Sababu mikoa hii kuongozwa na askari

Dar es Salaam. Kwa zaidi ya muongo sasa, magwanda ya kijeshi na taaluma ya ulinzi , imeshuhudiwa ikichukua nafasi zaidi katika teuzi za wakuu wa mikoa ya Kagera, Kigoma, Mtwara na Ruvuma.

Ingawa katika kipindi hicho baadhi ya raia wamewahi kupata nafasi za kuiongoza mikoa hiyo, askari wa Jeshi la Ulinzi wa Wananchi Tanzania (JWTZ) na maofisa wengine wa vyombo vya ulinzi na usalama, Jeshi la Polisi au Magereza ndio waliopewa nafasi zaidi.

Wachambuzi wa siasa na masuala ya ulinzi wanahusisha uamuzi huo na umuhimu wa usalama, wakisema mikoa hiyo ipo katika ukanda unaogusa moja kwa moja mipaka ya kimataifa.

Hata hivyo, wengine wanasema hakuna uhusiano wowote kati ya uteuzi wa askari hao na masuala ya usalama, wakisisitiza kuwa, hata kama mkuu wa mkoa angekuwa mwanajeshi, hawezi kutoa amri inayozidi mamlaka ya wadhifa aliyepewa.

Februari 9, 2026, Rais Samia Suluhu Hassan aliwaapisha viongozi mbalimbali, wakiwemo wakuu wa mikoa wawili—Kanali Yahya Kido wa Kagera na Kanali Donald Msengi wa Mtwara. Alisema mikoa hiyo ni kimkakati kwa masuala ya ulinzi wa nchi, ndiyo maana aliwatoa jeshini kutokana na umuhimu wake.

Rais Samia aliweka wazi kuwa wakuu wa wilaya watakaoapishwa katika mikoa ya Kagera na Mtwara watakuwa wale watakaoendana na wakuu wa mikoa aliowaapisha, kwani mikoa hiyo ni muhimu si tu kwa ulinzi, bali pia kwa usalama wa taifa.

“Nitakupangieni ma-DC ambao mnaweza kwenda nao na lugha moja ili kuimarisha ulinzi katika mikoa ile. Ni mikoa ya kimkakati kwetu… narudia, ile miwili ni mikoa muhimu kwetu, ndiyo maana nimetoa makanali jeshini nimewaleta huku,” alisema Rais Samia.

Mkoa wa Kagera unapakana na nchi nne (Uganda, Rwanda, Burundi na Kenya kupitia Ziwa Victoria), hivyo umekuwa na idadi kubwa ya wakuu wa mikoa na wilaya waliotoka jeshi.

Miongoni mwao walikuwa Meja Jenerali Salum Kijuu, Brigedia Jenerali Marco Gaguti, Meja Jenerali Charles Mbuge na sasa ni Kanali Yahya Kido.

Pia, baadhi ya ma-DC mkoani Kagera ni Kanali Fabian Massawe (Karagwe), Luteni Kanali Benedict Kitenga (Ngara), Kanali Michael Ngayalina (Karagwe), Kanali Denis Mwila (Missenyi), Kanali Mathias Kahabi (Biharamulo) na Luteni Kanali Wilson Sakulo (Ngara).

Mkoa wa Mtwara unaopakana na Msumbiji, maaskari waliowahi kuwa wakuu wa mkoa huo ni Kanali Donald Msengi, Kanali Patrick Sawala, Kanali Ahmed Abbas Ahmed na Brigedia Jenerali Marco Gaguti.

Ma-DC ni Kanali Patrick Sawala (Tandahimba), Kanali Ahmed Abbas Ahmed (Nanyumbu), Luteni Kanali Simon Gofia (Mtwara Mjini), Kanali Hosea Ndagala (Masasi), ACP Advera Bulimba (Newala) na Kanali Evance Balama (Mtwara).

Kigoma                                                            

Kigoma inapakana na Burundi (kaskazini na kaskazini-mashariki) na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (magharibi). Pia inapakana na Zambia (kusini-magharibi) kupitia Ziwa Tanganyika.

Mkoa wa Kigoma pia unapakana na nchi ya Zambia kwa mbali upande wa kusini-magharibi kupitia maji ya Ziwa Tanganyika (ingawa mpaka mkuu wa nchi kavu wa Tanzania na Zambia upo mkoani Songwe na Rukwa).

