Dar es Salaam. Zile kelele za baadhi ya wafanyabiashara kutishia kuandamana baada ya majina yao kutokuwamo kwenye orodha ya wanaotakiwa kurejea Kariakoo, sasa zimegeuka shubiri kufuatia kufunguliwa rasmi kwa soko hilo.
Soko la Kariakoo lilifunguliwa Februari 8, 2026 baada ya kukarabatiwa kwa miaka minne tangu lilipoungua moto na kuteketeza mali za wafanyabiashara. Tayari baadhi yao wamesharejea na kuanza biashara lakini wengine wameonyesha kusita.
Katika kipindi cha ujenzi, wafanyabiashara walihamishiwa kwa muda katika masoko ya Kisutu, Karume na Machinga Complex. Hata hivyo, kurejea Kariakoo kumekumbana na hofu ya kupoteza wateja waliowajenga kwa miaka minne pamoja na gharama kubwa ya kodi ya vizimba.
Karim Jabiri, mfanyabiashara wa nyanya aliyekuwa Machinga Complex, amesema kodi ya Sh120,000 kwa mwezi Kariakoo ni kubwa ukilinganisha na anacholipa sasa.
“Boksi la nyanya tunanunua Sh25,000, halafu ulipe ushuru wa Sh4,000 kwa siku, inafika Sh120,000 kwa mwezi. Hapa tulipo tunalipa karibu Sh24,000 kwa mwezi, angalau faida inaonekana,” amesema.
Salim Omar naye amesema muundo wa ghorofa wa soko hilo unaweza kuwa changamoto kwa biashara za bidhaa za bei nafuu kama nyanya, akihofia wateja kukwepa kupanda ghorofani kununua bidhaa zinazopatikana pia barabarani.
Kwa upande wake, Idrissa Makengwa wa Soko la Kisutu amesema eneo alilopata ni zuri na linaonekana kirahisi kwa wateja, hivyo anajifikiria kuondoka. Ameongeza kuwa wengi walipata hasara kubwa wakati wa ajali ya moto na wengine walilazimika kukopa ili kurejesha mitaji.
Ekelia Ndaga, mfanyabiashara wa mbogamboga, ameomba Serikali iwape muda wa miezi sita bila kulipa kodi ili wajipange upya.
“Tunarudi kama wageni. Wateja walishasambaratika. Itakuwa nafuu tukipewa muda wa kujipanga kwanza,” amesema.
Akifungua soko hilo, Rais Samia Suluhu Hassan aliitaka Tamisemi kuangalia uwezekano wa kupunguza kodi, lakini akasisitiza zisipunguzwe kiasi cha kushindwa kuliendesha soko. Alisema wasiomudu wanaweza kutafuta maeneo mbadala.
Meneja Mkuu wa Shirika la Masoko Kariakoo, Ashraf Abdulkarim, amesema wafanyabiashara wana siku 30 kuingia kwenye vizimba vyao, vinginevyo watanyang’anywa na kupewa wengine.
Kwa upande mwingine, Meneja wa Machinga Complex, Stella Mgumia, amesema hana tatizo na wafanyabiashara kumiliki maeneo zaidi ya moja iwapo wanazingatia masharti ya soko.
Mwakilishi wa wafanyabiashara, Ramadhani Kakandilo amesema si kosa kuwa na zaidi ya eneo la biashara, akisisitiza lengo ni kukuza uchumi.
Kwa mujibu wa Kakandilo, hadi sasa asilimia 80 ya wafanyabiashara wamesharejea Kariakoo.
Naye Meneja wa Soko la Kisutu, Rachel Mwakapoje, amesema hajapokea maelekezo rasmi ya kuwaondoa wafanyabiashara waliopo, huku akieleza kuwa soko hilo bado lina nafasi ya ziada. “Kuwaondoa au kutowaondoa hawa wafanyabiashara waliohamishiwa hapa nasubiri maamuzi ya uongozi wa juu, ingawa soko bado lina nafasi ya ziada halijajaa.”