Siku 100 za Rais Samia bila maridhiano, Katiba mpya

Wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu 2025, Rais Samia Suluhu Hassan aliahidi kuunda Tume ya Maridhiano na kuanzisha mchakato wa Katiba mpya ndani ya siku 100 za utawala wake, watanzania wanatamani kusikia kauli yake mpya.

Kwa watanzania wa aina yangu, tunaelewa kuwa ndoto hii ya Rais Samia na Chama chake cha Mapinduzi (CCM), tunaelewa vurugu za uchaguzi mkuu Oktoba 29 na siku zilizofuata, pengine ndio hasa zilivuruga kabisa ahadi hizi za Rais.

Rais Samia aliapishwa kushika wadhifa huo kwa mhula wa pili Novemba 3,2025 baada ya kuibuka na ushindi wa kura 31.9 milioni kati ya kura 32.6 milioni zilizopigwa sawa na asilimia 97.66 na kuvunja rekodi ya marais waliomtangulia.

Uchaguzi huo wa Rais, wabunge na madiwani uligubikwa na vurugu zilizotokana na maandamano yasiyo na baraka za Polisi na kusababisha mauaji vurugu zilizosababisha mauaji ya raia wasio na hatia, uporaji na uharibifu wa mali.

Lakini kabla ya siku hiyo, katika kampeni zake za kuomba watanzania wampe ridhaa ya kuliongoza taifa la Tanzania kwa mhula wa mwisho, Rais Samia aliahidi mambo makubwa mawili ndani ya siku 100 nayo ni maridhiano na Katiba mpya.

Hata alipolihutubia Bunge Novemba 14,2025, Rais Samia alisisitiza dhamira yake akisema moja ya mambo ambayo Serikali yake itafanya ndani ya siku 100 ni marekebisho ya Katiba kwa kuanza na Tume ya Usuluhishi na Maridhiano.

Dhamira hii ilionekana pia alipoukaribisha mwaka 2026 kwa wito wa mshikamano, maridhiano ya dhati na kuimarisha ustawi wa wananchi, akisisitiza kuwa taifa linahitaji uponyaji wa pamoja baada ya kipindi kigumu cha kisiasa na kijamii.

Akihutubia taifa kutoka Tunguu, Zanzibar, Rais  alisema serikali imeanza rasmi maandalizi ya kuunda Tume ya Maridhiano ya Kitaifa itakayoshirikisha  wadau wote muhimu nchini ili kukubaliana muundo, majukumu na utekelezaji wake.

Japokuwa waswahili wanasema ahadi ni deni na kwamba ilani ni mkataba kati ya watawala na watawaliwa, leo Rais Samia anapofikisha siku 100 madarakani, ni wazi kwa yaliyotokea Oktoba 29 yanaweza kuwa yamevuruga mipango yake.

Hakuna anayekataa kwamba kabla ya Oktoba 29,2025, ahadi ya Rais ilikuwa ni kuunda Tume ya Maridhiano na kuanzisha mchakato wa Katiba mpya ndani ya siku 100 za utawala wake, na kila mtanzania mwenye akili timamu aliunga mkono hili.

Ni kwa sababu mambo hayo mawili yanatarajiwa kuituliza nchi kutokana na hali za kisiasa ambazo nchi imepitia na kuacha majeraha ambayo yameibua chuki na roho za visasi dhidi ya Serikali ya CCM kiasi kwamba watu wanaombeana mabaya.

Katiba mpya ingetufanya tuwe na taasisi imara na zilizo huru kama Bunge, Mahakama, Polisi na vyombo vingine wala huu ukamataji holela na utekaji na watu kukamatwa ambao umechochea chuki ungedhibitiwa na sheria mama.

Ni Katiba mpya ambayo itasaidia kuzaliwa kwa mtoto anaitwa “Tume Huru ya Uchaguzi”, ambayo ni huru kweli sio kubadili jina, bali hadi muundo ili sasa isimamie chaguzi ambazo zitakuwa za kweli, huru na zinazoaminika na kukubalika.

Tume ya Maridhiano aliyoahidi Rais Samia ndani ya siku 100 ni muhimu kama mgonjwa na uji kwa sababu taifa limegawanyika, upendo na utu unayeyuka mithili ya barafu na mahusiano ya watawala na watawaliwa yametawaliwa na mashaka.

Kauli za baadhi ya viongozi wetu wa juu wa Serikali juu ya kilichotokea Oktoba 29,2025 zinazidi kutonesha majeraha badala ya kuponya kwa sababu hakuna anayetaka kukubali kuwa kuna mahali Serikali na vyombo vyake viliteleza.

Ni kweli Rais anasubiri ripoti ya Tume aliyoiunda kuchunguza na kubainisha chanzo halisi cha ghasia zilizotokea Oktoba 29 chini ya Jaji Mkuu mstaafu, Mohamed Chande Othmani, licha ya upinzani mkali juu ya wajumbe wanaounda Tume.

Kwa hiyo ili Rais aendelee na kuunda Tume ya Maridhiano, basi ni lazima apokee kwanza ripoti hii ya Tume ambayo japo imepata ushuhuda na maoni ya baadhi ya watanzania, ukweli ni kwamba wengi wamesita kujitokeza mbele ya Tume.

