Dar es Salaam. Haieleweki upande wa Jamhuri ulipatwa na nini, lakini ni ukweli usiobishaniwa kuwa upungufu wa hati ya mashitaka kuhusu ni lini hasa Said Yeguku aliuawa, umesababisha washitakiwa watatu kuachiwa huru na mahakama.
Katika hati ya mashitaka, upande wa Jamhuri ulidai marehemu, ambaye alikuwa maarufu kwa jina la Digala, mkazi wa Nyamato, Kijiji cha Mkamba Kiu, wilaya ya Mkuranga, Mkoa wa Pwani, aliuawa Januari 8, 2024, lakini ushahidi ukawa tofauti.
Ni kutokana na dosari hiyo, Jaji Hussein Mtembwa wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, aliyesikiliza shauri hilo, hakuwa na jinsi nyingine zaidi ya kuwaachia huru washitakiwa Mwanahamisi Pingili, Said Makwega na Sophia Manyanzo.
Uamuzi wa kuwaachia huru washitakiwa hao ulitolewa na Jaji Mtembwa katika hukumu yake aliyoitoa Februari 9, 2026, na kuwekwa katika tovuti ya mahakama jana, Jumanne, Februari 10, akisema Jamhuri wameshindwa kuthibitisha shitaka hilo.
Kulingana na maelezo ya kosa hilo la mauaji ya kukusudia yaliyotolewa na upande wa Jamhuri, Yeguku na washitakiwa walikuwa wakiishi kama majirani eneo la Nyamato katika kijiji hicho cha Mkamba Kiu, wilaya ya Mkuranga.
Ilidaiwa marehemu alikuwa mteja wa grosari inayomilikiwa na mshitakiwa wa pili ambapo Januari 8, 2024, saa 8:00 usiku, akiwa amelala na mkewe, ghafla alisikia mlango wake ukigongwa na washitakiwa hao watatu.
Yeguku aliwafungulia mlango, ambapo alichukuliwa kwa nguvu na kupelekwa katika grosari ya mshitakiwa wa pili. Akiwa hapo, ilidaiwa washitakiwa hao watatu kwa pamoja walimshambulia kwa gongo sehemu mbalimbali za mwili.
Baadaye marehemu alifanikiwa kutoroka eneo hilo na kukimbilia katika nyumba ya shahidi wa pili wa Jamhuri, na ndipo mkewe, aliyekuwa shahidi wa kwanza, naye alifika na kumpeleka Hospitali ya Kilimahewa kwa matibabu.
Alitibiwa na kushauriwa arejee Januari 26, 2024 kwa ajili ya uchunguzi zaidi, lakini kwa bahati mbaya siku hiyo hiyo alifariki dunia na tukio hilo likaripotiwa polisi, ambapo Januari 29, 2024, shahidi wa tano aliufanyia uchunguzi mwili huo.
Uchunguzi ulibaini sababu ya kifo ni majeraha aliyoyapata kichwani baada ya kupigwa na kitu butu, ambapo washitakiwa walikamatwa na kufikishwa kortini na kukanusha katakata kumshambulia marehemu kama ilivyodaiwa na Jamhuri.
Katika usikilizwaji wa shauri hilo, upande wa Jamhuri uliwakilishwa na mawakili wa Serikali, Amina Macha na Doris Kauwonga, wakati washitakiwa walitetewa na mawakili Sadick Muhimbi, Neema Saruni, Mwajuma Issa na Hilda Mushi.
Pande zote hazikuwasilisha majumuisho
Jaji Mtembwa alisema ni jambo lililo katika kumbukumbu za mwenendo wa kesi kuwa baada ya kuhitimisha usikilizwaji wa mashahidi, mawakili wa pande mbili walitakiwa kuwasilisha majumuisho ya mwisho kabla ya Novemba 6, 2024.
Mahakama iliwataka mawakili wa pande mbili (Jamhuri na Utetezi) kutoa hoja mbele ya mahakama iwapo ilikuwa sahihi kwa hati ya mashitaka kueleza marehemu aliuawa Januari 8, wakati ushahidi unaonyesha ni Januari 26, 2024.
Hata hivyo, Jaji alisema kwa mshangao hakuna wakili hata mmoja aliyewasilisha majumuisho hayo ya mwisho kwa maandishi kama mahakama ilivyoamuru.
Kulingana na kumbukumbu za mahakama, majumuisho ya mwisho kwa mshitakiwa wa kwanza na wa tatu yaliwasilishwa kortini Novemba 14, 2024, wakati majumuisho ya mshitakiwa wa pili yaliwasilishwa Novemba 15, 2024.
“Kwa kuwa hakuna rekodi juu ya sababu au uhalali wa kutowasilisha majumuisho hayo ya mwisho kwa maandishi kama ilivyoamriwa na mahakama, mahakama hii inachukulia wahusika waliondolea haki zao za kusikilizwa,” alisema.
“Hata majumuisho yaliyowasilishwa na mawakili wa washitakiwa hayawezi kuzingatiwa kwa kuwa yaliwasilishwa pasipo kuwepo amri ya mahakama ya kuongeza muda wa kuyawasilisha,” alisisitiza Jaji Mtembwa.
Je, kifo kilithibitishwa?
Jaji Mtembwa alisema baada ya kupitia kwa uangalifu hati ya mashitaka na ushahidi uliotolewa na Jamhuri na utetezi, swali linalokuja ni kama kosa waliloshitakiwa nalo limethibitishwa bila kuacha shaka ili watiwe hatiani.