Kutokana na mkoa huo kupakana na nchi hizo imekuwa na wakuu wa mkoa maaskari ambao ni Mkuu wa Jeshi la Polisi mstaafu, Balozi Simon Sirro. Kabla ya Sirro alikuwa askari polisi Thobias Andengenye, aliyekuwa na cheo cha  Kamishna wa Polisi (CP).

Andengenye kabla ya kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kigoma aliteuliwa kuwa Mkuu wa Jeshi la Zimamoto akiwa na cheo cha Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji (CGF).

Ma-RC wengine wa Mkoa wa Kigoma ni Brigedia Jenerali Emmanuel Maganga, Luteni Kanali Issa Machibya na Kanali Joseph Simbakalia.

Waliowahi kuwa ma-DC kwenye mkoa huo walikuwa Kanali Isaac Mwakisu (Kasulu), Kanali Simon Anange (Kasulu), Kanali Michael Ngayalina (Buhigwe), Kanali Evance Balama (Uvinza), Luteni Kanali Hanafi Mshery (Kibondo), Kanali Aggrey Magwaza (Kibondo), Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Advera Bulimba (Kibondo), Kanali Marco Guti (Kasulu) na Kanali Paschal Njiru       (Kakonko).

Mkoa wa Ruvuma unapakana na nchi ya Msumbiji upande wa kusini. Huu ndio mpaka mrefu zaidi wa mkoa huu, ukitenganishwa na Mto Ruvuma kuanzia wilaya ya Tunduru, Namtumbo hadi Nyasa.

Pia, mkoa huo unapakana na nchi ya Malawi upande wa magharibi. Mpaka huu upo ndani ya Ziwa Nyasa, ukitenganisha wilaya ya Nyasa na nchi ya Malawi.

Katika Mkoa wa Ruvuma ma-RC maaskari waliowahi kuongoza ni Kanali Abbas Ahmed Abbas, Kanali Laban Thomas na Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge.

Pia, wilaya za Mkoa wa Ruvuma nazo zimekuwa na maaskari, Wilaya ya Nyasa inayopakana nan chi ya Malawi ni wilaya ya kimkakati kwa sababu ya Ziwa Nyasa na mpaka wa maji.

Wilaya Nyasa iliongoza na ma-DC, Kanali Laban Thomas, Kanali Evance Balama. Wilaya ya Tunduru inayopakana nan chi ya Msumbiji, yenye changamoto za ujangili na usalama wa mpaka wa Mto Ruvuma.

Tunduru iliongozwa na Kanali Denis Mwila. Pia,   Luteni Kanali Simon Gofia amewahi kuhudumu katika mikoa ya kusini ikiwemo Ruvuma/Mtwara katika nafasi za ukuu wa wilaya.

Dk Hamisi Kondo, mchambuzi wa masuala ya ulinzi, anasema mikoa hiyo ipo katika ukanda unaogusa moja kwa moja mipaka ya kimataifa, hivyo inabeba changamoto za usalama wa taifa.

Anasema Kagera inapakana na Uganda, Rwanda na Burundi, Kigoma iko mpakani na Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Mtwara inapakana na Msumbiji, huku Ruvuma nayo ikiwa jirani wa Msumbiji.

Dk Kondo anaeleza historia ya migogoro ya kikanda, uhamiaji haramu, magendo ya silaha na changamoto za wakimbizi imeifanya Serikali kuona umuhimu wa viongozi wenye mafunzo ya kijeshi, wanaoelewa lugha ya operesheni, nidhamu na uamuzi wa haraka.

Anasisitiza kuwa mkuu wa mkoa katika maeneo hayo si usimamizi wa kiraia tu, bali kiungo muhimu kati ya vyombo vya usalama, Serikali Kuu na mamlaka za mitaa.

“Kiongozi aliyepitia mfumo wa kijeshi anaelewa mantiki ya utii wa amri, tathmini ya hatari na usiri wa taarifa, vitu ambavyo ni muhimu sana katika mikoa ya mipakani,” anaeleza.

Mchambuzi wa siasa na utawala wa umma Profesa Rehema Mwansasu, anasema tangu kuasisiwa kwa Taifa, Serikali imekuwa ikiangalia mikoa ya pembezoni kama nguzo zake za ulinzi wa mamlaka ya dola.

