Kakama yawahimiza vijana kuchangamkia fursa Kiswahili ikiadhimisha miaka 10

Dar es Salaam. Vijana wa nchi za Afrika Mashariki wamehimizwa kuwa wabunifu, kutumia fursa zinazozalishwa na ukuaji wa lugha ya Kiswahili kujiajiri na hata kutengeneza fursa za ajira kwa wengine.

Wito huo umetolewa leo Februari 12, 2025 jijini Dar es Salaam na Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Kiswahili Afrika Mashariki (Kakama), Dk Caroline Asiimwe alipotembelea ofisi za Mwananchi Communications Limited (MCL) ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 10 ya kamisheni hiyo.

Dk Asiimwe amesema kutambuliwa kwa lugha ya Kiswahili kama lugha rasmi kimataifa kumechochea fursa lukuki ikiwemo Tafsiri na Ukalimani, Ufundishaji wa Kiswahili kwa Wageni, uuzaji wa machapisho, Sanaa, uandishi wa machapisho na nyinginezo.

Pia, anasema hata katika zama hizi za ukuaji wa teknolojia kijana mwenye ujuzi na taaluma ya lugha ya Kiswahili anaweza kutumika katika timu ya ubunifu wa programu mbambali akijikita katika upandea wa lugha.

Hata hivyo amesema kutokana na lugha hiyo kuzidi kukua na kuendelea kutengeneza fursa wanaona kuna haja ya na muongozo utakaosimamia

“Kwa wale watumiaji wa lugha hii kwa malengo rasmi kwa mfano Tafsiri na Ukalimani pamoja na Ufundishaji wa lugha ya Kiswahili kuna haja ya kuwarasimisha na kuja na muongozo ili waweze kuelewa sheria na kanuni wanazopaswa kufuata na kuzingatia,”anaeleza.

Amesema hiyo itasaidia kupunguza fani hizo rasmi kufanywa na watu wasio na taaluma, ujuzi na umahiri katika lugha ya Kiswahili.

Ametolea mfano baadhi ya watu kufanya tafsiri na ukalimani bila ya kuwa na taaluma katika fani hizo.

Ameeleza kuwa changamoto hiyo imekuwa ikijitokeza haswa miaka ya hivi karibuni kutokana na ukuaji wa teknolojia.

Amesema baadhi ya watu wamekuwa wakitumia Akili Mnemba (AI) kufanya tafsiri huku wakiwa hawajui misingi na mambo ya kuzingatia wakati wa kufanya tafsiri matokeo yake hujikuta wakipotosha baadhi ya vitu.

“Baadhi ya watu kwa kigezo tu cha kuzungumza lugha ya Kiswahili wanafanya kazi za tafsiri au ukalimani lakini ukiangalia kwa kina ubora wa kazi waliyoizalisha utaona ina kiwango cha chini,”amesema.

Amesema hii inachangia kutokea kwa upotoshaji katika baadhi ya taarifa haswa katika majukwaa ya kidijitali.

“Ili kuondoa changamoto hiyo ni muhimu kwa wataalamu hawa kurasimishwa na kuwekewa sheria na miongozo ya kufuata,”amesema.

Ukuaji wa lugha ya Kiswahili Afrika Mashariki

Akizungumzia ukuaji na ueneaji wa lugha ya Kiswahili  katika ukanda wa Afrika Mashariki, Caroline amesema Kiswahili kimepaa na kuwa moja ya lugha rasmi na lugha za mawasiliano mapana miongoni mwa nchi wananchama wa Jumuiya hiyo.

“Tunajivunia kuwa sasa Kiswahili kimekua na kutambuliwa kuwa moja ya lugha rasmi na lugha ya mawasiliano mapana ndani ya nchi wanachama,” amesema.

Amesema Kiswahili baada ya wakuu wa nchi wananchama kukubaliana, kimerasimishwa kuwa lugha rasmi pamoja na lugha za Kingereza na Kifaransa.

Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki kutoka Tanzania, Abdullah Makame, amesisitiza juu ya umuhimu wa kutekeleza kwa vitendo maagizo na maelekezo yanayotolewa kuhusu ukuzaji na matumizi sahihi ya lugha ya Kiswahili nchini.

Amebainisha kuwa pamoja na kuwepo kwa sera na miongozo mbalimbali, bado kuna changamoto katika utekelezaji wake, hali inayochangia baadhi ya maamuzi na hatua kuchukuliwa bila kufuata utaratibu uliowekwa.

Ameeleza kuwa wakati mwingine masuala yanayohusu utekelezaji wa sera za lugha huchukuliwa kwa uzito mdogo au kuachwa yapitie hatua zisizo rasmi, jambo linaloweza kuathiri malengo ya kukuza na kuendeleza Kiswahili kitaifa na kimataifa.

“Kumekuwa na juhudi kidogo katika utekelezaji wa maelekezo na miakakati ya matumizi ya lugha ya Kiswahili hasa unaotokana na kuchewlewesdhwa kwa utungaji na marekebisho ya kanuni za kisheria,” amesema.

Mbunge huyo ametoa wito kwa jamii kuacha tabia ya kudharau tamaduni za ndani ikiwemo lugha ya Kiswahili na kushabikia lugha za kigeni akisisitiza kuwa kwa kufanya hivyo, wanadhaifisha hatua za kukuza na kupaisha lugha hii kimataifa.

Akizungumzia mafanikio ya Kamisheni hiyo, Caroline amesema kuna miradi mbalimbali ya ushirikiano kati ya Tanzania na mataifa mengine inayolenga kukuza Kiswahili, ikiwemo ushirikiano wa kitaaluma unaowezesha wataalamu na wanafunzi kutoka nchi jirani kama Uganda kuja nchini kujifunza na kubadilishana uzoefu kuhusu lugha hiyo.

“Hili linaonesha kuwa Kiswahili si lugha ya Tanzania pekee, bali ni rasilimali ya kikanda na kimataifa. Ni wajibu wetu kuhakikisha tunasimamia ubora wake kupitia sera na miongozo rasmi,” amesisitiza.

Mkuu wa Kitengo cha Mafunzo wa Kampuni ya Mwananchio Communications Limited (MCL) Rashid Kejo amesema Mwananchi inaunga mkono juhudi za kukuza na kueneza Kiswahili kupitia uzalishaji na usambazaji wa maudhui kwa lugha hiyo.

“Sisi Mwananchi tunaunga mkono na ni wadau muhimu katika kuendeleza na kukuza lugha hii kwani maudhui yetu tunayazalisha na kuyasambaza kwa lugha ya Kiswahili kupitia magazeti yetu ya Mwananchi na Mwananspoti ukiondoa gazeti la The citizen ambalo ni la kingereza,” amesema.

Maadhimisho ya miaka 10 Kakama

Katika kuadhimisha miaka 10 ya Kakama wadau mbalimbali wa Kiswahili na wananchi kutoka nchi nane za Jumuiya ya Afrika Mashariki, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Kenya, Rwanda, Somalia, Sudan Kusini, Uganda na Tanzania wanatarajiwa kukutana Februari 14, 2026 mjini Zanzibar kutathmini na kujadili mustakabali wa lugha ya Kiswahili Afrika Mashariki.