RAS ARUSHA AWEKA MKAZO KUIMARISHA UTALII NA KUONDOA URASIMU KWA WAWEKEZAJI

Na Pamela Mollel,Arusha 

Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Dk. Toba Alnason Nguvila, ameweka mkazo katika kuimarisha sekta ya utalii mkoani humo kwa kuwataka watumishi wa umma kufanya kazi kwa weledi, uwajibikaji na kuondoa urasimu unaoweza kukwamisha wawekezaji na wadau wa utalii.

Akizungumza na watumishi wa umma katika hafla fupi ya mapokezi iliyofanyika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha Februari 10, 2026, Dk. Nguvila amesema kuwa Arusha ni lango kuu la utalii, hivyo utendaji wa watumishi unapaswa kulenga kuweka mazingira rafiki kwa uwekezaji na utoaji huduma bora kwa wadau wa sekta hiyo.

Amesisitiza kuwa kila mtumishi ana wajibu wa kuwa kichocheo cha maendeleo ya utalii kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu bila kuweka vikwazo visivyo vya lazima vinavyoweza kudhoofisha ukuaji wa sekta hiyo muhimu ya uchumi.

“Nitahakikisha hakuna urasimu wala migogoro inayokwamisha wawekezaji wa utalii. Kila wilaya ina vivutio vyake, hivyo tunapaswa kushirikiana kuvikuza kwa manufaa ya mkoa na taifa kwa ujumla,” amesema Dk. Nguvila.

Aidha, amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri kutenga bajeti mahsusi kwa ajili ya shughuli za utalii, kubuni na kuimarisha vyanzo vipya vya mapato pamoja na kusimamia ukusanyaji wake kwa ufanisi.

Katika hatua nyingine, amewataka viongozi hao kuendesha kampeni za elimu na uhamasishaji wa wananchi kujiunga na Bima ya Afya kwa Wote, akieleza kuwa mpango huo utasaidia kuboresha ustawi wa wananchi na upatikanaji wa huduma za matibabu.

Awali, Dk. Nguvila alimshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini na kumteua kushika wadhifa huo, akiahidi kushirikiana na wataalamu wa ngazi zote kuhakikisha wananchi wa Arusha wanapata huduma bora kwa kuzingatia sheria na miongozo ya Serikali.