Sintofahamu siku 90 za SUK Zanzibar, mazungumzo yanaendelea

Dar es Salaam. Wakati jana Jumanne, Februari 10, 2026 zikitimia siku 90 za mwelekeo wa kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) Zanzibar, bado hatima ya mchakato huo haijawekwa wazi.

Katikati ya hali hiyo, Chama cha ACT Wazalendo kimesema mazungumzo na Chama cha Mapinduzi (CCM) yanaendelea vizuri na yamefikia hatua muhimu, huku wananchi wakiahidiwa kupewa taarifa rasmi mara taratibu za ndani zitakapokamilika.

Akizungumza leo Jumatano, Februari 11, 2026 akiwa ziarani Pemba, Makamu wa Kwanza wa Rais wa zamani na mgombea urais wa Zanzibar kupitia ACT Wazalendo katika uchaguzi wa Oktoba 29, 2025, Othman Masoud, amesema lengo la mazungumzo hayo ni kufikia mwafaka wa kudumu wa kisiasa.

“Baada ya uchaguzi, ACT Wazalendo kilishiriki mazungumzo ya kisiasa kutafuta mwafaka wa kudumu Zanzibar. Yamefikia hatua muhimu na ndani ya muda mfupi ujao wananchi watajulishwa rasmi yaliyofikiwa,” amesema Othman mbele ya wanachama wa Chake Chake na Mkoa wa Kusini Pemba.

Amesisitiza kuwa mazungumzo hayo yanalenga kurejesha imani ya wananchi kwa mchakato wa kidemokrasia, akieleza kuwa demokrasia haiwezi kusimama bila wananchi kuwa na imani na uchaguzi.

Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, Othman Masoud akizungumza na wanachama na viongozi wa chama wa mkoa wa Kusini Pemba kuhusu mwenendo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ( SUK). 



Katika uchaguzi huo, ACT Wazalendo ilidai kulikuwa na dosari. Othman alipata kura 139,399 (asilimia 23.22), akitanguliwa na Dk Hussein Mwinyi wa CCM aliyepata kura 448,892.

Kwa mujibu wa Othman, mazungumzo hayo yanaongozwa na yeye pamoja na mwenyekiti mstaafu wa ACT Wazalendo, Juma Duni Haji, huku upande wa CCM ukiongozwa na marais wastaafu Amani Abeid Karume na Dk Ali Mohamed Shein.

Kwa upande wake, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Zanzibar, Khamis Mbeto, amesema suala la SUK lipo kikatiba na mazungumzo yanaendelea, ingawa hakutaja kwa sasa nani anaongoza majadiliano kwa upande wa CCM.

Msingi wa siku 90 ulitokana na kauli ya Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, aliyotoa Novemba 13, 2025 akieleza kuwa kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar, chama cha upinzani kilichopata uwakilishi Baraza la Wawakilishi kinastahili nafasi katika Baraza la Mawaziri.

Kwa kuwa ACT Wazalendo ilipata viti 10 kati ya majimbo 50, hesabu hiyo ilitoa nafasi nne katika Baraza la Mawaziri. Dk Mwinyi alisema aliziacha wazi nafasi hizo kwa siku 90 akisubiri uamuzi wa ACT kuhusu kujiunga na SUK.

Hata hivyo, Mwanasheria Mkuu wa ACT Wazalendo, Omar Said Shaaban, alisema Katiba haijaweka shinikizo la lazima ndani ya siku hizo 90. Akifafanua Ibara ya 42(A) ya Katiba ya Zanzibar, amesema kifungu hicho kinahusu kujaza nafasi iwapo viongozi wa SUK watajiuzulu au kushindwa kutekeleza majukumu yao, si kuilazimisha SUK kuundwa ndani ya muda huo.

Hivyo, pamoja na kutimia kwa siku 90, hatima ya SUK Zanzibar bado inasubiri hitimisho la mazungumzo ya kisiasa kati ya pande husika.