Dodoma. Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolph Mkenda amesema zipo fursa mbalimbali ambazo zinatolewa na Serikali kwa wanafunzi wa kike ambao wanasoma masomo ya sayansi ikiwemo kupata mikopo kwenye bodi ya mikopo ya elimu ya juu, na kwa wale waliopata ufaulu mzuri kwenye mitihani yao ya kumaliza kidato cha sita kupata ufadhili wa kusoma chuo kikuu bure ndani na nje ya nchi kupitia ufadhili wa Samia Scholarship Extended.
Amesema yote hayo yanafanyika ili kuwahamasisha wasichana na watoto wa kike nchini kusoma masomo ya sayansi ambao idadi yao ni ndogo kulinganisha na wanaume.
Profesa Mkenda ameyasema hayo leo Jumatano Februari 11, 2026 Jijini Dodoma kwenye maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya wanawake na wasichana katika sayansi.
Amesema siku hiyo imetengwa na dunia kwa sababu bado kuna fursa ya kuwapata wanasayansi wengine na wazuri kutokana na wasichana na wanawake ambapo mpaka sasa hivi hawajaitumia kikamilifu.
”Takwimu zinatuambia idadi ya wanawake wanasayansi duniani ni takribani asilimia 36 ya wanasayansi wote lakini tunajua kuwa wanawake ni wengi kuliko wanaume. Hapa Tanzania sensa yetu inaonyesha kwamba asilimia 51 ya Watanzania ni wanawake kwa hiyo ingetarajiwa wanasayansi angalau nusu wawe ni wanawake.
“Kwa kadri tutakavyoweza kuongeza idadi ya wanawake katika sayansi tunajiongezea fursa ya kuwapata wanasayansi walio bora ambao watatusaidia sana katika kuendeleza nchi yetu. Ndiyo maana umoja wa mataifa umeona umuhimu wa kuwa na siku maalumu kama hii kukumbushana, kuhimiza na kuhakikisha kwamba tunawatia moyo hasa mabinti zetu wanaosoma waone umuhimu wa kusoma masomo ya sayansi tuweze kupata wanasayansi wengi duniani.”
Amesema zipo fursa mbalimbali zinazotolewa kwa wanafunzi wanaosoma masomo ya sayansi nchini kwani huwa wanapewa kipaumbele kwenye bodi ya mikopo lakini pia kwa wale waliofanya vizuri kwenye mitihani ya kumaliza kidato cha sita hupata ufadhili wa kusomeshwa chuo kikuu na Serikali.
Amebainisha kuwa kupitia ufadhili wa Samia Scholarship Extended ulioanza mwaka 2025 umefadhili wanafunzi 50 ambao watakwenda kuchukua digrii nje ya nchi ambapo mpaka sasa wanafunzi 16 wamekwenda nchini Afrika Kusini na wengine 34 watakwenda nchini Ireland kwa ajili ya masomo ya sayansi.
Naibu Waziri Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Maryprisca Mahundi amesema wasichana waliosoma sayansi wanajipunguzia ushindani kwenye soko la ajira hivyo amewahimiza wapende kusoma masomo ya sayansi.
Mahundi amesema wanawake mabingwa wa sayansi wanawategemea katika kuvumbua, kuhimiza na kuacha alama ili na mabinti wengine wafikie hatua waliyoifikia wao kwa kushirikiana na serikali bila kuwasahau watoto wa kiume.
Baadhi ya wanafunzi wa shule za msingi na sekondari za jijini Dodoma wakiwa kwenye picha ya pamoja kwenye maadhimisho ya siku ya kimataifa ya wanawake na wasichana katika sayansi yaliyofanyika leo Februari 11, 2026 Jijini Dodoma.
”Watoto wa kike nawaambia mwanamke kusoma sayansi inawezekana na ukafaulu vizuri na ukawa msaada katika mapambano ya kujenga Taifa, nikijitolea mfano mimi mwenyewe nilipokuwa O level nilisoma masomo yote enzi hizo sisi tulikuwa tunasoma masomo yote kama ni 12 au 14 na unafanya mitihani yote na bado tulikuwa tunapata division one (ufaulu daraja la kwanza),” amesema Mahundi na kuongeza kuwa,
”Nilisoma PCB (Physics, Chemistry and Biology) nikiwa na matamanio ya kuwa daktari wa watoto na wanawake lakini huo haukuwa mpango wa Mungu nikajikuta nimedondokea kwenye mikono ya wanasayansi lakini mainjinia (wahandisi).”
Naibu waziri huyo amesema kuwa hajuti bali anajivunia elimu ya sayansi aliyoipata kwenye vyuo vya sayansi vilivyopo hapa nchini na kuwataka wasibeze kwa kudhani kuwa waliosoma kwenye vyuo hivyo ufaulu wao ulikuwa mdogo kwani wanapokuwa kazini huwa wanafanya vizuri zaidi.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Bunge kuhusu masuala ya elimu, Mabula Magangila amesema sayansi ndiyo suluhisho la asilimia kubwa la changamoto za kidunia.
Amesema kwa kulitambua hilo Bunge litaendelea kutunga sera na sheria bora katika kuhakikisha mtoto wa kike anashiriki kikamilifu katika kupata elimu ya sayansi
“Sasa ni zamu ya mtoto wa kike asionekane ni dhaifu kwa namna yoyote ile kwa sababu anaweza kufanya vizuri sawa na mtoto wa kiume au zaidi, kwa hiyo watoto wote wapelekwe shule kwa usawa kwa sababu ubongo ni uleule,” amesema Magangila.