa wamejikita kwenye mnara wenye tanki kubwa la maji. Tulilazimika kutumia kiuatilifu kuwatawanya na kuwadhibiti hadi eneo lote likawa salama,” amesema Marugujo.

Kamanda huyo amewataja majeruhi kuwa ni Agness Timbi, Mohamed Shabani, Chiku Mussa, Hilari Athuman, Sabri Mengi, Ismail Mohamed, Amani Msimbe, Jackob Mnyaki, Mustapha Hassan, Violeth Brutusu, Brightness Mlema, Neema Omary, Mswahibu Ibrahim na Rukia Seif.

Ameongeza kuwa baada ya kuwadhibiti nyuki hao, kikosi chake kilihakikisha kinawapeleka majeruhi katika Kituo cha Afya cha Kata ya Lukobe kwa ajili ya matibabu zaidi.

Akisimulia tukio hilo, Mwenyekiti wa Mtaa wa Kambi Tano, Elianini Kimaro amesema hili ni tukio la pili la uvamizi wa nyuki katika eneo hilo.

Amesema mwaka jana tukio kama hilo lilisababisha kifo cha mtoto mmoja baada ya nyuki kuvamia makazi ya watu.

“Hawa nyuki walikuwa wameweka makazi yao kwenye tanki la maji bila mtu yeyote kufahamu. Ghafla walivamia na kuanza kuwashambulia wanafunzi pamoja na walimu,” amesema Kimaro.

Ameeleza kuwa katika tukio hilo mwalimu mmoja kati ya watatu waliojeruhiwa alikuwa na hali mbaya zaidi, lakini ametibiwa na hali yake kutengemaa kabla ya kuruhusiwa kurejea nyumbani.

Kuhusu ratiba ya masomo, Kimaro amesema baada ya tukio hilo wanafunzi wengi walikimbia nyumbani kwao kwa hofu na baadhi walibaki ndani ya madarasa kwa usalama. “Baada ya hali kutulia, wanafunzi wote waliruhusiwa kurudi nyumbani, masomo yataendelea kesho kama kawaida,” amesema.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Lukobe, Selestin Mbilinyi amesema baada ya juhudi za kikosi cha zimamoto na uokoaji kuwadhibiti nyuki hao, hali ya usalama imerejea na hakuna tishio lolote kwa sasa.

“Baada ya nyuki kudhibitiwa, tumewahakikishia wazazi na walezi kuwa mazingira ya shule ni salama. Kesho masomo yataendelea kama kawaida,” amesema Mbilinyi.

Taharuki ilitanda miongoni mwa wazazi na walezi wa wanafunzi wa Shule ya Msingi Kambi Tano pamoja na shule jirani ya Lukobe, wakihofia usalama wa watoto wao.

Hata hivyo, viongozi wa eneo hilo wamewahakikishia kuwa hatua stahiki zimechukuliwa na mazingira kwa sasa ni salama.

Askari wa kikosi cha zimamoto na uokoaji mkoa wa Morogoro wakipuliza dawa Kwa ajili ya kuwafukuza nyuki walioweka makazi kwenye tenki la maji la shule ya msingi kambitano iliyopo mtaa wa kambitano kata ya Lukobe Manispaa ya Morogoro ambapo Leo nyuki hao walitimuka na kung’ata wanafunzi 11 na walimu watatu wa shule hiyo. Picha Hamida Shariff



Mmoja wa wazazi, Joseph Exavery ameutaka uongozi wa shule kuweka utaratibu wa kukagua mazingira ya shule mara kwa mara ili kubaini mapema uwepo wa makazi ya nyuki au hatari nyingine zinazoweza kuhatarisha usalama wa wanafunzi.

“Shule hii ipo nje ya mji na mazingira yake yanaweza kuvutia nyuki, kama vile maboma ya nyumba, miti na mazao kama alizeti. Katika kipindi hiki cha joto kali, nyuki hujitokeza kwa wingi, hivyo ni muhimu walimu na viongozi wachukue tahadhari za mara kwa mara,” amesema Exavery.