Ninatamani, nasema ninatamani, moja ya mapendekezo ya Tume hii yawe kuitaka Serikali na vyombo vyake kukiri kuna mahali walikosea, kuomba radhi, kulipa fidia waathirika na kuwawajibisha watakaoonekana walitenda nje ya sheria.

Hii ni kwa sababu na hata Tume ya Jaji Othman imethibitisha hili kwa kusikiliza simulizi za mashuhuda na waathirika, kwamba miongoni mwa waliouawa kikatili kwa kupigwa risasi za kichwa au kifua au kujeruhiwa, hawakuwa wanaandamana.

Wapo waliuawa wakiwa majumbani na familia zao, wapo waliouawa wanatizama mpira, wapo waliouawa wakitafuta usafiri, wapo waliouawa wakirejea nyumbani na wapo waliouawa wakiwa kazini, si sawa kuwaweka kundi la waandamanaji.

Hata kama waliouawa na kujeruhiwa na baadhi walikuwa raia wa nje kama tulivyoaminishwa, lakini walistahili kuuawa?Hivi ilikuwa ni lazima tuanze na risasi za moto? Magari ya washawasha yalikuwa wapi, mabomu na hata risasi za mpira.

Ninaamini yote haya Tume ya Jaji Othman itakuja na majibu kwa sababu moja ya hadidu za rejea ni kuchunguza mazingira na hatua zilizochukuliwa katika kubaini na kukabiliana  ghasia zilizojitokeza Oktoba 29,2025 na baada ya uchaguzi.

Katika kipindi hiki tukisubiri ripoti ya Tume itakayomwezesha Rais kuunda Tume ya Usuluhishi na Maridhiano, viongozi wetu na kila mtu waache kutoa kauli zinazotonesha majeraha ya Oktoba 29 kwa kutupa lawama badala ya kuponya.

Lakini katika kipindi hiki pia, Jeshi letu la Polisi liache kufanya ukamataji ambao uko nje ya misingi ya kisheria na kuibua taharuki ya utekaji ambayo ni moja kati ya viini na chuki vilivyotufikisha katika ghasia zile za siku ya uchaguzi Oktoba 29.

Washukiwa wa makosa ya jinai, tena wengine wana anuani (address), wanakamatwa kihuni, hawapewi haki za kuwasiliana na wakili au ndugu, wanafichwa katika vituo havijulikani na wanashikiliwa zaidi ya saa 24 za kisheria.

Kwa hiyo tunapotafakari siku 100 za Rais Samia madarakani, tutafakari pia mwenendo wa Jeshi letu la Polisi kama unachangia kuliponya taifa au kutonesha majeraha maana wao ndio wananyooshewa kidole na chuki zilizotamalaki nchini.

Kanuni kubwa kabisa katika kutafuta maridhiano ni kukiri na kukubali makosa na wala kufanya hivi si udhaifu, kwani kunafanya yule uliyemkosea aone kweli unajutia (remorse) kile ulichomfanyia ili sasa arejeshe moyo na kusamehe.

Lakini tukiendelea kuwa katika “state of denial” (kuukataa ukweli) wakati watanzania wa leo wa kizazi cha digitali wanafahamu kila kilichotendeka, ni kutatua matatizo yetu kwa kujifanya kama hayapo kama Nyerere alivyosema.

Ninampongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kukiri kuna tatizo ndio maana akaunda Tume kuchunguza vurugu hizo za Oktoba 29, lakini kuna kauli zinaendelea kutolewa ambazo zinaondoa kabisa maana na umuhimu wa Tume.

Lakini natamani Rais aunde Tume ya Ukweli na Maridhiano (TRC) kama iliyoundwa Afrika Kusini hasa tukimnukuu Askofu Desmond Tutu akisema “Without truth, there can be no reconciliation”, akimaanisha bila ukweli hakuna maridhiano.

Nafahamu Rais anasubiri ripoti ya Tume aliyoiunda kuchunguza vurugu za Oktoba 29 ikiongozwa na Jaji mkuu mstaafu Othman Chande, ni muhimu tume hiyo ikatoa sura ya maridhiano ya kweli na isibue maswali na hisia hasi kwa wananchi.

Turidhiane bila kuficha mapanga nyuma, hatutatoboa na nimsihi sana Rais Samia, akemee propaganda za makada uchwara wa CCM na baadhi ya viongozi wa Dini na waumini, wanaotumika kuleta propaganda na mgawanyiko badala ya kuponya.

Huu si wakati wa kuleta propaganda kushambulia vyama vya upinzani hasa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wakati tunawafahamu waliohamasisha kilichotokea Oktoba 29 kupitia mitandao ya Kijamii. Tufungue ukurasa mpya.

Ninaamini, mvumilivu hula mbivu, ni kweli leo ni siku 100 za ahadi ya Tume ya Maridhiano na kuanza kwa mchakato wa Katiba mpya, hebu tukubali kuwa bila kujua nini hasa kilitokea Oktoba 29 hadi idadi ya vifo, tutaridhiana nini.