Makada waliokimbilia Chaumma mbioni kurejea tena Chadema

Dar es Salaam. Kada wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Patrick Assenga, amesema yupo kwenye maandalizi ya mwisho kukihama chama hicho na kurejea Chama cha Demokrasia na maendeleo (Chadema) kuendeleza mapambano.

Amesema sababu ya kufanya hivyo zipo tatu kwanza kimepoteza mvuto, uelekeo na maono waliyofikiria kuyafikia, kutokulaani mambo yanayowakwaza wananchi na kukosoa vyama vingine vya upinzani badala ya chama tawala.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa Chaumma, John Mrema, amejibu yeyote atakayetangaza kuondoka kama Assenga ni haki yake, kwani hakuna anayelazimishwa kujiunga au kubaki katika chama chochote cha siasa.

“Ni haki na utashi wa mtu binafsi,  hiyo ndiyo demokrasia. Ana haki ya kutimiza haja ya moyo wake,” amesema.

Assenga ni miongoni mwa wanachama waliokihama Chadema, wakiwa kwenye mwambata wa kundi la G55, kujiunga na Chaumma kwa kile walichodai kutimiza malengo ya kugombea nafasi za ubunge wakikinzana na msimamo maarufu wa Chadema… hakuna mabadiliko hakuna uchaguzi.

Assenga aliyekuwa anashika nafasi ya uweka hazina wa Kanda ya Pwani kabla ya kujiuzulu na kujiunga na Chaumma akiwa sambamba na makada wengine aliwania ubunge Moshi Mjini, Mkoa wa Kilimanjaro ingawa hakushinda.

Baada ya uchaguzi huo, Kada huyo alikuwa kimya hadi Februari 11, 2026 alipojitokeza kufuatilia kesi ya uhai ya Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu mahakamani huku akionyesha ishara ya chama hicho.

Mwananchi ilimpigia leo, Februari 12, 2026, Assenga na katika maelezo yake, amesema chama hicho kimepoteza mwelekeo, hivyo hawezi kuendelea kubaki ndani yake na kwamba yuko katika hatua za mwisho kurudi Chadema.

“Siku chache zijazo nitatangaza rasmi uamuzi wangu wa kurudi nyumbani Chadema kuendeleza mapambano. Kwa umri wangu siwezi kustaafu siasa,” amesema.

Amesema hawezi kubaki katika chama kinachoshiriki uchaguzi huku matokeo makubwa yakijitokeza kama yaliyotokea Oktoba 29, 2025 lakini hakitoki hadharani kulaani wala kutoa msimamo wake.

“Unakuta kinashiriki vikao vya vyama vya mkakati, lakini unaona kabisa kimepoteza mwelekeo. Badala ya kushughulika na chama tawala, kinajihusisha zaidi na vyama vingine vya siasa,” amesema.

Amesema wajibu wa chama cha siasa ni kukosoa sera zisizoridhisha za chama tawala na kuwasilisha sera mbadala kwa lengo la kushinikiza utekelezaji unaowaletea wananchi ustawi bora.

“Ukiona chama kinatoka kwenda kukosoa vyama vingine vya upinzani na kuacha kilichopo madarakani, tafsiri yake hakijui kinashiriki siasa kwa ajili ya nini,” amesema.

Amesema hawezi kubaki katika chama ambacho, mambo mabaya yanapotokea kitaifa, hakisemi chochote. Ameongeza kuwa hali hiyo inaonyesha chama kimepoteza mwelekeo na kwamba anachokifanya ni kuzungumzia uhalisia uliopo ndani ya chama.

“Ni uhalisia uliopo ndani ya chama. Nimeshawaeleza, lakini hakuna majibu. Inaonekana ni kweli tumekuwa ‘projekti’. Nikueleze, wengi watakihama chama mimi natangulia,” amesema.

Amesema Chaumma kimepoteza hewa ya oksijeni na kilichobaki ni kifo, akieleza kuwa chama cha siasa kinategemea watu na kinapaswa kuonyesha ukaribu na wananchi, hasa wanapopitia shida.

Amesema Chaumma kilipata viongozi mashuhuri na wenye nguvu na kama kingekuwa na malengo thabiti kingepiga hatua kubwa,  lakini bila kuwa karibu na wananchi hakiwezi kuwa na kesho bora.

“Ni makada wengi ambao hawakubaliani na mwelekeo wa chama, lakini wanashindwa namna ya kutoka. Nawahakikishia narudi nyumbani na wengi watakuja,” amesema Assenga.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa Chaumma, John Mrema, amesema yeyote atakayetangaza kuondoka kama Assenga ni haki yake, kwani hakuna anayelazimishwa kujiunga au kubaki katika chama chochote cha siasa.

“Ni haki na utashi wa mtu binafsi, hiyo ndiyo demokrasia. Ana haki ya kutimiza haja ya moyo wake,” amesema.

Alipoulizwa kuhusu madai ya Chaumma kupoteza mwelekeo, amesema: “Sidhani kama anaeleweka anachosema. Labda aseme mwelekeo uliopotea ni upi, alitaka kwenda wapi, na mwelekeo wa Chaumma ni upi?”

Kwa mujibu wa Mrema, Assenga alijiunga na Chaumma kwa masilahi binafsi, lakini anaona hakuyapata, na madai yake mengi hayana hoja.

“Mwelekeo wake ulikuwa kupata kiti, na hakukipata. Chaumma iko dhabiti, na muda mfupi ujao tutakuja na pakeji mpya ya shughuli kama mwanzo mpya baada ya uchaguzi,” amesema.

Katika hatua nyingine, Mwananchi ilimtafuta kada mwingine wa chama hicho, Henry Kileo ambaye yuko kimya kujua mustakabali wake katika majibu yake amesema kwa sasa hajihusishi na masuala ya siasa na amejiingiza katika shughuli za kibiashara ili kurejesha hasara aliyopata  katika uchaguzi.

“Nimekaa mbali na siasa, sijui chochote. Niko na biashara zangu tangu tumalize uchaguzi. Mambo yanayoendelea siyajui, sijaongea na wanachama, na siingii katika majukwaa kabisa,” amesema.

Alipoulizwa kama yuko tayari kurudi Chaumma, amesema: “Nikiwa tayari nitajua cha kufanya, lakini kwa sasa niko bize na shughuli zangu. Ndiyo maana sifuatilii kinachoendelea.”

Alipoulizwa, akiwa kiongozi wa G55, haoni kama ukimya wake unaathiri waliokuwa wanamfuata, amesema: “Kila mtu anafanya mambo yake kulingana na vipaumbele alivyojiwekea. Kwa sasa ninashughulika na mambo yangu binafsi.”

Amesema shughuli za siasa zinahitaji uchumi imara, na kwa vyama vya upinzani mazingira ya kiuchumi ni magumu, ndiyo maana ameona ni muhimu kuweka nguvu katika eneo hilo.

“Sijui kama wamekaa vikao wala watakaa lini. Nimekaa mbali na chama; sijui chochote kinachoendelea,” amesema Kileo.