Pande mbili siku 100 za Rais Samia

Dar es Salaam. Muhula wa pili wa urais wa Samia Suluhu Hassan unatimiza siku 100 leo. Kwa tathmini ya wadau, ni kipindi kilichoonesha mwanga wa utekelezaji wa ahadi zake, huku wengine wakitilia shaka baadhi ya mambo.

Samia aliapa kuwatumikia Watanzania zaidi ya milioni 60 Novemba 3, 2025, baada ya kushinda katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 29 mwaka huo, ikiwa ni uongozi wake wa muhula wa pili Ikulu.

Wanaosema kuna mwanga wa matumaini, wanaijenga hoja hiyo kwa kurejea mafanikio ya utekelezaji wa ahadi alizozitoa wakati wa kampeni, ikiwemo kukomesha uzuiaji wa maiti hospitalini, ajira kwa walimu na wataalamu wa afya, bima ya afya kwa wote na fedha za uwezeshaji wajasiriamali.

Kwa wanaotilia shaka, wanajenga hoja kwa kutoona dalili za utekelezaji wa baadhi ya ahadi, ikiwemo ya kuanzishwa kwa mchakato wa Katiba mpya, Gridi ya Taifa ya Maji, huduma bure za matibabu kwa wagonjwa wa moyo, saratani, figo na kisukari, na kudumisha amani, mshikamano na haki za raia.

Kwa maneno mafupi, tathmini ya wadau inaonesha utendaji wa Rais Samia kwa siku 100 umebeba matumaini na mashaka ndani yake, hasa kwa zile ahadi ambazo Watanzania walitamani zianze kutekelezwa, ikiwemo Katiba mpya.

Lakini wapo waliosema uongozi wake utakwenda vema na atayavuka mengi iwapo atajikita kuirudisha falsafa yake ya R4 (ustahimilivu, kujenga upya, maridhiano na mageuzi), wakisema itasaidia kuleta mshikamano, umoja na upendo miongoni mwa Watanzania.

Kuna matumaini, bado Katiba mpya

Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Sheikh Nuhu Mruma, anasema Rais Samia baadhi ya aliyoyahidi ameyatekeleza kwa ufanisi na baraza hilo linampongeza, lakini bado Katiba Mpya hawajui utekelezaji wake utakuaje au mchakato unasubiria hatua ya maridhiano kwanza.

“Ingawa suala hili lina mchakato kidogo hadi kulifikia, lakini aliliahidi ndani ya siku 100. Kikubwa tunampongeza, kwa yale machache yaliyobakia, basi yapate utekelezaji.

“Yale yaliyotekelezwa yanapaswa usimamizi bora na endelevu ili kuleta maendeleo kwa jamii. Waliopewa majukumu ya kusimamia wasimamie kikamilifu ili dhamira ya Rais Samia itimie na wananchi wanufaike,” anasema Sheikh Mruma.

Anasema yaliyoahidiwa ndani ya siku 100 ni machache, lakini kuna mengi, ikiwemo kuongeza juhudi za umoja na mshikamano katika Taifa, yanapaswa kuwekewa msukumo ili kuleta tabasamu kwa Watanzania.

Hoja kama hiyo ilitolewa pia na Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Maaskofu na Masheikh (inayosimamia haki, amani na maadili kwa jamii ya madhehebu ya dini zote), Askofu William Mwamalanga, anasema pamoja na ahadi hizo kutekelezwa, Rais Samia anapaswa kulitilia mkazo suala la Katiba mpya.

“Katiba mpya imepigiwa kelele kwa muda mrefu, ndiyo maana Rais Samia alipoahidi ndani ya siku 100 kuhusu mchakato huo, alifurahiwa na kila Mtanzania. Lakini katika hilo hajagusa hata kimoja, kwa sababu Katiba mpya ni jambo la muhimu,” anaeleza.

Aidha, Askofu Mwamalanga anamshauri mkuu huyo wa nchi kurudi kwenye falsafa za R nne (kujenga upya, mageuzi, maridhiano na ustahimilivu) zitakazowezesha pia waliofungwa kisiasa kurudi uraiani.

“Rais Samia alikumbuke lile faili la R nne, litampa heshima kubwa sana. Unajua tunaelekea kwenye Kwaresma na mfungo wa Ramadhan, lazima watu warudi kwenye mapatano ndani ya mioyo yao,” anasema Mwamalanga.

Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Dodoma, Christian Ndosa, anasema ndani ya siku 100 Rais Samia amejitahidi kutekeleza ahadi zake, ingawa si kwa asilimia zote.

“Nguvu aongeze kwenye upatikanaji wa dawa za uhakika katika hospitali ambako bado kuna changamoto hiyo,” anaeleza Askofu Ndosa.

Kuhusu demokrasia, Askofu Ndosa anasema kuna changamoto zake, lakini Rais Samia akiongeza nguvu kidogo ataweza kutatua matatizo yanayoikumba eneo hilo.

“Kama tulivyosema katika ujumbe wa Krismasi kwamba hata walioko kwenye magereza waachiwe huru, namshauri Mama (Rais) awaachie, mambo yatakwenda vizuri sana,” anasema Askofu Ndosa.

Kwa upande wake, Askofu wa Kanisa la Anglikana, Dayosisi ya Dar es Salaam, Jackson Sostheness, anasema kuhusu yasiyotekelezwa, kila kitu kina wakati na mchakato, ingawa kuna mambo angependa kuona yanapewa kipaumbele kwa namna moja au nyingine.

Kwa mujibu wa Askofu Sostheness, mambo hayo ni mshikamano wa kitaifa, akisema unapaswa kuangaliwa kwa upana wake, akirejea vurugu za Oktoba 29, 2025.

“Kumekuwa na dalili au chembechembe za ufa wa kidini, kuona kwamba dini fulani na fulani… kinachopaswa ni viongozi wa dini kuwa katika mstari mmoja na kuwa na lugha moja kuwasaidia Watanzania.

“Nampongeza kwa utekelezaji wa ahadi alizoahidi, lakini nasisitiza jitihada zifanyike ili viongozi wa dini tutembee pamoja na tutofautiane kwenye mitazamo tu,” anaeleza Askofu Sostheness.

Wadau wa afya, demokrasia

Rais wa Chama cha Wafamasia Tanzania (TPS), Fadhili Hezekiah, anasema mengi yanayoonekana katika siku 100 ni matokeo ya maandalizi ya muda mrefu, lakini sasa yamepata kasi na uwezeshaji wa kisera.

“Bima ya afya kwa wote imepata msukumo mkubwa katika siku hizi 100. Sambamba na hilo, tumeona jitihada za dhati za kuchochea uanzishwaji wa viwanda vya dawa nchini, jambo ambalo ni muhimu katika kuboresha upatikanaji wa dawa na kupunguza gharama,” anasema Hezekiah.

Anasema hatua ya Serikali kumteua Naibu Katibu Mkuu mahususi kusimamia sekta ya dawa na vifaa tiba ni ishara ya kutambua umuhimu wa eneo hilo katika mfumo mzima wa afya.

“Hii haitahusu uzalishaji pekee, bali pia usambazaji na matumizi sahihi ya dawa ili kuongeza tija na thamani ya fedha. Tunaona katika siku hizi 100 michakato mingi ikiwekwa sawa kuhakikisha mfumo unafanya kazi kwa ufanisi,” anasema.

Kwa mujibu wa Hezekiah, mwelekeo huo umefungua fursa mpya za ajira kwa wafamasia, hususan wale wenye uwezo wa kuandika miradi, kufanya tafiti na kushirikiana na wadau wa maendeleo.

Kwa upande wake, Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Mugisha Nkoronko, anasema siku 100 za mwanzo zimeonesha wazi shauku na utashi wa kisiasa katika sekta ya afya.

Anasema siku 100 ni kipindi kifupi kutatua changamoto zote zinazoukabili mfumo wa afya nchini, akisisitiza haja ya kuongeza kasi ya utekelezaji.

“Tunahitaji kasi zaidi katika kuongeza idadi ya wafanyakazi wa kutosha, kupanua wigo wa huduma, kusimamia ubora wa huduma na kuboresha maslahi ya watumishi wa sekta ya afya, hususan madaktari wazalendo,” anasema.