Kulingana na Jaji, katika kesi za mauaji ya kukusudia kama hiyo, upande wa mashitaka ni lazima uiridhishe mahakama kuwa kuna mwanadamu alikufa, kifo chake hakikuwa cha kawaida, na washitakiwa ndio waliosababisha kifo hicho.
Akichambua ushahidi, Jaji alisema shahidi wa kwanza, ambaye ni mke wa marehemu, alieleza kuwa Januari 25, 2024, mumewe alihudumiwa katika Kituo cha Afya cha Kilimahewa na alishauriwa arejee siku inayofuata kwa uchunguzi zaidi.
Lakini kwa bahati mbaya alifariki Januari 26, 2024, siku ambayo madaktari walimtaka arudi hospitali kwa uchunguzi zaidi endapo afya yake isingetengemaa.
Shahidi wa tatu, ambaye ni ndugu wa marehemu, alieleza kuwa alijulishwa juu ya kifo cha ndugu yake Januari 26, 2024 na, kutokana na wito wa polisi, Januari 29, 2024 alishiriki katika uchunguzi wa mwili wake Hospitali ya Mkuranga.
Kwa upande wake, shahidi wa tano, ambaye ndiye aliyeufanyia uchunguzi mwili wa marehemu, alifanya uchunguzi huo Januari 29, 2024 na akasema inaonekana mtu huyo alikuwa amefariki siku tatu kabla ya siku hiyo ya uchunguzi.
“Kwa kuegemea ushahidi wa mashahidi namba 1, 3, 4 na 5 wa Jamhuri na shahidi wa pili wa utetezi, ninaridhika kuwa Said Yeguku ni marehemu na alifariki Januari 26, 2024 kutokana na majeraha kichwani yaliyosababishwa na kupigwa na kitu butu.”
Je, washitakiwa ndio wanahusika na kifo?
Jaji alisema baada ya kuthibitisha Yeguku alikufa na kifo chake hakikuwa cha asili (natural death), hoja ya pili inayopaswa kuamuliwa ni kama washitakiwa ndio wanahusika na kifo hicho na kama ni wao, je, waliua wakiwa na nia ovu?
“Kabla ya kuingia kwa undani kuangalia kama washitakiwa wanahusika na kifo hicho, kwanza nitachambua kwa kifupi kama hati ya mashitaka iliandikwa kwa usahihi na upande wa mashitaka,” alisema Jaji Mtembwa na kuongeza:
“Kama nilivyoeleza awali, pande zote walipewa nafasi ya kuieleza mahakama kuhusu usahihi wa hati ya mashitaka, lakini kwa uwazi na bila uhalali walishindwa kufanya hivyo kwa kufuata amri ya mahakama. Matokeo ya kukataa huku, nilizingatia kuwa wamepoteza haki yao ya kusikilizwa.”
Jaji alisema ni jambo la msingi katika haki ya jinai kwamba msingi wa kesi yoyote ya jinai ni hati ya mashitaka, na kwamba ndiyo moyo, ubongo na damu ya mchakato wa haki katika usikilizwaji wa kesi yoyote ya jinai.
“(Hati ya mashitaka) ina jukumu la pande mbili: kumfahamisha mshtakiwa asili ya mashtaka na kumruhusu kuandaa utetezi wake,” alisema Jaji, na kuongeza kuwa hilo linaifanya hati ya mashitaka kuwa muhimu katika usikilizwaji wa kesi ya jinai.
Jaji alisema maelezo yanayopatikana katika hati ya mashitaka yanafanya kuwa takwa la lazima kwa upande wa mashitaka kwamba ushahidi utakaoletwa na mashahidi wao uunge mkono maelezo ya shitaka analoshitakiwa nalo mshtakiwa.
“Pale ambapo tarehe mahsusi ya tukio imetajwa kuhusiana na shitaka lolote la jinai, ushahidi wa mashitaka ni lazima uonyeshe tukio lilitendeka siku hiyo. Kunapokuwa na utofauti, hati ya mashitaka lazima ifanyiwe marekebisho,” alisema.
Jaji alisema katika kesi hiyo, hati ya mashitaka inaeleza kuwa Yeguku aliuawa Januari 8, 2024, lakini hakukuwa na ushahidi wa mashahidi wa upande wa Jamhuri ulioonyesha aliuawa Januari 8, 2024.
Alisema ushahidi wa Jamhuri unaonyesha ingawa alishambuliwa Januari 8, 2024, alikuja kufariki Januari 26, 2024, na ni vigumu kueleza kwa nini hati ya mashitaka ilieleza aliuawa Januari 8 licha ya kuhudhuria hospitali Januari 25.
Jaji alisema kwa maoni yake, hati ya mashitaka haikuandaliwa sawasawa, na hivyo kutowatendea haki washitakiwa kwa kuwa hawakuweza kuandaa utetezi wao kutokana na utofauti uliokuwepo kati ya hati ya mashitaka na ushahidi halisi.
Kulingana na Jaji, katika mazingira hayo, upande wa mashitaka ulipaswa kuifanyia marekebisho hati ya mashitaka ili iungwe mkono na ushahidi, lakini kushindwa kuirekebisha kunaonyesha marehemu aliuawa Januari 26 na si Januari 8.
“Hii haisababishi tu kukiukwa kwa haki, bali pia inafanya kesi ya mashitaka kukosa uthibitisho,” alisema Jaji, na kuongeza kuwa utofauti huo kati ya hati ya mashitaka na ushahidi kuhusiana na tarehe kunafanya kosa lisithibitishwe.
Ni kwa msingi huo, Jaji aliamuru washitakiwa wote watatu waachiliwe huru.