KANALI KIDO ATEMBELEA OFISI ZA CCM MKOA WA KAGERA

Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kanali Yahya Ramadhani Kido, Februari 12, 2026 ametembelea Ofisi za Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kagera kwa lengo la kujitambulisha na kusalimiana na viongozi wa chama ngazi ya mkoa na wilaya.

Ziara hiyo imefanyika siku moja baada ya Kanali Kido kuwasili mkoani Kagera kufuatia uteuzi wake wa hivi karibuni kuwa Mkuu wa Mkoa huo. Katika ziara hiyo, aliambatana na Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera, Bw. Stephen Ndaki, pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Mwl. Erasto Sima.

Kanali Kido alipokelewa katika ofisi hizo na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Kagera, Ndg. Kareem Amri (MNEC), kwa niaba ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa na viongozi wengine wa chama.

Akizungumza wakati wa salamu za utambulisho, Kanali Kido alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Taifa, kwa kumuamini na kumteua kushika wadhifa huo.

Ameahidi kutoa ushirikiano wa dhati katika kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia maelekezo na dira ya Mheshimiwa Rais ya kuwahudumia wananchi kwa ufanisi.

Kwa upande wake, Ndg. Kareem Amri alimpongeza Kanali Kido kwa uteuzi huo na kumtakia mafanikio katika majukumu yake mapya. 

Aidha, alimkabidhi Ilani ya CCM inayobainisha ahadi na vipaumbele vilivyokusudiwa kutekelezwa katika Mkoa wa Kagera, akimtaja Mkuu wa Mkoa kuwa msimamizi mkuu wa utekelezaji wa ilani hiyo ngazi ya mkoa.

Ziara hiyo imeelezwa kuwa ni sehemu ya utaratibu wa kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na Chama katika kusimamia na kutekeleza mipango ya maendeleo kwa manufaa ya wananchi wa Kagera.