Dk Mwigulu atoa maelekezo kudhibiti wagonjwa wapya wa saratani

Dar es Salaam. Kufuatia tahadhari ya wataalamu wa afya kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) kuonya ongezeko la ugonjwa wa saratani kwa zaidi ya asilimia 60 kufikia 2030, Waziri Mkuu Dk Mwigulu Nchemba ametoa wito kwa Wizara ya Afya kuandaa mkakati madhubuti wa kupunguza idadi ya wagonjwa wapya wa saratani.

Mkakati huo, Dk Mwigulu ameutaja kama nguzo muhimu ya kupunguza athari za kupotea kwa rasilimali na nguvu kazi ya taifa.

Serikali inatangaza mkakati huo wakati ambapo takwimu za Wizara ya Afya zinaonyesha Tanzania kukadiriwa kurekodi wagonjwa wapya wa saratani 45,000 kila mwaka, huku vifo vitokanavyo na ugonjwa huo vikiwa takribani 30,000.

Aidha, takribani wagonjwa 27,000 sawa na asilimia 60 ya waathiriwa wapya wa saratani huhitaji huduma za tiba kwa mionzi (radiotherapy), lakini ni wagonjwa 4,000 pekee sawa na asilimia 15 wanapata huduma hizo.

Waziri Mkuu ametoa maelekezo hayo leo Alhamisi, Februari 12, 2026 katika maadhimisho ya miaka 30 ya Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) pamoja na kongamano la Kimataifa la Saratani yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.

“Kutokana na tahadhari ya wataalamu wa afya kutoka WHO kuhusu ugonjwa wa saratani kuongezeka kwa zaidi ya asilimia 60 ifikapo mwaka 2030, Wizara ya Afya mnapaswa kuandaa mikakati ya kupunguza idadi ya wagonjwa wapya,” amesema.

Dk Mwigulu, akieleza hatua zilizochukuliwa kudhibiti saratani, amesema Serikali inatekeleza Mpango Mkakati wa Kudhibiti Saratani 2026/2027–2030/31 wenye lengo la kupunguza vifo vitokanavyo na ugonjwa huo walau kufikia asilimia 30 ifikapo mwaka 2030.

Amesema Serikali imelenga kupanua huduma za saratani katika mikoa mbalimbali kwa kuimarisha utafiti, mafunzo, takwimu na kujenga rasilimali watu wenye ujuzi wa ngazi ya ubingwa na ubingwa bobezi.

“Uhamasishaji uimarishwe ili wananchi wafanye uchunguzi na kinga mapema pamoja na kuimarisha elimu ya afya, kudhibiti matumizi ya tumbaku, pombe kali, kuimarisha chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi pamoja na homa ya ini.

Bado zipo jamii ambazo kila mgonjwa anapopata tatizo huelekeza hisia kwenye imani potofu. Enzi hizo zimepita, tutumie vipimo vya kisayansi vya uchunguzi tunusuru maisha yetu,” amesema.

Msisitizo wa Dk Mwigulu ni kwa wataalamu wa afya kuendelea kutoa elimu kwani hisia zikielekezwa kwenye imani potofu, wagonjwa watacheleweshwa kupata uchunguzi wa kitaalamu na wakicheleweshwa watapunguziwa asilimia za kupata matibabu na kupona.

Dk Mwigulu amesema kupitia maadhimisho hayo, wataalamu wataweka bayana safari ya mapambano dhidi ya saratani kwa kuangalia wapi tulipo, tulipotoka na tunapoelekea.

Amesema kongamano hilo la kimataifa la saratani ni jukwaa muhimu kwa mustakabali wa mapambano dhidi ya saratani barani Afrika.

“Tunaamini Afrika haiwezi kushindwa vita dhidi ya saratani ikiwa kila nchi itafanya kazi kwa jitihada, lakini kama kila nchi itafanya kazi peke yake Afrika haiwezi kushinda vita hivi vya saratani. Hivyo, ili kufikia malengo tunahitaji ushirikiano wa kikanda katika utafiti, mafunzo, kubadilishana wataalamu na uzoefu,” amesema.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Tanzania ipo tayari kushirikiana na nchi zote za Afrika na kupitia ORCI itaendelea kuwa kituo cha kikanda kwa bara zima katika mapambano ya saratani.

