Unguja. Licha ya Meli ya MV Mapinduzi II kukamilika matengenezo yake, lakini imeshindwa kufanya kazi kwa sababu ya kukosa sehemu ya kutia nanga katika bandari ya Malindi gati namba 3.
Kutokana na hali hiyo, meli hiyo itasubiri kukamilika kwa ujenzi wa bandari ya Maruhubi inayoendelea kujengwa.
Hayo yamebainishwa leo Alhamisi Februari 12, 2025 na Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Badria Attai Masoud katika mkutano wa Baraza la Wawakilishi unaoendelea Chukwani Unguja Zanzibar.
Badria alikuwa kijibu swali la mwakilishi wa Wingwi, Kombo Mwinyi Shehe aliyetaka kujua hali ya sasa ya meli hiyo baada ya kufanyiwa matengenezo makubwa.
Badria amesema katika bandari ya Malindi gati namba tatu lililokuwa likitumika awali na meli hiyo kabla ya kuharibika, kwa sasa Serikali imetoa kipaumbele kwa meli za mizigo kushusha mizigo na vyakula ili kuondosha changamoto ambayo inaweza kujitokeza ikizingatiwa katika kipindi hiki cha kuelekea katika mwezi mtukufu wa Ramadhan.
“Meli ya MV Mapinduzi II ipo katika hali nzuri na tayari kufanya kazi ya kuchukua abiria na mizigo, itaanza kazi baada ya kukamilika ujenzi wa bandari ya Maruhubi unaotarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi huu,” amesema Badria.
Hata hivyo, katika swali la nyongeza la mwakilishi huyo, alipoomba kujua ujenzi wa bandari hiyo umefikia hatua gani, Naibu Waziri amesema upo katika hatua mbalimbali kwani inajengwa kwa awamu.
Amesema Serikali imetumia Dola za Marekani 3.875 milioni sawa na Sh10.07 bilioni hadi kukamilisha matengenezo yake.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Shirika la Meli Zanzibar (Shipco), Makame Hasnuu Makame mbali na eneo hilo kutumiwa kushushia meli za mizigo, lakini kina cha maji kipo juu ikilinganishwa na uwezo wa meli hiyo.
Amesema meli hiyo inazama mita nne kwenda chini lakini pale eneo hilo yakijaa maji inakuwa mita mbili.
“Mapinduzi kwa pale haiwezi kwenda, awali ilikuwa ikiegeshwa hapo lakini kuna mabadiliko makubwa ya mifumo ya bahari, angalau inatakiwa kuwe na mita tano za kina cha maji,” amesema.
Meli hiyo ya abiria na mizigo ina urefu mita 90 na upana mita 17 ina uwezo wa kubeba abiria 1,200 na tani 200 za mizigo. Ilijengwa kuanzia mwaka 2013 hadi Desemba 2015 nchini Korea Kusini kwa Dola za Marekani 30.5 milioni (Sh71.4 bilioni) zilizotolewa na SMZ.
Wakati akitangaza uamuzi wa Serikali wa kuachana na kuiuza meli hiyo badala yake ifanyiwe matengenezo, Agosti, 2022, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Dk Khalid Salum Muhamed alisema awali ilionekana haiwezi kutengenezeka lakini Serikali imeamua kuitengeneza.
Alisema bei elekezi ya meli hiyo ni ilikuwa Dola za Marekani 14 milioni (Sh32.9 bilioni) na kati ya wazabuni watatu waliojitokeza, mmoja aliyeonekana kuwa na kiwango cha juu ni Dola za Marekani 802,654 (Sh1.8 bilioni) sawa na asilimia 5.7.