Mbunge Dk Makame uchelewaji uchangiaji bajeti Jumuiya Afrika Mashariki unavyokwamisha maendeleo

Dar es Salaam. Kufuatia kusuasua kwa utekelezaji wa mipango ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kunakosababishwa na ukata wa fedha, Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (Eala) kutoka Tanzania, Dk Abdullah Hasnuu Makame amewataka wakuu wa nchi kukutana kujadili namna ya kuziba nyufa ili kuinusuru Jumuiya hiyo.

Dk Makame amebainisha hayo leo Februari 12, 2026 jijini Dar es Salaam alipotembelea ofisi za kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL), akiwa kama mwenyekiti wa Kamati ya Bunge (Eala) ya Masuala Mtambuka.

Amesema kwa sasa jumuiya iko kwenye hali mbaya kutokana na kukosekana kwa fedha kunakokwamisha utekelezaji wa masuala mbalimbali yanayopitishwa na Bunge hilo kwa ajili ya ustawi wa jumuiya na utekelezaji wa itifaki zake.

Amebainisha kwamba michango ya wanachama, ambayo ndiyo chanzo kikuu cha fedha za EAC, imekuwa haikidhi mahitaji kwa sababu baadhi ya nchi wanachama hazichangii, ambapo ni asilimia 38 pekee ya michango ndiyo inatolewa huku asilimia 62 ikiwa haitolewi.

Pia, mbunge huyo amesema mipango na maazimio yanayopitishwa na Eala yamekuwa hayatekelezwi kwa sababu tofauti, ikiwamo kukosekana kwa fedha kwa ajili ya kuanzisha taasisi zitakazoongeza mtangamano wa jumuiya.

Dk Makame amebainisha kwamba anaiona jumuiya ikiwa mahututi huku ikihitaji wakuu wa nchi kuingilia kati ili kuinusuru na hali hiyo na kuifanya ifikie malengo ya kuanzishwa kwake, ikiwamo kufikia mtangamano wa Afrika Mashariki.

“Hili jambo, inatakiwa wakuu wa nchi wakae wenyewe katika kikao chao, walitafakari, waangalie ni wapi kuna nyufa na wapi kuna matatizo warekebishe. Chombo chetu, EAC, hakitakiwi kianguke, hakitakiwi kisimame.

“Tunakwenda na ile nadharia ya baiskeli, baiskeli haisimami kwa sababu ikisimama imeanguka. Baiskeli haina gia ya kurudi nyuma, inakwenda mbele, basi Jumuiya yetu inatakiwa iende mbele,” amesema mbunge huyo.


Amesisitiza kwamba lazima ufanyike utaratibu wa kuinusuru jumuiya kwa kuangalia utekelezaji wa mkataba wa kuanzishwa kwake ili kuhakikisha unatekelezwa kikamilifu na kuziba nyufa zote zinazoirudisha nyuma.

Dk Makame amesema mwenendo wa baadhi ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kutowasilisha michango yao ya kila mwaka unazorotesha ufanisi katika utekelezaji wa mipango ya jumuiya hiyo.

Amesema Jumuiya ina nchi wanachama wanane, na bajeti yake inategemea michango yao ambayo hutumika kwenye shughuli za uendeshaji wa jumuiya, ikiwemo kulipa mishahara ya watumishi, wabunge na majaji.

“Inapotokea kuna nchi hailipi, maana yake ile bajeti ambayo ndiyo mpango kazi wa mwaka mmoja wa utekelezaji unakuwa unaathirika sana kwa sababu jumuiya ina vyombo na taasisi ambavyo vinajikuta vinasuasua kutokana na ufinyu wa bajeti,” amesema.

Amebainisha kwamba nchi ambazo zinalipa michango yao kila mwaka ni Kenya, Tanzania, Uganda na Rwanda. Nchi ambazo hazilipi ni Sudan Kusini, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Somalia.

Mkataba unahitaji kila nchi ilipe ndani ya wakati

Malimbikizo ya Sudan Kusini yaliwahi kufikia dola za Marekani milioni 45, lakini Katibu Mkuu aliyeondolewa aliwashawishi walipe angalau dola milioni 15 ili wasamehewe kiasi kinachobaki, na kwamba waendelee kulipa michango ya kila mwaka.

“Sijajua kama uamuzi ule ulitokana na nini, lakini Sudan Kusini ilipokuwa mwenyekiti wa EAC, ndipo mwenyekiti akatangaza kwamba Sudan Kusini imesamehewa.

“Hii sasa ni mwaka wa tatu, Sudan Kusini imelimbikiza deni lake, tayari imesharudi palepale na hata hivyo kufutwa kwa deni lake ni jambo lililoleta matatizo kwa sababu kwanza halipo kisheria, mkataba hauruhusu kufutwa kwa deni. Deni likilimbikizwa lazima lilipwe. Mkataba hauna sehemu ya kufuta deni,” amesema.

