Ukaguzi, usajili na uteuzi maofisa ulinzi taarifa binafsi mbioni kuanza

Mbeya. Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) imetangaza kuwa inatarajia kuanza ukaguzi wa uzingatiaji wa sheria kwa kufuatilia utekelezaji wa maagizo ya usajili na uteuzi wa maofisa ulinzi wa taarifa binafsi, pamoja na kuchukua hatua za kisheria pale ukiukwaji utakapobainika.

Akizungumza Februari 11, 2026 jijini Mbeya wakati wa ufunguzi wa semina kwa maofisa ulinzi wa taarifa binafsi, Mkurugenzi Mkuu wa tume hiyo, Dk Emanuel Mkilia, amesema

Tume imejipanga kuhakikisha sheria ya ulinzi wa taarifa binafsi inatekelezwa kikamilifu kwa vitendo, ikiwa ni pamoja na kufuatilia taasisi ambazo hazijakamilisha taratibu za usajili na uteuzi wa maofisa husika.

“Ukaguzi huu unatarajiwa kuanza Aprili 9 mwaka huu,” amesema Dk Mkilia.

Aidha, ameeleza kuwa Tume itaendesha mafunzo, elimu na kampeni za uhamasishaji nchi nzima kwa taasisi za umma na binafsi ili kuhakikisha utekelezaji wa sheria unakuwa madhubuti na unaolinda masilahi ya wananchi.

Kwa mujibu wa Dk Mkilia, mafunzo hayo yanalenga kuimarisha uwezo wa taasisi katika kutekeleza Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, Sura ya 44, na kuhakikisha ukusanyaji, uchakataji, uhifadhi na matumizi ya taarifa binafsi vinafanyika kwa kuzingatia matakwa ya sheria, kanuni na viwango vya kitaaluma.

“Tunatarajia kuona mabadiliko ya vitendo ndani ya taasisi, kuimarika kwa mifumo ya udhibiti wa taarifa binafsi, kuongezeka kwa uwajibikaji na kupungua kwa vitendo vinavyokiuka faragha au kuhatarisha usalama wa taarifa za wananchi,” amesisitiza.

Maafisa Ulinzi wa Taarifa binafsi kutoka taasisi za umma na binafsi Nyanda za Juu Kusini wakiwa katika ushiriki wa mafunzo ya siku tatu yaliyoandaliwa na Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) yanayofanyika jijini Mbeya.



Akifungua mafunzo hayo, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Beno Malisa, ameshauri Tume hiyo kuhakikisha inaweka adhabu kali kwa wanaokiuka sheria, hasa wanaojihusisha na uvujishaji wa taarifa au faragha za watu kwa maslahi binafsi.

“Tunatamani kuona adhabu kali zinazolingana na madhara ya uvujishaji wa faragha za watu. Wapo wanaofanya kama biashara kuuza maudhui ya watu, jambo ambalo si sahihi. Lazima hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya wanaofanya hivyo,” amesema Malisa.

Kwa upande wao, washiriki wa mafunzo hayo wamesema yatawasaidia kuongeza uelewa na ufanisi katika kulinda taarifa binafsi katika maeneo yao ya kazi.

Adelin Kakoko, mmoja wa washiriki, amesema mafunzo hayo yamekuja wakati muafaka kwani yataongeza uelewa wa watumishi wa umma na binafsi kuhusu wajibu wao wa kisheria katika kulinda taarifa binafsi.

“Kwa sasa tumepata uelewa zaidi kuhusu utunzaji wa taarifa binafsi kwa kuzingatia sheria, taratibu na kanuni. Mafunzo haya yatatuongezea uwezo wa kubaini na kuziba mianya ya uvujishaji wa taarifa,” amesema Adelin.

Naye Ipyana Jengela amesema matarajio yao ni kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao na kuhakikisha taasisi wanazozitumikia zinafikia malengo kwa kuzingatia sheria na miongozo iliyopo.

“Tunatarajia kujifunza zaidi ili kuongeza uelewa na ufanisi katika kusaidia taasisi zetu kutekeleza majukumu kwa mujibu wa kanuni na miongozo. Mafunzo haya ni muhimu sana kwetu,” amesema Jengela.

Kwa ujumla, Tume imeweka bayana kuwa haitasita kuchukua hatua kwa taasisi au watu watakaokiuka sheria, huku ikisisitiza kuwa ulinzi wa taarifa binafsi ni msingi wa kulinda haki, faragha na usalama wa wananchi.