UCHAMBUZI WA MALOTO: Siku 100 zinavyotofautisha mihula miwili ya Rais Samia

Julai 24, 1933, Rais wa 32 wa Marekani, Franklin Delano Roosevelt ‘FDR’, alihutubia umma wa taifa lake na kueleza kipimo cha siku 100 tangu alipoingia madarakani. Siku 100 za FDR zilitimia Juni 11, 1933. Aliapishwa kuwa Rais, Machi 4, 1933.

FDR aliingia ofisini akiikuta nchi ikiteswa na mdororo mkubwa wa kiuchumi (Great Depression). Hali hiyo ilisababishwa na anguko la uchumi wa viwanda kwenye nchi za Magharibi.

Katika kuikabili Great Depression, FDR alianzisha kampeni aliyoiita New Deal (Dili Mpya) ambayo utekelezaji wake aliugawa katika mpango alioupa jina la R tatu (3 Rs).

R hizo zilikuwa na maana ya Relief (Nafuu) kwa wasio na ajira pamoja na maskini. Recovery (Uhuishaji) wa uchumi mpaka kufikia kiwango cha kawaida. Reform (Mageuzi) ya mfumo wa kifedha na kudhibiti kutojirudia kwa msukosuko wa uchumi wa viwanda.

Kufikia malengo hayo, FDR ndani ya siku 100, aliliita Bunge la Marekani (Congress), chemba zote mbili, Baraza la Wawakilishi na Seneti. Kisha, miswada 15 ikapitishwa na sheria mpya 76 zikatungwa ili kuwezesha matokeo yaliyokusudiwa.

Ni kuanzia hapo, siku 100 za mwanzo ofisini, zimekuwa kipimo cha awali cha uelekeo wa nchi baada ya Serikali mpya kuingia madarakani. Kutoka nchi kwa nchi, serikali hadi serikali, tathmini ya siku 100 hujenga sura ya aina ya uongozi kabla hata ya kupitisha bajeti ya kwanza. Kipindi cha kampeni, wagombea hujinadi kwa ilani, ahadi za jumla, na ahadi za siku 100.

Juni 27, 2021, Rais Samia Suluhu Hassan, alimitiza siku 100 tangu alipoingia madarakani muhula wake wa kwanza ulioanza Machi 19, 2021. Leo, Februari 11, 2026, ni siku ya 100 tangu Rais Samia alipokula kiapo kuongoza muhula wake wa pili ulioanza Novemba 3, 2025. Tofauti ya nyakati ndiyo msingi wa makala.

Juni 27, 2021, niliandika makala mbili ambazo zote zilichapwa na gazeti hili bora la Mwananchi. Ya kwanza niliipa kichwa “Siku 100 za tofauti ya urais na ufalme”. Ya pili ilibeba utambulisho “Siku 100 za uongozi wa usikivu, utu na uponyaji”. Dhahiri, makala hizo mbili zilitafsiri vema aina ya uongozi wa Rais.

Makala ya kwanza ilisimama na hoja kuwa siku 100 za muhula wa kwanza, Rais Samia alijipambanua kama kiongozi badala ya kuwa mtawala. Alijitofautisha na mtangulizi wake aliyetaka nguvu zake zidhihirike kwenye kila mhimili. Alifunika Bunge, akataka awe juu ya Mahakama.

Msingi wa makala ya pili ulikuwa kuchambua matendo aliyoyafanya Rais Samia ndani ya 100 za muhula wa kwanza. Kuwasamehe mashehe 36 wa Uamsho, waliokuwa mahabusu kwa takriban miaka nane. Onyo la kutotaka kodi za dhuluma. Agizo kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kufuta kesi zote za kubambikia watu. Takukuru wakafuta kesi 47 za ubambikiaji.

