Dar es Salaam. Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC), limewaasa waumini wake na jamii kwa jumla kusimamia misingi ya matendo mema kama inavyoagizwa na maandiko matakatifu.
Wito huo umetolewa katika ujumbe wa baraza hilo kwa waumini wa Kanisa Katoliki kuelekea mfungo wa Kwaresma unaoanza Jumatano ijayo ya Februari 18, 2026 likinukuu maandiko matakatifu katika ujumbe wa mfungo huo, “Ndugu msichoke kutenda mema (2The 3:3).”
Katika ujumbe huo wenye kura 52 ukiwa umetolewa na maaskofu 41 wakiongozwa na Rais wao, Wolfgang Pisa, umegusia masuala mbalimbali.
“Katika Kwaresma hii ya mwaka 2026, sisi maaskofu wenu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, tukiongozwa na wazo kuu la mwaka wa Jubilei, 2025 la mahujaji wa matumaini, tumeona ni vyema kuja na ujumbe unaosema: “Ndugu msichoke kutenda mema,” tukijiwekea malengo mbalimbali ya kutusaidia kiroho,” linaeleza baraza hilo.
Maaskofu hao wamesema licha ya changamoto na matatizo yanayojitokeza katika jamii yakiwamo ya asili kama majanga ya mafuriko, njaa, ukame na yale ya kijamii kama mafarakano, vita, usaliti na umaskini hayapaswi kuwavunja moyo watu badala yake wanapaswa kuvumiliana, kujenga moyo wa kusamehe na kudumu katika matendo mema.
Katika taarifa yake iliyotolewa jana Jumatano Februari 11, 2026, baraza hilo limeisihi jamii kudumisha tabia ya kutenda mema, kusameheana, kusaidia wenye uhitaji na kudumisha upendo na mshikamano katika jamii kama ushuhuda wa kiimani.
“Tena tusichoke katika kutenda mema, maana tutavuna kwa wakati wake, tusipozimia kiroho, hivyo lazima tutii himizo hilo kwa maana tutavuna endapo tutatekeleza agizo hilo la kutenda mema,” linaeleza baraza hilo.
Aidha, Baraza hilo limeasa Kwaresma hii ikawe chachu ya kufuta maumivu katika jamii, kufariji wenye shida, kuunganisha jamii na kujenga matumaini mapya kwa kumtumaini Mwenyezi Mungu na kuenzi matendo mema daima kwa ustawi wa kiroho na maisha kiujumla.
Ujumbe huo umeweka wazi matatizo yanayotokea katika jamii yakiwamo njaa, vita, magonjwa, mifarakano, usaliti, umasikini, mabadiliko ya tabia nchi yanayosababisha ukame, mafuriko na kuisababishia jamii maumivu hayapaswi kudumu na kuifanya jamii kuasi kusudi la Mungu.
“Ujumbe huu wa Kwaresma utupatie matumaini kuwa pamoja na changamoto zozote tunazoweza kupitia hapa duniani, tumaini letu ni Mungu mwenyewe kwani hapa duniani sisi na makazi yetu ni mbinguni lakini tutambue kwamba bila kufika huko lazima kila mtu ayaishi mapenzi ya Mungu,” wameasa maaskofu.
Kwaresma ni tendo la kiimani ambalo waumini wa madhehebu ya Kikristo kote ulimwenguni hushiriki mfungo wa siku 40 kama moja ya matendo makuu ya kiimani yanayoagizwa na maandiko matakatifu katika kuwajenga wakristo kiimani na kujijengea mazingira ya kuwa karibu zaidi na Mungu kiroho.
“Maandiko ya Mungu yanasema mtumishi wa Mungu Musa kwa siku arobaini alikuwa mlimani akimsikiliza Mungu, katika kipindi hicho alifunga kula na kunywa (Kut24:12-18). Hii inatufundisha kuwa siku hizi arobaini zina mchango mkubwa katika kurekebisha mwenendo wa maisha yetu tukiongozwa na maandiko matakatifu,” linaeleza baraza la maaskofu.
Katika ujumbe huo, TEC imetaja mambo ya kuzingatia ili kuweza kuishi katika maisha ya wema yanayompendeza Mungu likiweka wazi kuwa, kuishi kwa wema ni safari inayopaswa kukua siku kwa siku ikiambatana na matendo muhimu ambayo mwanadamu anapaswa kuyaishi bila kuchoka, ambayo ni pamoja na kudumisha sala, kutii na kuishi maagizo ya neno la Mungu, kuenenda katika roho na kutenda haki kwa watu wote.
Mengine ni kusamehe bila kulipiza kisasi na kutokukata tamaa na kuvumilia likionya kuwa kukata tamaa ni dhambi na kutokusamehe kuzuia sadaka kupokewa na Mungu.
“Maana mkisamehe watu makosa yao, Mungu wa mbinguni atawasamehe nanyi pia. Lakini msipowasamehe watu makosa yao, naye Baba yenu hatawasamehe makosa yenu (Mt 6:14-15),” linaeleza baraza hilo.