Msanifu barabara ya njia nane, BRT afariki dunia ajalini, atakavyokumbukwa

Dar es Salaam. Umewahi kupita katika barabara ya njia nane kutoka Kibaha hadi Kimara, ukaona magari yakitiririka kwa mpangilio na kasi na kulifanya Jiji la Dar es Salaam likionekana la kisasa na lenye pumzi mpya?.

Pengine ulifurahia tu safari yako bila kujiuliza, ni nani aliyekaa kimya ofisini akatafakari, akachora mstari wa kwanza wa ramani iliyozaa mradi huo mkubwa na unaoling’arisha Jiji la Dar es Salaam hasa unapoingia na kutoka.

Basi ukae na kujua nyuma ya taswira hiyo ya kisasa alikuwepo mtaalamu mahiri, Humphrey Shoo ambaye pia ni Mwasisi wa Kampuni ya Safi, kabla ya zege kumwagwa na kabla ya mitambo kuvuma, katika barabara hiyo inayoanzia Kimara, Dar es Salaam hadi Pwani, alitumia kalamu, karatasi na fikra makini kufanya usanifu wa mradi huo unaoonekana kiuhalisia.

Kalamu yake ilibeba maono ya kupunguza msongamano wa magari, kuunganisha watu na biashara na kuipa Dar es Salaam sura inayostahili kulingana na hadhi yake ‘jiji la kibiashara’. Barabara hiyo si njia tu ya kupitisha magari; ni alama ya maendeleo iliyoanzia kwenye ubunifu wa makaratasi na mtaalamu huyo.

Kama haitoshi pia, umewahi kuvuka flay over inayoelekea Mloganzila inayounganisha maisha na matumaini? Kabla halijasimama imara juu ya nguzo zake, basi Shoo alifanya usanifu wake kwa kutumia kalamu na karatasi.

Ingawa kuna kasumba ya kutoaminika kwa wataalamu wazawa, hasa inapokuja miradi mikubwa, kwa Shoo kwake hilo halikuwa tatizo. Yeye ndiye aliyepima ardhi hiyo, akahesabu mizigo, akachambua mtiririko wa maji na changarawe, na kuhakikisha usalama wa maelfu watakaolivuka kila uchao.

Humphrey Shoo, wa tatu kutoka kulia, akiwa katikati ya mazungumzo na baadhi ya wataalamu wenzake katika moja ya miradi aliyowahi kuhusika nayo katika shughuli za usanifu enzi za uhai wake.



Alikuwa sehemu ya kizazi kipya cha wataalamu wazawa waliotafsiri ndoto za Taifa kuanzia kwenye makaratasi na kuwa miundombinu inayoonekana, inayoishi, na inayohudumia wananchi kila siku. Kazi zake hazikupiga kelele.

Kwa masikitiko makubwa, ajali ya barabarani imeondoa uhai wa mtaalamu huyu alipokuwa safarini ya kikazi, baada ya kupata ajali mkoani Lindi. Tukio hilo lilitokea Februari 7, 2026, ambapo watu wawili walifariki dunia kufuatia basi alilokuwa amepanda kuligonga lori kwa nyuma.

Katika ajali hiyo, kati ya wawili hao basi alikuwa Shoo, mtoto mdogo na wengine 12 walijeruhiwa. Kifo chake ni pigo kwa familia, marafiki, na sekta ya ujenzi nchini. Hata hivyo, katika majonzi hayo, mchango wake unaendelea kusimama imara, na wenye thamani, ukiwa umechorwa kwa wino usiofutika.

Ajali kama inavyotokea mara nyingi imekatisha tena maono na matumaini ya mipango ya Watanzania wengi katika kuendelea kuiona Tanzania mpya. Wadau wa sekta hiyo wamemzungumzia na kumuelezea kwa upekee kama mtu aliyekuwa kinara, aliyefanya mambo kwa vitendo na kuthibitisha kuwa wataalamu wa ndani wanaweza.

Mmoja wa wahandisi wa kampuni aliyoanzisha, Dominica Chrispin, amesema kifo chake kimewashtua, kwani amefariki dunia akiwa kwenye safari ya kikazi kwenda mikoa ya Lindi na Mtwara kwa ajili ya ukaguzi wa usalama na ubora wa barabara zilizojengwa.

“Alikuwa anakwenda kuona kama waliojenga wamezingatia ramani zinazoonyesha maeneo hatarishi. Ingawa hakuwa amezoea kusafiri kwa mabasi, siku hiyo alipanda usafiri huo ndipo alipokutana na ajali akiwa barabarani,” amesema.