Mtaalamu wa masuala ya afya, Dk Elisha Osati, anasema uelekeo wa uongozi wa Rais Samia ni mzuri, hasa matokeo chanya katika utekelezaji wa bima ya afya kwa wote, uzalishaji wa dawa na kuondosha uzuiaji wa maiti.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga, anadai siku 100 za uongozi wa Serikali zimegubikwa na juhudi za kutuliza joto la kisiasa, lakini mvutano kati ya wananchi na Serikali bado unaendelea.

“Kuna mambo mengi Serikali inasema imeyatekeleza, lakini wananchi wanasema hayajaonekana. Hizi zimekuwa siku 100 za mvutano mkubwa, hasa katika mitandao ya kijamii,” anasema.

Henga anasema katika kipindi hicho, baadhi ya wapinzani waliopo magerezani wameendelea kulalamikia kukosa haki, wakitaka kusikilizwa licha ya jitihada za Serikali kutoa ufafanuzi.

Kuhusu tume ya kuchunguza matukio ya Oktoba 29, Henga anasema ingawa hadi sasa haijatoa mrejesho kwa wananchi, lakini ilishakosa uungwaji mkono kwa umma tangu kuundwa kwake.

Makamu Mwenyekiti wa Taifa wa NCCR–Mageuzi (Bara), Joseph Selasini, anadai hawajaridhika na hali iliyopo hadi pale ukweli utakapojulikana kuhusu kilichotokea Oktoba 29.

“Kama wanazungumzia maridhiano, wanaridhiana na nani na juu ya jambo gani? Kama hawakiri kuwa kuna tatizo linalohitaji maridhiano, basi maridhiano yenyewe yatakuwa juu ya nini?” anahoji.

Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar, Khamis Mbeto, anasema ndani ya siku 100 Rais Samia ameonesha utayari wa kuzungumza kukiwa na jambo ili kuhakikisha nchi inakuwa na amani na utulivu.

“Ameunda kitu kikubwa katika kudumisha maridhiano, tume ya kuchunguza yaliyojitokeza Oktoba 29, na kuonesha utayari wa kuzungumza yote hayo kuhakikisha kuna amani na utulivu,” amesema.

Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, Juma Ali Khatibu, anapongeza utekelezaji wa ahadi zilizoahidiwa na mkuu huyo wa nchi tangu ashike madaraka katika muhula wa pili.

“Ameanza kazi vizuri na anapaswa kuungwa mkono na viongozi wengine wa kisiasa ili atekeleze malengo yake kwa maslahi mapana ya Taifa, licha ya changamoto zilizopo,” anasema Khatibu.

Hata hivyo, Khatibu amekumbushia Serikali kutekeleza ahadi yake ya upatikanaji wa Katiba mpya, akisema ni jambo linalosubiriwa kwa matumaini makubwa na Watanzania.

Mchambuzi wa masuala ya siasa, Seif Nassor, anasema nchi inaendelea kushuhudia amani, utulivu na maendeleo ya kijamii, hali inayoashiria mwanzo mzuri wa uongozi wa Rais Samia licha ya changamoto za awali.

“Amani na utulivu ni msingi wa maendeleo. Nchi ilikuwa katika mtafaruku mkubwa, lakini sasa wananchi wanaendelea na shughuli zao za kila siku kama kawaida,” anasema Nassor.

Anadai bado kuna changamoto za kiusalama, akirejea matukio ya Oktoba 29 yaliyohusisha uchomaji wa miundombinu ya umma, akisema kurejesha hali ya kawaida ni kazi inayohitaji mshikamano wa kitaifa.

Seif anamshauri Rais Samia kushirikiana na wataalamu wa sekta mbalimbali ili kupata ushauri wa kitaalamu utakaosaidia kusukuma gurudumu la maendeleo.

Mkurugenzi wa Shirikisho la Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Deogratius Massawe, anasema siku 100 za uongozi wa Rais Samia zina matumaini.

“Zina matumaini, lakini kuna sehemu za kisekta tunaziangalia ili tuone zinaendaje ili kuendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050. Tunafanya uchambuzi wa kina, na ninadhani Februari 15 tutakuwa na majibu sahihi,” anasema Massawe.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Lutengano Mwinuka, anasema ni mapema kuelezea kilichofanyika ndani ya siku 100 za utendaji wa Rais Samia, hasa katika kipindi ambacho kama nchi baadhi ya fedha katika utekelezaji wa majukumu yake zilikuwa zikitegemewa kutoka kwa wahisani ambao sasa wameonekana kulegalega.

