WAKATI Yanga ikisaliwa na dakika 90 za kujitetea ili kutinga hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, wapinzani wao katika mchezo huo, JS Kabylie wako tumbo joto wakihofia mchezo huo, huku mmoja wa mastaa wa kikosi hicho akitoboa kile wanachofia.
Mchezo kati ya timu hizo unaopigwa Zanzibar, wikiendi hii ndiyo utakaokuwa wa mwisho wa kundi B linalohusisha timu zingine mbili ambazo ni FAR Rabat na Al Ahly.
Akizungumza na Mwanaspoti, kiungo wa zamani wa Simba anayeichezea JS Kabylie, Babacar Sarr amesema wanakuja kucheza mchezo mgumu dhidi ya Yanga ambayo inafanya vizuri hasa inapocheza nyumbani.
Sarr aliichezea Simba msimu wa 2024/25 akitumikia kikosi hicho chini ya kocha Mualgeria Abdelhak Benchikha, lakini hakudumu kwa muda mrefu kwani alicheza kwa miezi sita pekee.
Amesema Yanga ina timu nzuri na hesabu wanayokuja nayo ni kuhakikisha kwamba wanawazuia viungo wake ambao ni wabunifu wanapokabiliana na wale wa timu pinzani.
Sarr alibainisha kuwa bahati mbaya kwao ni kwamba mchezo utachezwa Zanzibar, hivyo waamini kwamba watakosa msaada wa mashabiki wa Simba ambao walitarajia kwamba wangekuwa upande wao.
“Kama kuna jambo gumu kwetu kwa sasa ni mechi dhidi ya Yanga. Itakuwa ya mwisho, lakini yenye upinzani wa tofauti sana, na wote tunahitaji kupata pointi tatu muhimu,” amesema mchezaji huyo akionyesha kwamba chama lake haliji tu nchini likiwa na fikra za kupoteza mchezo huo.
Mchezaji huyo aliongeza kwamba Yanga ina mastaa wenye ubora na uzoefu mkubwa kwenye michuano ya ndani na kimataifa.
Sarr amesema siyo mara ya kwanza kwa Yanga kucheza mashindano ya klabu ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF), hivyo inajua jinsi ya kucheza mechi ngumu za kuamua hatma ya timu hata pale inapokuwa inapitia kipindi kigumu.
“Yanga ina mastaa wenye ubora na uzoefu mkubwa hasa kwenye michuano ya kimataifa, kwani siyo mara yao ya kwanza kushiriki, hivyo wanajua jinsi ya kucheza mechi ngumu za kuamua hatma ya timu,” amesema mchezaji huyo aliyeondoka Simba akiwa haimbwi, lakini akajikuta alamba dili katika timu hiyo yenye historia kubwa Algeria.
Katika hatua nyingine, Sarr alizungumzia kile ambacho mastaa wanakifanya kwa sasa ikiwa ni njia mojawapo ya kusaka ushindi katika mchezo huo.
Amesema benchi la ufundi la timu yao limewapa kazi maalumu ya kuhakikisha viungo wa Yanga hawapati nafasi ya kuanzisha mashambulizi ili kupunguza uwezekano wa kufungwa kwa urahisi.
“Tumepewa kazi moja tu ya kupambana na viungo na eneo la mbele kwa ujumla. Ni vigumu kuwadhibiti, kwani nafasi hizo zinachezwa na mastaa ambao baadhi yao nawafahamu vyema,” amesema mchezaji huyo akisisitiza licha ya ugumu, lakini watakabiliana nao.
Aliongeza kwamba dakika 90 ndizo zitaamua timu ipi itaibuka na ushindi, kwani wanaingia kwenye mchezo huo bila kutazama matokeo yaliyopita.
“Dakika 90 zitaamua ni nani itaibuka na ushindi. Kwa sasa tunaingia kwenye mchezo huu bila kutazama matokeo yaliyopita ili kupata nguvu zaidi,” amesema.
JS Kabylie ilitoka suluhu na Yanga ikiwa nyumbani kwao, Novemba 28, 2025. Timu hizo zote zipo Kundi B katika michuano hiyo, zikiwa pamoja na Al Ahly ya Misri ambao ni vinara na FAR Rabat ya Morocco inayoshika nafasi ya pili ambazo zitakutana huko Misri.