Unguja. Wauzaji wa huduma za utalii 300 kutoka mataifa 20 barani Afrika na kwingineko duniani wamekusanyika Zanzibar kushiriki Jukwaa la Nne la Utalii na Uwekezaji, hatua inayotajwa kuendelea kuchochea ukuaji wa sekta ya utalii visiwani humo.
Jukwaa hilo la siku mbili lililoanza jana, Jumatano Februari 11, na kuhitimishwa leo, Alhamisi Februari 12, 2026, linawakutanisha wadau wa utalii kutoka katika nyanja mbalimbali wakiwamo wawekezaji, waendeshaji wa hoteli, waongoza watalii, taasisi za kifedha na watunga sera.
Akizungumza leo alipotembelea maonesho yanayoambatana na jukwaa hilo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale, Dk Aboud Suleiman Jumbe, amesema utalii wa Zanzibar unaendelea kukua kila siku kutokana na majukwaa kama hayo yanayochangia kuitangaza kimataifa.
Amesema mkutano huo una umuhimu mkubwa kwa Zanzibar kwa kuwa unawakutanisha zaidi ya watu 300 katika sekta ya utalii kutoka mataifa mbalimbali, jambo linaloongeza wigo wa kuitangaza Zanzibar katika masoko tofauti duniani.
“Hii ina maana kubwa kwa Zanzibar. Kukutana kwa mataifa mengi na wadau zaidi ya 300 wa sekta ya utalii kunasaidia kuitangaza Zanzibar kimataifa, ndiyo maana tunaona kila mwaka tunapiga hatua zaidi katika sekta hii,” amesema Dk Aboud.
Amesema jukwaa hilo sasa limevuka mipaka ya kuwa tukio la ndani kwa Wazanzibari pekee; limekuwa jukwaa la kuitangaza Zanzibar na Tanzania kwa ujumla katika anga la kimataifa kwa lengo la kuifanya Zanzibar kuwa kitovu cha utalii barani Afrika.
Kwa mujibu wa Dk Aboud, maendeleo ya jukwaa hilo yanaonekana pia katika kuongezeka kwa ushiriki wa sekta binafsi katika kusimamia, kuratibu na kuendesha shughuli zake, jambo linalochochea ukuaji wa uchumi na kuibua fursa mpya za uwekezaji na ubia.
Akieleza mwenendo wa uwekezaji, amesema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, miradi 590 imesajiliwa, mingi ikiwa ya utalii, yenye thamani ya zaidi ya Dola za Marekani bilioni 6 (Sh15.611 trilioni). Hii inalinganishwa na miradi 1,300 yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 14 (Sh36.426 trilioni) iliyosajiliwa katika miaka yote iliyotangulia.
“Ukiangalia takwimu hizi unaona wazi kuwa sekta ya utalii na uwekezaji inakua kwa kasi. Sekta binafsi nayo inaendelea kuimarika na kuchangia katika mapato ya nchi,” amesema.
Ameongeza kuwa katika kipindi cha takribani miezi sita iliyopita, hususan Desemba mwaka jana na Januari mwaka huu, idadi ya watalii wanaoingia Zanzibar imevunja rekodi kwa kuzidi watalii 100,000 kwa mwezi, hali ambayo haijawahi kushuhudiwa.
“Hatua hii inaonyesha kuwa shabaha ya kufikia watalii milioni 1.5 ifikapo mwaka 2030 inawezekana,” amesema.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Kilifair Promotion Co. Ltd, waandaaji wa maonesho ya Z-Summit, Dominic Shoo, amesema licha ya kuwa na washiriki zaidi ya 120 katika maonesho, jumla ya wauzaji wa huduma za utalii 300 wamejisajili kushiriki jukwaa hilo.
Amesema ushiriki wa mataifa 20 ni ishara ya kuongezeka kwa mwamko wa kimataifa kuhusu Zanzibar, akibainisha kuwa kila mwaka jukwaa hilo limekuwa likionyesha mabadiliko chanya na matokeo yenye tija kwa taifa.
“Tunatarajia kuona biashara kubwa zaidi. Lengo letu ni kuonesha dunia vivutio vya Zanzibar na kiwango cha ukuaji wa utalii wake,” amesema Shoo.
Ameongeza kuwa wanapanga kuanzisha Wiki ya Utalii itakayojumuisha shughuli mbalimbali za sekta hiyo ili kuongeza ushawishi, kukuza utalii na kuimarisha shughuli zake.
Ofisa Mkuu wa Fedha wa Benki ya Exim, mdhamini mkuu wa jukwaa hilo, Shani Kinswaga, amesema huduma za kifedha ni nguzo muhimu katika biashara ya utalii, hususan katika kuwezesha miamala rasmi na kukuza uwekezaji.
“Tunaendelea kushirikiana na wadau wa utalii katika kurahisisha huduma za kibenki kwa watalii, kuboresha mifumo ya malipo na kusaidia miradi ya kukuza biashara ya utalii,” amesema Kinswaga.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wawekezaji wa Utalii Zanzibar (ZATI), Suleiman Ali Mohamed, amesema jukwaa hilo limeleta mafanikio makubwa kwa kuwa sasa linaanza kuvutia washiriki kutoka mataifa mengi zaidi duniani.
“Hii ndiyo kasi tuliyolenga. Tunatarajia kuifanya Zanzibar kuwa kivutio kikuu kwa Afrika na ulimwengu mzima,” amesema.
Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Waongoza Watalii nchini Ghana, Yvonne Donkor, amesema wameshiriki jukwaa hilo kutokana na kuvutiwa na amani, upendo na mshikamano wanaouona Zanzibar, mambo yanayochangia kuvutia watalii wengi zaidi.