Tofauti namba moja ya siku 100 za mihula miwili ya Rais Samia ni kuwa muhula wa kwanza hakuwa na ahadi za kutekeleza, isipokuwa ulibeba Ilani ya CCM na kutembea nayo. Aliingia madarakani kikatiba baada ya mtangulizi wake, Dk John Magufuli, kufariki dunia akiwa ametimiza siku 132 tangu alipoapa kuongoza muhula wake wa pili.

Siku 100 za muhula wa pili wa Rais Samia zina madeni. Alikuwa mbeba bendera ya CCM Uchaguzi Mkuu 2025. Kuna mambo aliahidi na ametekeleza, mathalan, ajira 12,000 alizoahidi kwa mgawanyo walimu 7,000 na watumishi wa sekta ya afya 5,000, hizi tayari zilishatolewa. Kuna marufuku ya maiti kuzuiwa hospitali sababu ya madeni ya ankara za matibabu, hili agizo lilishatolewa.

Aliahidi bima ya afya kwa wote na majaribio yameanza. Ahadi nyingine za siku 100 zilikuwa kuunda tume ya maridhiano, vilevile kuanza kwa mchakato wa katiba mpya. Novemba 14, 2025, Rais Samia alipohutubia Bunge la 13, kwa ajili ya kulizindua, alisema mambo ya katiba na tume, yatasubiri Tume ya Uchunguzi wa kadhia ya Oktoba 29, 2025. Hayo ni madeni.

Siku 100 za muhula wa kwanza wa Rais Samia, zilibeba matumaini makubwa kwa wananchi wa makundi yote. Wafanyabiashara walipata matumaini, wanasiasa waliiona nyota njema, waliodhulumiwa uhuru wao waliziona siku njema. Wafaanyakazi waliokaa miaka sita bila nyongeza ya mishahara na kuoandishwa madaraja, walipata mwangaza. Siku 100 za muhula wa pili wa Rais Samia zipo kwenye hali tata.

Taifa linasubiri hatima ya kadhia ya Oktoba 29, 2025. Watu waliopoteza maisha, majeruhi, mali zilizoharibiwa na kuibwa. Taifa lina mgawanyiko mkubwa. Muhula wa pili wa Rais Samia, kuna watu hawazungumzi lugha ya Kitanzania. Maoni ya mitandaoni imejaa uasi. Wapo walioomba Marekani iivamie Tanzania, na Donald Trump ashike dola. Mawazo ya kutukuza ukoloni baada ya miaka 64 ya uhuru.

Siku 100 za muhula wa pili wa Rais Samia, mitandaoni kuna vuguvugu la kuidai Tanganyika. Lugha hatari kwa Muungano. Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar (Tanzani), inakaribia kutimiza miaka 62. Katika hiyo, zaidi ya miaka 46, imeongozwa na marais kutoka Tanganyika. Chini ya miaka 16 ambayo haitimii ni chini ya marais Wazanzibari.

Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, miaka 21 na miezi mitano, Rais wa tatu Benjamin Mkapa na Rais wa Nne, Jakaya Kikwete miaka 20. Rais wa Tano, Magufuli, miaka mitano na miezi minne. Wote hao ni Watanganyika. Rais wa Pili, Ali Hassan Mwinyi, miaka 10, na sasa Rais Samia hata miaka mitano hajatimiza.

Hapohapo, wapo watu hukosoa Mwinyi kuitwa Mzanzibari. Asili yake Tanganyika, Mkuranga, Pwani. Alipelekwa Zanzibar akiwa mtoto, akasoma, akaoa Zanzibar, akajenga familia Zanzibar, akaitumikia Zanzibar tangu ukoloni na hata baada ya Mapinduzi, kisha akawq Rais wa Zanzibar. Historia ya Mwinyi inampambanua kama Mzanzibari zaidi kuliko Mtanganyika.

Leo, Rais Samia akiwa ametimiza siku 100 za muhula wake wa pili, hali ya nchi inatoa maelekezo ya kazi kubwa kufanyika. Rushwa ni tatizo kubwa na linavunja nyoyo za wazalendo, hamasa za mitandaoni zinachochea chuki ya Muungano. Taifa linahitaji tiba.