Wagosi waanza kuvimba, waipiga mkwara JKT Tanzania 

USHINDI mtamu. Baada ya kupata ushindi wa kwanza ndani ya miezi miwili na siku 15, Coastal Union imewapiga mkwara maafande wa JKT Tanzania itakayokutana nao mechi ijayo kwamba, wajiandae tu kuchezea kichapo kwani  gari la Wagosi wa Kaya limeshawaka Ligi Kuu Bara.

Coastal ilipata ushindi mnono wa mabao 4-1 dhidi ya TZ Prisons na kuzika mzimu wa kukaa siku 76 bila kushinda mechi ya Ligi Kuu, kwani rekodi zinaonyesha ilishinda mara ya mwisho Novemba 26 mwaka jana ilipoinyoa Mashujaa kwa mabao 2-0 kwenye Uwanja wa nyumbani wa Mkwakani.

Meneja wa timu hiyo, Abdul Ubinde, ameliambia Mwanaspoti  kuwa lengo lao ni kuvuna pointi tatu muhimu kwa kila mechi iliyopo mbele yao baada ya awali kucheza mechi sita mfululizo bila ushindi.

Ubinde alisema kikosi hicho kimefanya maandalizi ya kutosha baada ya kurejea kutoka Mbeya na kwamba morali ya wachezaji ipo juu kufuatia ushindi huo mkubwa.

“Tunaiheshimu JKT Tanzania ni timu ngumu na yenye nidhamu kubwa, lakini sisi tunahitaji pointi tatu kwa sasa kila mechi kwetu ni kama fainali,” alisema Ubinde.

Ubinde aliongeza kuwa wanajua presha ya kucheza dhidi ya JKT nyumbani kwao, lakini wamejipanga kuhakikisha wanaondoka na matokeo chanya.

“Tunajua rekodi zinaonyesha hatujawa na matokeo mazuri sana ugenini dhidi ya JKT, lakini mpira unachezwa uwanjani. Tumejipanga vizuri, wachezaji wako tayari kupambana kuhakikisha wanaziwania pointi hizo,” ameongeza.

Tangu mwaka 2018, Coastal Union na JKT Tanzania zimekutana mara 11 kwenye Ligi Kuu Bara katika mechi hizo, zimetoka sare mara tatu na timu zote zikishinda mara nne.

Hata hivyo, takwimu zinaonyesha kuwa Coastal imekuwa na wakati mgumu inapocheza ugenini dhidi ya Maafande hao. Kati ya ushindi wa mechi hizo dhidi ya JKT, Coastal imeshinda mara moja tu ugenini.

Kwa upande wa JKT, katika mechi nne walizoshinda, imepoteza mara moja tu nyumbani, jambo linaloonyesha uimara wao wanapocheza mbele ya mashabiki wao.

20 Okt 2018: Coastal 0-0 JKT

02 Mar 2019: JKT 1-0 Coastal

04 Feb 2020: JKT 1-1 Coastal

26 Jul 2020: Coastal 0-1 JKT

28 Sep 2020: Coastal 1-0 JKT

21 Feb 2021: JKT 2-0 Coastal

18 Dec 2023: JKT 0-1 Coastal

25 May 2024: Coastal 0-0 JKT

25 Sep 2024: JKT 2-1 Coastal

07 Feb 2025: Coastal 2-1 JKT

22 Sep 2025: Coastal 1-2 JKT