TANZANIA YALENGA ASILIMIA 51 YA WANAWAKE KATIKA SAYANS

……………

Na Carlos Claudio, Dodoma.

Serikali imesisitiza dhamira yake ya kuendelea kuwekeza katika elimu ya sayansi ili kukidhi mahitaji ya soko la ajira na kasi ya ukuaji wa teknolojia duniani, huku ikiweka mkazo maalum katika kuongeza ushiriki wa wanawake na wasichana katika sekta hiyo.

Akizungumza Februari 11, 2026 jijini Dodoma wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake na Wasichana katika Sayansi, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amesema sayansi ni mhimili muhimu wa maendeleo ya taifa kiuchumi na kijamii.

Profesa Mkenda amesema kuwa maendeleo ya sayansi yanaonekana wazi katika sekta mbalimbali, hususan afya, ambapo teknolojia za kisasa zimewezesha utoaji wa huduma za kibingwa hapa nchini. Ametolea mfano Hospitali ya Benjamin Mkapa, akisema kwa sasa wagonjwa wenye matatizo ya figo wanaweza kupandikizwa figo na kuendelea kuishi maisha ya kawaida, jambo linaloonesha hatua kubwa ya kisayansi iliyofikiwa.

“Takwimu zinaonesha kuwa takribani asilimia 36 ya wataalamu wa sayansi duniani ni wanawake. Tanzania tunalenga kufikia angalau asilimia 51 ya ushiriki wa wanawake katika sayansi,” amesema Profesa Mkenda.

Ameeleza kuwa Serikali inaendelea kupanua fursa za elimu ya sayansi kupitia ufadhili wa masomo chini ya programu ya Samia Scholarship, pamoja na kuhamasisha wanafunzi kusoma masomo ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati (STEM). Lengo ni kuwa na wanasayansi wa kutosha na wenye ubora katika sekta zote muhimu za maendeleo.

Aidha, Waziri huyo amesema Serikali inawekeza katika kuboresha miundombinu ya elimu ya sayansi, ikiwemo maabara, vifaa vya kisasa na mazingira rafiki ya kujifunzia ili kuendana na ushindani wa kimataifa katika uchumi wa maarifa.

Maadhimisho ya mwaka 2026 yameenda sambamba na uzinduzi wa kampeni ya “Africa Educate Her” nchini Tanzania, inayolenga kuongeza upatikanaji wa elimu kwa wasichana na kuwapa fursa sawa za kujifunza, kubuni na kufanikiwa katika taaluma za sayansi.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhandisi Mary Prisca Mahundi, amesema wizara yake itaendelea kuboresha sera na mikakati ya kuwawezesha wanawake na wasichana kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya sayansi, huku akisisitiza umuhimu wa malezi bora yanayowajengea watoto wa kike misingi imara ya elimu.

Awali, akizungumza kwa niaba ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo, Mbunge wa Jimbo la Msalala, Mabula Magangila, amesema kamati hiyo inaendelea kushuhudia mabadiliko chanya katika sekta ya elimu, akibainisha kuwa mtoto wa kike kusoma sayansi ni fursa si tu kwa familia bali kwa taifa zima, kwa kuwa mwanamke ni mlezi na nguzo muhimu ya jamii.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu kutoka Wizara ya Elimu, Profesa Ladislaus Mnyone, amesisitiza umuhimu wa kuwekeza zaidi katika tafiti na ubunifu unaowashirikisha wanawake na wasichana ili kuongeza ushindani wa Tanzania katika uchumi wa maarifa unaokua kwa kasi duniani.

Maadhimisho hayo yamebeba ujumbe wa kuhamasisha jamii kuunga mkono ushiriki wa wanawake na wasichana katika sayansi, ikiwa ni hatua muhimu ya kufikia maendeleo jumuishi na endelevu.