Mapinduzi ya utafiti yaliyookoa maisha ya mamilioni

Kilombero. Taasisi ya Afya Ifakara (IHI) imeeleza mafanikio makubwa ya kisayansi yaliyochangia kuokoa mamilioni ya maisha Tanzania na duniani huku ikiweka bayana dira ya kukabiliana na changamoto mpya za afya ikiwemo magonjwa ya mlipuko, mabadiliko ya tabianchi na usugu wa vimelea dhidi ya dawa.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa maadhimisho ya miaka 70 ya taasisi hiyo iliyofanyika leo Alhamisi, Februari 12, 2026 Ifakara mkoani Morogoro, Mkurugenzi wa IHI, Dk Honorati Masanja, amesema taasisi hiyo haisherehekei tu historia yake, bali inazindua awamu mpya ya ubunifu na utafiti unaolenga kujenga mifumo imara ya afya kwa vizazi vijavyo.

“Hatujakusanyika kuadhimisha tarehe kwenye kalenda, bali kusherehekea miongo saba ya ustahimilivu, uvumbuzi na kujitolea kwa afya ya binadamu. Kutoka maabara ndogo ya mwaka 1956 hadi taasisi huru ya kimataifa inayoongozwa na Watanzania, safari yetu ni ushahidi wa nguvu ya ushirikiano na maono ya mbali,” amesema Dk Masanja.

Amesema taasisi hiyo ilianzishwa chini ya Taasisi ya Tropiki ya Uswisi (Basel), kufuatia ziara ya Dk Rudolf Geigy mwaka 1949 aliyebaini Ifakara kuwa eneo mwafaka kwa tafiti za magonjwa ya kitropiki, hususan Malaria.

Baadhi ya waliowahi kuwa wakurugenzi wa Taasisi ya Afya Ifakara, IHI wakiwa katika picha ya pamoja wakati wakizindua maadhimisho ya miaka 70 tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo. Wa pili kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa sasa Dk Honorati Masanja.



Mapambano dhidi ya malaria

Dk Masanja amesema kwa miaka 70 IHI imekuwa mstari wa mbele katika vita dhidi ya malaria. Watafiti wake walihusika katika majaribio ya awali ya chanjo ya Malaria barani Afrika, ikiwemo chanjo ya SPF66, pamoja na tafiti zilizochangia matumizi ya vyandarua vyenye viuatilifu (ITNs) vilivyobadili mkakati wa kimataifa wa kudhibiti malaria.

“Taasisi ilitoa ushahidi uliochangia Tanzania kuachana na dawa ya chloroquine na kuanza kutumia dawa mseto za artemisinin (ACTs), hatua iliyookoa maelfu ya maisha,” amesema Dk Masanja.

Mbali na Malaria, amesema IHI imefanya tafiti zilizoimarisha huduma za afya ya mama na mtoto, kupunguza vifo vya wajawazito na watoto wachanga, pamoja na kuboresha mifumo ya utoaji huduma vijijini.

Katika mapambano dhidi ya kifua kikuu na Ukimwi, amesema taasisi imechangia maboresho ya uchunguzi wa TB, tafiti za tiba fupi, na mifumo ya utoaji huduma za VVU inayolenga jamii.

Mwenyekiti wa Bodi ya IHI, Abraham Mnzava amesema taasisi hiyo sasa inaelekeza nguvu katika maeneo mapya.

Ameyataja maeneo hayo ikiwemo matumizi ya akili mnemba (AI), tafiti za vinasaba, ufuatiliaji wa magonjwa yanayochochewa na mabadiliko ya tabianchi, na mkabala wa Afya Moja (One Health).

“Dunia inakabiliwa na milipuko mipya, usugu wa vimelea dhidi ya dawa na changamoto za usawa katika huduma za afya. Hii si kumbukumbu tu, bali ni jukwaa la kujipanga kwa miaka 70 ijayo,” amesema.

“Katika mwaka huu wa maadhimisho, taasisi itafanya makongamano ya kisayansi, mijadala ya urithi na usawa, mashindano ya ubunifu kwa vijana, pamoja na uzinduzi wa Mfuko wa Ubunifu wa IHI utakaosaidia kuendeleza tafiti na suluhisho bunifu,” amesema.

Baadhi ya waliowahi kuwa wakurugenzi wa Taasisi ya Afya Ifakara, IHI wakiwa katika picha ya pamoja wakati wakizindua maadhimisho ya miaka 70 tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo. 



Akizungumza kwa niaba ya viongozi wa zamani wa taasisi hiyo, mmoja wa waliowahi kuwa wakurugenzi na Mtanzania wa kwanza kushika nafasi hiyo mwaka 1994, Dk Andrew Kitua ameeleza kuwa mafanikio ya IHI yametokana na ushirikiano wa muda mrefu na wenye usawa kati ya Tanzania na Uswisi.

“Miaka 70 inaonesha ukomavu na uimara katika kukabiliana na mabadiliko ya sera, ufadhili na mwelekeo wa magonjwa. Lakini pia ni safari iliyogharimu juhudi za wengi, wakiwemo waliotangulia mbele za haki,” amesema, akiongoza dakika moja ya ukimya kuwakumbuka waliotoa mchango wao.

Viongozi wa taasisi hiyo walitoa shukrani kwa Serikali ya Tanzania kwa kuweka mazingira wezeshi kwa utafiti wa sayansi, pamoja na washirika wa kimataifa waliounga mkono taasisi hiyo kwa miongo saba.

Walisisitiza kuwa mafanikio ya IHI hayapimwi kwa machapisho ya kisayansi pekee, bali kwa maisha yaliyookolewa, sera zilizoboreshwa na jamii zilizoimarishwa.

Akimwakilisha Katibu Mkuu, Mkuu wa maboresho sekta ya afya kutoka Wizara ya Afya, Dk Timothy Honanji amesema kwa kipindi kirefu taasisi hiyo imefanikiwa kufanya tafiti nyingi na kuchangia katika ugunduzi wa magonjwa na chanjo duniani.

“Tafiti zenu zimeendelea kuwa kinara duniani kote, hamjawahi kuwa mmechakachua. IHI inafahamika zaidi kwa kufanya kazi kama timu.

“Sekta ya afya tuna bahati tunasherehekea miaka 70 wakati tayari tuna dira ya miaka 50 huu ni muda wenu watafiti mtuambie tutavuka vipi hapa tulipo,” amesema Dk Honanji.

Mfamasia mwandamizi kutoka Tamisemi, Dk Regina Richard ameitaka taasisi hiyo kufanya kazi ya ziada kuhakikisha wanatangaza tafiti na gunduzi mbalimbali ili kazi zao ziifikie jamii na kuleta matokeo chanya.