Dk Mwigulu atoa maelekezo kulinda bidhaa, uwekezaji wa ndani

Mkuranga. Waziri Mkuu wa Tanzania, Dk Mwigulu Nchemba ameagiza kuondolewa kwa misamaha ya kodi kwa bidhaa zinazoingizwa kutoka nje ya nchi ambazo zinazalishwa nchini kwa kiwango cha kutosha, akisisitiza hatua hiyo ni muhimu kulinda viwanda vya ndani, ajira za Watanzania na ustawi wa uchumi wa Taifa.

Maelekezo hayo ameyatoa leo Alhamisi Februari 12, 2026 wilayani Mkuranga mkoani Pwani baada ya kuzindua kiwanda cha mabati cha Lodhia, akieleza kuwa haiwezekani Tanzania ikaendelea kuwa soko la bidhaa za nje wakati ina uwezo wa kuzalisha ndani ya mipaka yake.

Dk Mwigulu ameielekeza Wizara ya Fedha kuchukua hatua za haraka kufuta misamaha ya kodi inayotolewa kwa bidhaa zinazozalishwa kwa wingi nchini, sambamba na kuziba mianya yote ya ukwepaji kodi na udanganyifu unaofanywa na baadhi ya wafanyabiashara wasiokuwa waaminifu.

Ameongeza licha ya Tanzania kuwa na makubaliano ya kikanda ya kibiashara, Serikali itakuwa makini kuhakikisha makubaliano hayo hayatumiwi vibaya kama njia ya kuingiza bidhaa kutoka mataifa ambayo hawajakubaliana.

Waziri Mkuu amezitaka pia wizara zinazohusika na biashara, uwekezaji na udhibiti kukutana kwa pamoja kuchambua kama kuna haja ya kufanya marekebisho ya kisheria ili kuimarisha ulinzi wa uwekezaji wa ndani.

Amesisitiza mapendekezo yoyote ya mabadiliko yawasilishwe kabla ya Bunge la Bajeti linalotarajiwa kuanza Aprili 2026.

Amesema vita dhidi ya magendo na ukwepaji kodi ni sehemu ya mkakati mpana wa kujenga mazingira sawa ya ushindani kwa wazalishaji wa ndani.

“Tukiruhusu ukwepaji wa kodi, hatutakuwa na mazingira mazuri ya biashara. Wale wanaozalisha kwa kufuata sheria wataumizwa na ushindani usio wa haki,” ameonya.

Akizungumzia umuhimu wa uwekezaji, Dk Mwigulu amesema kuvutia wawekezaji ni hatua ya kwanza, lakini kulinda uwekezaji huo na kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa zinapata soko ni hatua muhimu zaidi kwa uendelevu wa viwanda.

“Zamani tulitegemea misaada, lakini enzi hizo zimepitwa na wakati. Sasa tunajenga uchumi unaotegemea sekta binafsi. Hii ndiyo itakayozalisha ajira, kuongeza mapato ya ndani na kukuza uchumi wetu,” amesema.

Kwa upande wake, Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua madhubuti kulinda viwanda vya ndani dhidi ya ushindani usio wa haki kutoka nje.

Amesema kwa sasa nchini kuna viwanda vitano vya mabati vinavyozalisha jumla ya tani 900,000 ambazo ni zaidi ya mahitaji ya bidhaa hiyo, hivyo hakuna sababu ya bati kuingizwa kutoka nje ya nchi na Serikali imeweka mikakati ya kuhakikisha zinapata soko la uhakika.

“Tumeweka hatua za kodi kwa mabati yanayoingizwa kutoka nje ili kulinda wazalishaji wa ndani. Aidha, tunahakikisha mabati yasiyo na viwango yanaondolewa sokoni,” amesema.

Judith alibainisha kuanzia Julai hadi Desemba 2025, zaidi ya mabati 700,000 yasiyo na ubora yalikamatwa na kuondolewa sokoni ili kuwalinda wananchi dhidi ya bidhaa duni.

Waziri wa Ujenzi na Mbunge wa Mkuranga, Abdalla Ulega, amesema jitihada zinafanyika kuifanya Mkuranga kuwa kitovu cha viwanda kwa kuboresha miundombinu muhimu, hususan barabara.

Amesema kipande cha Barabara ya Kilwa kutoka Mbagala hadi Kongowe ambacho kilikuwa kero kwa muda mrefu sasa kinajengwa kwa kiwango cha njia nne kwa gharama ya Sh51 bilioni, fedha zilizoidhinishwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

“Barabara hii itarahisisha usafirishaji wa malighafi kuja viwandani na bidhaa kutoka viwandani kwenda sokoni. Miundombinu bora ni kichocheo kikubwa cha uwekezaji,” amesema Ulega.

Mbali na hilo, Ulega amemuomba Waziri Mkuu kuipandisha hadhi Mkuranga kuwa manispaa kutokana na ongezeko la mapato na idadi ya watu, pamoja na kuharakisha maendeleo ya bandari ya asili ya Shungubweni ili kusaidia shughuli za kibandari na usafirishaji wa mizigo ya viwandani.

Naibu Waziri wa Fedha, Mshamu Munde, amesema uwekezaji wa kiwanda hicho ni kielelezo cha utekelezaji wa sera za Serikali za kuongeza thamani ya malighafi za ndani na kupanua wigo wa viwanda.

Amesema mradi huo utasaidia kupunguza utegemezi wa uagizaji wa mabati kutoka nje, kuongeza mapato ya ndani, kupanua wigo wa kodi na kuchochea ajira katika mnyororo mzima wa thamani wa sekta ya chuma na ujenzi.

“Tunauona uwekezaji huu ukiwa na mchango mkubwa katika utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050 inayolenga kujenga uchumi wa viwanda, shindani na jumuishi,” amesema Munde, akiahidi kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki ya kisera na kisheria kwa sekta binafsi.

Mwenyekiti na mwanzilishi wa Kampuni ya Lodhia, Arun Lodhia, amesema mazingira bora ya biashara yaliyowekwa na Serikali yamewawezesha kupanua uwekezaji wao kutoka viwanda viwili hadi kufikia vitano kwa sasa.

Amesema kampuni hiyo ina mpango wa kuanzisha mradi wa kuzalisha nondo tani 1,000 kwa siku, hatua itakayoiweka Tanzania miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa bidhaa za chuma barani Afrika.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, amesema mkoa huo kwa sasa una jumla ya viwanda 301, kati ya hivyo 235 vikubwa na vya kati, na umejipanga kuongeza uwekezaji zaidi.

Amesema katika siku 100 za uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, mkoa umeandaa kongani saba mpya za viwanda, huku viwanda vinane vikianza uzalishaji.

“Tumejifunza kuwa uwekezaji hauhitaji urasimu wala rushwa, bali unahitaji maamuzi ya haraka. Ukimchelewesha mwekezaji, nchi nyingine itamchukua. Sisi Pwani tumejipanga kuhakikisha tunakuwa kielelezo cha uchumi wa viwanda,” amesema Kunenge.