Kahama. Katika harakati za kudumisha usalama wa wananchi na mali zao, Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga limewataka jeshi la jadi, sungusungu pamoja na wananchi kushirikiana na jeshi hilo katika kudhibiti uhalifu.
Hayo yamesemwa leo Februari 11, 2026 na Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga, Janeth Magomi wakati akizungumza na wananchi wa kata ya Lunguya iliyopo Halmashauri ya Msalala, mkoani Shinyanga.
“Sungusungu ni wadau muhimu katika kuhakikisha usalama katika jamii, lakini mnapaswa kufanya kazi yenu kwa kuzingatia sheria, taratibu na kushirikiana kwa karibu na Jeshi la Polisi na kuepuka kujichukulia sheria mkononi,” amesema Magomi.
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga, Janeth Magomi akizungumza na Jeshi la jadi, Sungusungu pamoja na wananchi wa kata ya Lugunya iliyopo Halmashauri ya Msalala wilayani Kahama mkoani Shinyanga.
Pia ameongeza kuwa, “Tunawahimiza wananchi kutoa taarifa za uhalifu mapema, kushirikiana na sungusungu na polisi, na kuepuka kuwaficha wahalifu kwani kufanya hivyo kunahatarisha usalama wa jamii nzima,” ameongeza Magomi.
Kwa upande mwingine amesisitiza kuwa usalama ni jukumu la kila mmoja na Jeshi la polisi haliwezi kufanya kazi hiyo peke yake bila ushirikiano wa wananchi pamoja na vikundi vya ulinzi shirikishi kama sungusungu.
Baadhi ya wananchi wa kata ya Lugunya iliyopo Halmashauri ya Msalala wilayani Kahama mkoani Shinyanga, wakimsikiliza kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga, Janeth Magomi.
Mkazi wa Lunguya, Kazimili Lushinge ameeleza kuwa wahalifu hawatoki maeneo ya mbali bali ni watu wanaoishi nao na kuna watu wanawakingia kifua na kuwafichia maovu yao ni bora kutoa taarifa mapema kuliko kulea maovu,
“Wahalifu hawatoki mbali tunaishi nao humuhumu kama hatuwezi kuwaonya kuacha uhalifu, basi tutoe taarifa kwa mamlaka husika kushughulika nao maana tunarudishana nyuma kimaendeleo” amesema Lushinge.