Wakati vyama vya Democratic na Republican vikilitazama sakata la Mafaili ya Epstein kisiasa, wakifikiria mtaji wakati wa uchaguzi wa nusu muhula mwaka huu (2026) na uchaguzi mkuu wa 2028, ukweli ni kwamba kashfa hiyo haipaswi kupewa tafsiri yoyote ya kisiasa na wanasiasa.
Vitendo vya Epstein na wenzake ni kielelezo cha jinsi watu ambao wangepaswa kuaminika katika ukuaji wa watoto wanaweza kuwa hatari zaidi kwa usalama wa kizazi kipya. Ni somo pia kwamba pesa zikimilikiwa na mtu mwovu, jamii hutaabika.
Ndani ya nyaraka za Mafaili ya Epstein kuna majina ya watu mashuhuri kutoka kada mbalimbali; wanasiasa wamo, wafanyabiashara matajiri, magwiji wa teknolojia, wanazuoni, wasanii wenye mafanikio, waandishi, viongozi wa dini na kadhalika. Ni ufafanuzi kuwa kashfa ya Epstein haihusu wanasiasa peke yao.
Mathalan, bilionea Marc Rowan, ambaye ni Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa kampuni ya Apollo Global Management, ametajwa. Kibiashara, washirika wa Rowan ni Josh Harris na Leon Black, ambao nao wametokeza ndani ya vielelezo vya tuhuma za Epstein na wateja wake.
Hali si shwari Hollywood. Nguli wa filamu Woody Allen; mtayarishaji na mwongozaji wa filamu Brett Ratner; mwigizaji Kevin Spacey; mtengeneza filamu Steve Tisch; gwiji mwingine wa utayarishaji wa filamu Harvey Weinstein; na gwiji Bill Cosby ni majina makubwa ya Hollywood ambayo yameonekana kwenye maudhui ya Mafaili ya Epstein.
Jumuiya ya muziki wa hip hop haivuki bila kuguswa. Rapa bilionea Shawn Carter “Jay Z” na nyota Terrence Thornton “Pusha T” wametokeza ndani ya Mafaili ya Epstein. Wamo pia wanamichezo na wawekezaji wa sekta ya michezo kama Joe Gibbs, Jean Todt, Brian Vickers, Michael Waltrip na Casey Wasserman.
Mfalme wa Pop, Michael Jackson, jina lake linasomeka kwenye Mafaili ya Epstein, pamoja na watu wengine maarufu katika sekta ya burudani, Andres Serrano na Peggy Siegal. Wanamitindo Ava Cordero na Ever Anderson-Dubin wametajwa; vilevile mwanamazingaombwe David Copperfield.
Waandishi Dan Ariely, Peter Attia na David Brooks wamo, pamoja na watu maarufu wanaobeba haiba ya vyombo vya habari Marekani kama Michael Wolff na Mehmet Oz; mtaalamu wa tiba mbadala Deepak Chopra; vilevile kiongozi wa kiroho wa imani ya Kibudha ya Kitibeti (Dalai Lama), Tenzin Gyatso.
Mbunge wa zamani wa Buckingham, Robert Maxwell, na binti yake, Ghislaine Maxwell, wametajwa kwa ukubwa kwenye Mafaili ya Epstein. Tajiri wa Kijapani Joi Ito; mwanasheria Brad Karp; mwanasanaa Jeffrey Koons; mwanamama mchangisha fedha za kisiasa Mary Richardson Kennedy; na mwanasaikolojia Stephen Kosslyn nao ni sehemu ya maudhui.
Mfanyabiashara tajiri Robert Kotick; mwanadiplomasia wa Norway Mona Juul; mjasiriamali wa intaneti Christopher Poole; mwandishi Joshua Ramo; mwenyekiti wa kampuni ya EL Rothschild, Lynn Forester de Rothschild, ambaye ana hadhi kubwa kwenye ukoo mkubwa wa Ulaya (Rothschild family); Soon-Yi Previn, ambaye ni mke wa Woody Allen; mwandishi Al Seckel; na mwanasheria David Schoen pia wamo.
Nguli wa sekta ya fedha Jes Staley; jaji wa zamani wa Marekani Ken Starr; na bilionea Les Wexner ni sehemu ya orodha. Unaweza kurejea jina kwa jina, ukabaini kwamba hao ni wenye umaarufu kijamii na mitandaoni. Wana nguvu kubwa ya kifedha na ushawishi wa kijamii. Inadhaniwa kwamba orodha ni ndefu zaidi. Hapo ndipo kwenye shinikizo la kutaka mafaili yote yawekwe wazi.
