NI rasmi sasa Mohammed Bajaber kawekwa pembeni Simba hii ni baada ya Clatous Chama kukabidhiwa jezi namba 17 ambayo ndio chaguo la nyota huyo Mzambia tangu ametua Tanzania, anayoitumia pia akiwa na kikosi cha timu ya taifa ya Zambia ‘Chipolopolo’.
Chama aliyerejea Simba kupitia dirisha dogo la usajili akitokea Singida Black Stars, mara baada ya kutua Msimbazi kwa mara nyingine alianza kutumia jezi namba 24 katika Ligi Kuu Bara kabla ya jana dhidi ya KMC akionekana kuirejea namba 17 anayoitumia katika mechi za kimataifa za CAF.
Kabla ya Chama kutua, jezi hiyo ilikuwa inatumiwa na Bajaber aliyetokea Kenya Police ambaye hajawa na namba nzuri za kucheza kutokana na kusumbuliwa na majeraha na tayari gazeti hili lilisharipoti kuwa kiungo huyo huenda akaondolewa katika mfumo kutokana na majeraha aliyonayo.
Akizungumzia suala la kuipata jezi hiyo, Chama amesema ni sehemu ya mafanikio yake kuvaa namba 17 mgongoni hana sababu nyingine yoyote zaidi na anaheshimu wachezaji wote ambao wanathamini kile anachokiomba.
“Nimefurahia kuvaa jezi namba 17 tena nikiwa na Simba naahidi msimu mzuri na ushirikiano wa kutosha kwa wachezaji wenzangu ili tuweze kufikia malengo.”
Chama amemvua namba kiungo huyo Mkenya akiwa ni wa tatu sasa, wakiwamo wawili ndani ya Simba na mmoja wa Yanga aliyoitumikia pia kwa msimu mmoja kabla ya kutua Singida Black Stars msimu huu na kucheza kwa miezi sita kabla ya kurejea Msimbazi mwezi uliopita.
Zoezi la kukabidhiana jezi namba lilifanyika wakiwa katika maandalizi ya msimu ambapo Farid Mussa aliamua kumuachia Chama namba 17 alipojiunga na Yanga msimu wa 2024/25 akitokea Simba naye kuamua kuchukua namba 28.
Chama ndani ya kikosi cha Yanga alicheza kwa msimu mmoja kwenda Singida Black Stars ambako pia aliendelea kuvaa jezi namba 17, Akiwa Simba aliivaa jezi hiyo tangu alipotua kuanzia msimu wa 2018 hadi 2024 na amekuwa akiivaa hadi katika timu ya taifa ya Zambia.
Chama mara baada ya kurudi tena Simba kutoka RS Berkane ya Morocco baada ya awali kuuzwa, aliomba kuvaa jezi namba 17 ambayo ilikuwa inavaliwa na Pape Sakho kipindi hicho hakuwa na hiyana akamkubalia Mzambia huyo kiroho safi.
“Sina tatizo na hii jezi kumwachia kwani sikuja Simba na hii jezi, nimemsikia Chama na ninaamini ni mchezaji mzuri ingawa sijawahi kumuona,” sehemu ya maneno ya Sakho kipindi hicho alipokuwa anaiachia jezi namba 17.
Baada ya kuachia namba 17 Sakho alipewa jezi namba 10 aliyokuwa akiitumia Ibrahim Ajibu kipindi hicho akiwa ameondoka kikosini na kutua Azam FC kwa mkataba wa mwaka mmoja na sasa anakipiga KMC.