Kwa mantiki hiyo, amesema kuweka viongozi waliopitia vyombo vya ulinzi ni njia ya kuimarisha uwepo wa Serikali katika maeneo ambayo kihistoria yamekuwa mbali na kitovu cha maamuzi ya Taifa.

Ameeleza wakuu wa mikoa hao huonekana kama wawakilishi wa moja kwa moja wa Rais, wenye mamlaka ya kuhakikisha sera na maamuzi ya kitaifa yanatekelezwa.

“Hii siyo hofu ya wananchi, bali ni dhana ya dola kujihakikishia uthabiti wake katika maeneo yenye changamoto za kijiografia na kihistoria,” ameeleza.

Mchambuzi huo amesema uteuzi wa wanajeshi au maofisa wa usalama si bahati mbaya, ni mkakati wa kisiasa wa kudhibiti mazingira ambayo yakiachwa bila uangalizi yanaweza kuwa chanzo cha misukosuko.

Mbali na usalama, Mchambuzi wa siasa, Mussa Nyange, amesema mikoa hiyo imekuwa ikikumbwa na changamoto za kiutendaji zinazohitaji viongozi wenye uthubutu na uwezo wa kusimamia mifumo migumu.

Ameeleza Kigoma na Ruvuma, zimekuwa zikikabiliwa na changamoto za miundombinu, biashara za mipakani zisizo rasmi na uratibu wa shughuli za wakimbizi na wafanyabiashara wadogowadogo.

Amesema viongozi waliotoka jeshini mara nyingi huja na mtazamo wa utekelezaji kwanza, wakisisitiza ratiba, uwajibikaji na ufuatiliaji wa karibu.

“Katika maeneo ambayo urasimu umekuwa ukikwamisha maendeleo, kiongozi mwenye misingi ya kijeshi huonekana kama mtu anayevunja mazoea,” amesema Nyange.

Hata hivyo, amekiri kuwa mtazamo huo una changamoto zake, hasa pale unapokosa mizania kati ya nidhamu na ushirikishwaji wa wananchi.

Pia, amesema mikoa hiyo imewahi kupitia vipindi vya taharuki, ama migogoro ya wakimbizi Kagera na Kigoma, au changamoto za kiusalama Mtwara zinazohusishwa na ukaribu wake na Msumbiji.

Katika mazingira hayo, amesema jamii mara nyingi huanza kuizoea mamlaka yenye sura ya ulinzi na Serikali hujenga imani kwamba uwepo wa kiongozi wa aina hiyo utaleta utulivu.

Kwa upande wa Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Conrad Masabo amesema zipo sababu za kikoloni zilizojificha katika utaratibu huo.

Katika ufafanuzi wake, mwanazuoni huyo anasema mikoa ambayo mara nyingi wanateuliwa askari kuiongoza, imepakana na nchi ambazo kulikuwa na ugumu wa kuingiliana enzi za ukoloni.

Anaeleza baada ya vita vya kwanza vya dunia, Rwanda na Burundi zilizokuwa koloni la Ujerumani zikawa chini ya Ubelgiji, huku Kenya Uganda na Tanganyika zikawa chini ya Uingereza.

Aina ya hiyo ya wakoloni, anasema ilitengeneza ugumu kwa Tanganyika kuingiliana na Rwanda na Burundi, lakini ilikuwa rahisi Mtanganyika kuingia Kenya na Uganda.

Mazingira hayo, anasema yalisababisha kuimarishwe ulinzi mipakani, jambo lililoendelea hadi sasa.

Hata hivyo, anasema hakuna utofauti wowote kati ya mkuu wa mkoa askari na raia, kwa sababu wote wanatekeleza jukumu moja na hakuna mwenye mamlaka ya kutoa amri ya kijeshi zaidi ya ile ya uenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama.

“Haina tija kwa sababu hata ukimweka raia akawa Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama hizo taarifa zitapelekwa kwenye kambi za jeshi.

“Akishakua Mkuu wa Mkoa wa kijeshi ataweza kutoa amri ya kijeshi? Ataishia kutoa amri kulingana na wadhifa wake wa mkuu wa mkoa,” anasema.