Vitendo vya Epstein vya kuwatumia mabinti wadogo kingono si jambo linalobishaniwa. Hukumu za Epstein na baadhi ya watu wake wa karibu zipo wazi kwa jamii. Agosti 10, 2019, Epstein alikutwa amefariki dunia akiwa ndani ya mahabusu maalum katika gereza la Metropolitan Correctional Center (MCC), New York.
Taarifa za kitabibu zilisema Epstein alijiua. Umma haukukubali ukweli huo moja kwa moja. Nadharia kubwa ni kwamba Epstein aliuawa ili watu wazito alioshirikiana nao (wateja wake) wawe salama. Epstein alikuwa akishikiliwa kwa makosa ya usafirishaji wa binadamu kwa ajili ya ngono na kuwatumikisha mabinti wadogo kingono, yaani ubakaji.
Ghislaine Maxwell alikuwa mpenzi wa Epstein. Hivi sasa yupo jela akitumikia kifungo cha miaka 20 baada ya kukutwa na hatia ya kutenda uhalifu wa kingono na kuwanyanyasa mabinti wadogo kwa kushirikiana na Epstein. Juni 28, 2022, Jaji Alison Nathan wa Mahakama ya Shirikisho, Manhattan, New York, aliamuru Ghislaine kwenda jela miezi 240 (miaka 20).
Ghislaine, mwanamke kutoka familia yenye hadhi kubwa Uingereza, akiwa mtoto wa mbunge wa zamani wa jimbo la Buckingham, Robert Maxwell, mbali na kuwa mpenzi wa Epstein, mafaili yanamtaja kuwa ndiye aliyehusika kwa sehemu kubwa kutafuta mabinti wadogo na kuwasafirisha kwenda kwenye makasri ya Epstein walikofanyiwa vitendo vya ngono.
Ni kashfa ya ulimwengu kwamba Epstein aliwafanyia ukatili wa kingono mabinti wadogo. Kashfa inatanuliwa kuwa nyakati za uhalifu wake alikuwa akiwachukua mabinti wadogo na kuwapa kama zawadi wateja wake wawatumie, na wengine aliwatumia yeye mbele ya wageni wake. Hao wageni au wateja ni watu mashuhuri, matajiri na wanasiasa wakubwa.
Idara ya Upelelezi ya Marekani (FBI), pamoja na polisi, walibaini kuwa ndani ya makasri ya Epstein alifunga kamera za siri zilizorekodi kila kilichotendeka ndani. Inaaminika kuwa aliwategea wateja wake kamera ili abaki na siri zao. Ni kanuni kwamba ukiwa na siri nzito ya mtu, unaweza kumgeuza kuwa mateka wako.
Inadaiwa kuwa alitumia siri za wateja wake kujiongezea utajiri, vilevile kupata ulinzi wa kutokamatwa, maana kesi dhidi yake ingemaanisha anguko la mibuyu mingi msituni. Ndiyo sababu kila linalochomoza kwenye Mafaili ya Epstein hutengeneza kichwa kikubwa cha habari. Watu wanataka kujua alikuwa na uhusiano gani na Epstein.
Je, alikuwa na ushirika wa kibiashara, kijamii, au alikuwa sehemu ya uhalifu mkubwa uliokuwa ukitendeka ndani ya makasri ya bilionea huyo? Endapo jina linatajwa halafu ikaelezwa ulikuwa unakwenda kwenye kasri lolote la Epstein, wasiwasi dhidi ya heshima yako huwa mkubwa. Ikitokea picha yako ikaonyesha ulikuwa ndani ya jumba la Epstein, uadilifu wako huingia mashakani.
Inavuma sasa, lakini sakata la Mafaili ya Epstein ni haki iliyocheleweshwa kwa muda mrefu. Waliojaribu kulalamika walipitia msukosuko mkubwa na kuishia kuvuna fedheha ya kijamii. Inafundisha pia kuwa mapambano ya haki dhidi ya mtu mwenye fedha na mamlaka ya kijamii—iwe ya dola (hard power) au nguvu ya ushawishi (soft power)—huhitaji hata mkono wa Mungu kuvuka.
Maria Farmer ni mwanamke wa kwanza kuripoti polisi tukio la kubakwa na Epstein. Maria, msanii aliyekuwa akifanya kazi kwa Epstein, aliripoti tukio lake la kubakwa na bilionea huyo mwaka 1996. Hata hivyo, malalamiko yake hayakufanyiwa kazi. Hakuna uchunguzi wowote uliofanywa dhidi ya Epstein.