Kutokana na athari za saratani, Dk Mwigulu amesema Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kuweka mifumo ya kisera na kutekeleza mipango na mikakati dhidi ya ugonjwa huo.

“Moja ya hatua zilizofanyika ni kuimarisha wigo wa uchunguzi wa saratani za aina mbalimbali ikiwemo saratani ya mlango wa kizazi, tezi dume na utumbo mpana kwa kusogeza huduma ngazi ya msingi.

Hatua hii imetekelezwa kwa kuimarisha mifumo ya rufaa ili wagonjwa wapate huduma kwa wakati na kuweka kipaumbele katika utoaji wa elimu kwa umma,” amesema.

Waziri Mkuu huyo amesema hatua hiyo inalenga kupunguza idadi ya wagonjwa wanaofika hospitali wakiwa katika hatua ya mwisho ya ugonjwa ambapo tiba huwa ghali na uwezekano wa kupona hupungua.

Akieleza utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote, Dk Mwigulu amesema Serikali imefanya uamuzi wa kihistoria kuanzisha bima hiyo iliyoanza kutekelezwa kwa awamu.

Utekelezaji wa bima hiyo, Dk Mwigulu amesema umeanza ndani ya siku 100 za Rais Samia na vipimo vya magonjwa sugu vimeanza kugharamiwa na Serikali kwa asilimia 100 ikiwemo saratani.

Kupitia mfumo wa Bima ya Afya kwa Wote, Dk Mwigulu amesema kila mwananchi atapata huduma za kinga, uchunguzi wa mapema, tiba na ufuatiliaji wa saratani bila kujali kipato chake.

“Mfumo huu utaondoa vikwazo vya kifedha na kulinda familia dhidi ya umasikini unaotokana na gharama za matibabu na kuwezesha Serikali kupanga na kugharamia saratani kwa ufanisi zaidi,” amesema.

Katika uimarishaji wa huduma, Dk Mwigulu amesema Serikali imeendelea kutenga fedha kuimarisha miundombinu na huduma zingine za saratani na tayari imewekeza Sh 18.5 bilioni katika uanzishwaji na ujenzi wa PET/CT scan, mashine ya kuzalisha mionzi na ongezeko la dawa za saratani kufikia asilimia 99.

Dk Mwigulu alihitimisha maagizo yake katika mkutano huo kwa kutaka jitihada ziongezwe kufanya tafiti zenye kutatua changamoto za wananchi kwa kuzingatia uhalisia wa nchi zetu.

Akizungumzia hatua zinazochukuliwa na Serikali kudhibiti ugonjwa wa saratani, Waziri wa Afya, Mohammed Mchengerwa amesema Serikali imeimarisha elimu ya afya kwa umma na kampeni za kinga.

Amesema elimu hiyo huwasaidia wananchi kuchukua hatua mapema ya uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi, tezi dume na ngozi.

Pia, Mchengerwa ametaja eneo lingine lililoimarishwa na Serikali ni huduma za uchunguzi na rufaa kwa wanawake waishio mijini na vijijini kupitia huduma mkoba.

“Tumeimarisha huduma kwa watu wenye ualbino na wanaoishi na VVU,” amesema.

Katika hatua nyingine, Mchengerwa amesisitiza kuunganishwa kwa huduma za saratani na huduma zingine za msingi za afya, ambao ameutaja kuwa msaada wa kuwabaini watu walio kwenye hatua kubwa ya hatari na kuongeza ufanisi wa rufaa na matibabu sahihi yanapatikana kwa wakati.

Akitoa maelekezo yake, Mchengerwa ameelekeza hospitali zote nchini kuhakikisha zinawapeleka wagonjwa wote ORCI kwani kuna wataalamu wengi na vifaa, na kwamba wagonjwa wakitakiwa kwenda hospitali nyingine maelekezo yatatoka ORCI kwenda hospitali hizo.