Kwa sasa nchi zote zinalipa kiwango sawa cha takribani dola milioni 7 kwa mwaka, lakini kuna hoja za pembeni kwamba Rwanda na Burundi wangelipa kiwango cha chini kuliko Tanzania na Kenya. Ni sawa, lakini jambo hilo linatakiwa kuwa katika mapendekezo au uamuzi wa mawaziri.

Ibara ya 143 na 146 ya Mkataba wa EAC inazungumzia kuwekeana vikwazo na kusimamishwa uanachama.

Vitu hivi vinatakiwa kufanywa na wakuu wa nchi na wanafanya hivyo kutokana na mapendekezo ya mawaziri. Lakini changamoto ni kwamba unakuta mawaziri hawana kauli moja kwa sababu wanaochangia na wasiochangia wanakaa pamoja kuamua jambo, wanashindwa kukubaliana.

Sisi kama wabunge wa Eala, tuna imani kwamba tuna viongozi katika Jumuiya ambao ni wakuu wa nchi na wao wanaweza kutekeleza wajibu wao vizuri kuinusuru hii jumuiya.

Jumuiya iliporomoka mwaka 1977, lakini mwaka 1999 viongozi wakasisitiza kwamba jumuiya lazima irudi kwa sababu sisi ni wamoja, tulitenganishwa na michoro ya kwenye ramani, lakini sisi ni watu wamoja.

Waasisi wa Jumuiya waliapa kwamba hii jumuiya haitakuja kuanguka kwa sababu tumesaini mkataba. Huu mkataba utakuwa ndiyo kiongozi wetu, ndiyo Katiba yetu, tutaifuata.

Leo baadhi ya nchi zikijitokeza hazilipi, hazifanyi wajibu wake, mfano nyingine zinafungiana mipaka, wakati EAC ina misingi ikiwemo ujirani mwema, kusuluhisha migogoro kwa njia ya amani. Leo tunagombana wenyewe ndani kwa ndani, tukitaka kutafuta suluhu, haipatikani ndani mpaka twende Doha, Qatar au Washington. Maana yake kuna tatizo katika jumuiya yetu.

Mwaka 2013, EAC ilikamilisha itifaki ya umoja wa fedha. Ilizungumzwa kwamba itatumia kipindi cha miaka 10 kuanzia mwaka 2014 hadi 2024; kutakuwa na mpango kazi wa kutekeleza itifaki hiyo, na katika kipindi hicho zitaanzishwa taasisi nne ambazo ni taasisi ya fedha, taasisi ya ufuatiliaji na utekelezaji, taasisi ya takwimu na baadaye ipatikane Benki Kuu ya Afrika Mashariki na kuwa na sarafu moja.

Mwaka 2022, mawaziri wa fedha walikubaliana kusogeza mbele hadi 2031, lakini mpaka sasa mipango hiyo minne hakuna hata mmoja uliotekelezwa au kuanzishwa.

Miswada ikiletwa bungeni, wabunge tunaipitisha kwa jinsi walivyohitaji.

Nchi hizi hazijaonyesha kwamba kuna ule utayari na ari ile ya kutekeleza mtangamano. Kuna haja ya kutangamana; kuna malengo ya kutangamana yameainishwa katika Ibara ya Tano ya Mkataba wa Afrika Mashariki.

“Ipo haja ya wakuu wa nchi kuketi kutafakari na kutoa maelekezo ambayo yanatekelezeka lakini wayabane na muda, waseme hili litekelezwe ndani ya muda fulani, hili litekelezwe ndani ya muda fulani, vinginevyo kwa hivi tunavyokwenda.

“Jumuiya iko katika wodi ya wagonjwa mahututi na daktari wa Jumuiya ni wakuu wa nchi, wao ndiyo wenye tiba. Waende wakakae, wakapitie, kwa sababu hii jumuiya iliundwa kwa maono na maelekezo yao kama wakuu wa nchi, sasa wao waishi ndoto zao,” amesema.

“Kuna changamoto ya usimamizi na utekelezaji wa Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo viongozi wetu wanapochukua madaraka katika ngazi ya urais au uwaziri, wanaapa kwamba watalinda na kutetea Katiba.

“Huu mkataba ni sehemu ya Katiba za nchi wanachama kwa sababu uliridhiwa, kwa hiyo kutotekeleza mkataba ni kutotekeleza Katiba. Utekelezaji wa Katiba hautakiwi kufumbiwa macho na asiyetekeleza Katiba hatakiwi kuonewa haya,” amesema.

Mgonjwa akiingia chumba cha wagonjwa mahututi, daktari akija atafanya shughuli yake. Kwa sababu hao madaktari tumesema ni wakuu wa nchi, sisi tuna imani nao.

Tunaomba wakuu wa nchi wafanye jukumu lao ili jumuiya hii inusurike. Hatutaki kuamini kwamba watashindwa kufanya jukumu hili tukaona jumuiya inazama; ikizama maana yake madaktari hawajafanya wajibu wao