Dar es Salaam. Jitihada za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) za kupangua kwa mbinu za kiufundi kesi ya mgogoro wa mgawanyo usio sawa wa rasilimali kati ya Tanzania Bara na Zanzibar inayokikabili, zimegonga ukuta baada ya Mahakama kutupilia mbali pingamizi lake.
Kesi hiyo ya madai namba 8323 ya mwaka 2025 imefunguliwa na Makamu Mwenyekiti mstaafu wa Chadema-Zanzibar, Said Issa Mohamed, pamoja na wajumbe wawili wa Bodi ya Wadhamini wa Chadema kutoka Zanzibar, Ahmed Rashid Khamis na Maulida Anna Komu.
Wadaiwa katika kesi hiyo inayosikilizwa na Jaji Hamidu Mwanga wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Dar es Salaam, ni Bodi ya Wadhamini Waliosajiliwa wa Chadema na Katibu Mkuu wa chama hicho.
Wadai wanadai kumekuwa na mgawanyo usio sawa wa mali za chama na rasilimali za kifedha kati ya Tanzania Zanzibar na Tanzania Bara, kinyume cha Sheria ya Vyama vya Siasa na Katiba ya chama hicho.
Pia wanadai kuna ubaguzi wa kidini na kijinsia, pamoja na utoaji wa maoni na matamko yenye nia ya kuvuruga Muungano kati ya pande mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kesi hiyo ilipotajwa Septemba 29, 2025, wadaiwa waliibua pingamizi la awali wakihoji mamlaka ya mahakama hiyo kuisikiliza.
Waliiomba mahakama hiyo iitupilie mbali kesi bila kuisikiliza, wakidai haina mamlaka ya kuisikiliza, huku wakibainisha sababu saba za pingamizi hilo.
Pamoja na mambo mengine, katika pingamizi hilo wadaiwa walidai madai ya wadai yanahusu mambo ya kikatiba, lakini kesi hiyo imefunguliwa kama kesi ya madai ya kawaida badala ya kesi ya kikatiba.
Desemba Mosi, 2025, Jaji Mwanga alielekeza kesi hiyo isikilizwe kwa njia ya maandishi na akapanga kutoa uamuzi kuhusu pingamizi hilo Februari 17, 2026 au tarehe yoyote kabla ya hapo ambayo pande zote zitajulishwa.
Leo, Februari 11, 2026, mahakama hiyo imetoa uamuzi ambapo imetupilia mbali pingamizi hilo.
Jaji Mwanga amesema baada ya kupitia hoja za pingamizi la wadaiwa na majibu ya wadai, amejiridhisha kuwa hoja hizo hazina mashiko ya kisheria.
Amesema baadhi ya hoja za pingamizi zilizotolewa na wadaiwa, zikiwemo zinazohusiana na mamlaka ya mahakama, zilishawahi kuamuliwa hivyo hazikupaswa kurejeshwa tena kama pingamizi isipokuwa kwa njia ya rufaa.
Pia amesema hoja nyingine, ikiwemo ya wadai kutostahili kufungua kesi hiyo kwa kuwa ni viongozi, zinahitaji ushahidi baada ya kusikilizwa kwa pande zote na hivyo hazistahili kuwa hoja za pingamizi la kisheria.
Kuhusu madai ya kesi hiyo kufunguliwa kama kesi ya madai ya kawaida badala ya kesi ya kikatiba, Jaji Mwanga amesema masuala ya ukatiba, ikiwemo ubaguzi, pia yanatajwa katika Sheria ya Vyama vya Siasa, hususan kifungu cha 6 cha sheria hiyo.
Hivyo amesema masuala ya kikatiba yanapotajwa katika sheria ya kawaida yanapaswa kwanza kushughulikiwa kupitia sheria hiyo kabla ya kufunguliwa kama kesi ya kikatiba.
“Kuzingatia hayo yaliyoelezwa hapo, mahakama hii inaona kwamba hoja za pingamizi hili hazina mashiko kwa kiwango kilichoelezwa; hivyo pingamizi hilo halina mashiko na mahakama inalitupilia mbali,” amesema Jaji Mwanga baada ya uchambuzi wa hoja hizo na kurejea sheria na maamuzi ya kesi mbalimbali.
Kwa uamuzi huo, sasa mahakama itaendelea na usikilizwaji wa kesi ya msingi kwa tarehe itakayopangwa.
Katika kesi ya msingi, walalamikaji wanaomba Mahakama itamke kuwa wadaiwa wamekiuka kifungu cha 6A(1), (2) na (5) cha Sheria ya Vyama vya Siasa, Sura ya 258 Marejeo ya mwaka 2019, na iwaelekeze wazingatie kifungu hicho.
Pia wanaiomba Mahakama itamke kuwa ugawaji wa fedha, mali na rasilimali kwa ajili ya shughuli za kisiasa na kiutawala kati ya Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar unaofanywa na wadaiwa ni kinyume cha sheria na ni batili.
Vilevile wanaomba mahakama isitishe kwa muda shughuli zote za kisiasa mpaka maagizo ya mahakama yatakapotekelezwa, na itoe zuio la kudumu dhidi ya matumizi ya mali, fedha na rasilimali za chama hadi walalamikiwa watakapotekeleza matakwa ya sheria husika pamoja na kulipa gharama za kesi.
Wadai hao wanawakilishwa na jopo la mawakili linaloongozwa na Wakili Shaban Marijan akisaidiana na mawakili Gido Simfukwe na Alvan Fidelis.
Wadaiwa wanawakilishwa na jopo la mawakili linaloongozwa na Dk Rugemeleza Nshala na Hekima Mwasipu pamoja na mawakili wengine kadhaa.
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, amewasilisha maombi akiomba kuunganishwa katika kesi hiyo kama mdaiwa mwenye maslahi.
Wajibu maombi katika shauri hilo ni pamoja na wadai katika kesi ya msingi, yaani Said na wenzake kwa upande mmoja, na Wadhamini wa Chadema pamoja na Katibu Mkuu ambao ni wadaiwa katika kesi ya msingi.
Hata hivyo, wajibu maombi hao ambao ni wadai katika kesi ya msingi, yaani Said na wenzake, wamemuwekea pingamizi la awali.
Maombi hayo yametajwa mahakamani hapo leo huku Lissu mwenyewe akihudhuria, na akaomba apatiwe majibu ya maombi yake na kiapo kinzani kutoka kwa wajibu maombi.
Jaji Mwanga amewaelekeza wajibu maombi hao kumpatia nakala ya majibu yao na kiapo kinzani huku akipanga kusikiliza pingamizi hilo Februari 17, 2026, tarehe ambayo kesi ya msingi pia itatajwa.
Ingawa mawakili wa wajibu maombi, Said na wenzake, wameomba pingamizi hilo lisikilizwe kwa njia ya maandishi, Lissu ameomba ajibu hoja hizo kwa mdomo akidai kuwa kwa kuwa yupo mahakamani haoni haja ya kuandika; ombi ambalo mahakama imekubaliana nalo.