“Kwa hiyo ni lazima turejee kuona mipango itaendaje kuendana na uhalisia huo, mipango iweje, vyanzo vya mapato na matumizi yanakuwaje. Sijaona mabadiliko yanayoendana na uhalisia wa kile tulichonacho na tunachoweza kupata ili kuendana na hali halisi,” anasema.

Katika hilo, Profesa Haji Semboja wa Chuo Kikuu cha Zanzibar (SUZA) anasema kitendo cha kuapishwa na kusema kazi iendelee kilikuwa ni ishara kuwa ataendelea kutekeleza yale aliyokuwa akiyafanya katika awamu ya kwanza.

Anasema jambo hilo lilifanya biashara kuendelea kufanyika, kuendelea kujenga imani kwa wawekezaji kwa kuona kuwa hakuna kitu kitakachobadilika, jambo ambalo limeendelea kuvuta mitaji mingi.

“Angalizo tu ni haya yote yanayopangwa yafanyike kwa mujibu wa sheria na kanuni zilizopo, tusijaribu kutafuta kitu kipya,” anasema.

Katibu wa Taasisi na Jumuiya za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda, anasema kuna ahadi zilitolewa kuleta maridhiano, kuondoa hofu na kuleta matumaini, lakini bado hajafanikiwa.

“Ninachoona bado hofu imeendelea kutanda kwa wananchi katika kiwango ambacho kinaonekana kwa macho, ukipita sehemu mbalimbali unaona askari wametanda hapa na pale,” anasema.

Mwananchi limezungumza na wananchi juu ya siku 100 na kuwa na mitazamo tofauti. Mkazi wa Sokoine, jijini Mbeya, Samson Mwakalukwa, anasema utekelezaji wa mpango wa bima ya afya kwa wote umeleta matumaini katika ahadi alizotoa Rais Samia.

“Tumeona baadhi ya ahadi zake kwetu ameanza kutekeleza, aliahidi kongani za viwanda ambazo kwa sasa tunasubiri utekelezaji wake, ila kwenye bima ya afya kwa wote hatumdai,” anasema Mwakalukwa.

Naye Neema Mwakajila wa Sokoine anasema ahadi za taa za barabarani ili kusaidia vijana kujiajiri katika maeneo ya Ilomba, Sae, Uyole na barabara ya Chunya jijini Mbeya bado hazijatekelezwa.

“Aliahidi kongani za viwanda hatujaona, taa za barabarani bado, na hata ajira kwa vijana tatizo ni kubwa. Tunaomba kuona anatufikia wananchi moja kwa moja ili miaka mitano yake iwe na mabadiliko chanya,” anasema Neema.

Rahil Salimu, mkazi wa jijini Mwanza, anasema siku 100 za Rais Samia zinaleta matumaini kwa wanafunzi wanaomaliza vyuo katika kada mbalimbali kwa sababu ndani ya siku hizo Serikali imetoa ajira kama alivyoahidi wakati wa kampeni. Kwa hiyo, anaona kama amejitahidi kutimiza baadhi ya ahadi na kuwapa motisha vijana wanaosoma na wale waliokuwa majumbani muda mrefu bila ajira.

Kwa upande wake, Amos Chacha, mkazi wa Musoma, mkoani Mara, anasema siku 100 za Rais Samia kwake haoni jambo kubwa lililofanyika kwa sababu changamoto za wananchi bado zipo na zinaendelea.

“Binafsi sioni sababu ya kumpima mtu utendaji wake ndani ya siku 100, kwani ni muda mfupi tumpe angalau mwaka mmoja ili tuwe na namna nzuri ya kumpima utendaji wake.

Anasema haiwezekani mtu akamaliza changamoto ndani ya siku 100, hata kama ni kutekeleza mradi, hakuna mradi unaoweza kutekelezwa kwa muda huo.

Kwa hiyo, anadhani ni bora kumpa Rais muda wa kutimiza majukumu yake kabla ya kumpima, kwani uchaguzi unafanyika kila baada ya miaka mitano, kipindi kinachotosheleza kutathmini utendaji wake kulingana na ahadi alizotoa na matokeo aliyoyafanikisha.