Amemwelezea alikuwa zaidi ya mhandisi wa kawaida, akitajwa kuwa mtaalamu mwenye uwezo wa hali ya juu aliyekuwa akiaminika na mamlaka mbalimbali kila alikokwenda.

“Shoo alikuwa zaidi ya mhandisi. Alikuwa na akili nyingi, na popote alipokwenda mamlaka ziliridhika bila kuwa na mashaka na uwezo wake. Amehusika kuchora ramani za barabara zote za mwendokasi (BRT),” amesema.

Amemwelezea kuwa alikuwa miongoni mwa wataalamu wa kwanza kubobea katika usanifu wa barabara hizo, akiwa na uzoefu mkubwa alioupata baada ya kupata fursa ya kusoma nje ya nchi.

“Alikuwa mtaalamu wa kwanza kuwa na ujuzi wa kuchora barabara hizo na alipata uzoefu mkubwa kupitia masomo yake ya nje ya nchi. Pia, alihusika katika usanifu wa barabara yenye njia nane,” amesema.

Katika maisha yake ya kazi, Chrispin amesema Shoo alishiriki katika miradi mingi ndani na nje ya Tanzania, ikiwemo Zambia, na alikuwa mtaalamu wa kuandaa ripoti, jambo ambalo ni changamoto kwa wengi katika tasnia hiyo, hasa kwenye miradi ya kimataifa.

“Ameshiriki katika miradi mingi hadi Zanzibar. Alikuwa hodari wa kuandika ripoti na alihusika katika miradi ya mataifa mbalimbali,” amesema.

“Kifo chake ni pigo kubwa. Amefundisha wataalamu wengi na hakuwa mchoyo wa maarifa. Tunamuenzi kwa namna ya kipekee kwa sababu alikuwa mtu mwenye moyo wa kipekee na alithamini mawazo ya wengine,” amesema.

Humphrey Shoo wa kwanza, enzi za uhai wake.



Amesema wataendelea kuuenzi mchango wake kwa kuhakikisha kampuni aliyoianzisha inaendelea kusimama imara.

“Hakuwa mtu wa tamaa. Tutamuenzi kwa kuhakikisha kampuni aliyoianzisha inadumu na miradi yote aliyoianzisha inaendelea,” amesema.

Mtaalamu kutoka kampuni ya Estim iliyojenga barabara ya Kimara hadi Kibaha, Fred Nyenga, amesema kifo cha mhandisi huyo ni pigo kubwa kwa sekta ya ujenzi wa barabara, hususan miradi ya Mabasi ya Mwendokasi (BRT).

Nyenga amesema marehemu alikuwa nguzo muhimu katika usanifu wa barabara za BRT, akieleza kuwa miradi hiyo ina changamoto nyingi zinazohitaji utaalamu wa hali ya juu.

“Barabara za BRT ujenzi wake una changamoto; ukikosea unalazimika kumuita aje kurekebisha. Tunaweza kupata mbadala, lakini kumpata kama yeye ni changamoto,” amesema.

Amesema marehemu alikuwa msanifu mahiri wa barabara na madaraja, aliyebobea katika kupanga miundombinu kwa kuzingatia mahitaji ya wananchi.

Alibuni ramani ya barabara ya njia nane kutoka Kimara hadi Kibaha na kuamua maeneo ya vituo kulingana na idadi ya watu katika maeneo husika.

“Alikuwa miongoni mwa timu ya kwanza kuchora ramani za Mabasi ya Mwendokasi na alihusika pia katika kuweka alama za usalama barabarani kupitia kampuni yake ya Safi,” amesema Nyenga.

Mbali na hilo, alishiriki kuchora ramani za barabara za Mji wa Serikali Mtumba pamoja na miradi mingine kwa kushirikiana na wataalamu wengine.

Nyenga amesema licha ya mchango wake mkubwa, marehemu alikuwa mtu wa kawaida asiyejipambanua wala kujitangaza.

“Kwa wataalamu wa barabara alikuwa mtu mkubwa sana. Tulipokwama, tulimfuata yeye na alikuwa tayari kumkaribisha mtu yeyote,” amesema.

Ameongeza marehemu alisanifu madaraja mengi katika mkoa wa Dar es Salaam na alitoa mchango mkubwa katika utekelezaji wa miradi ya BRT kuanzia lot ya kwanza hadi ya nne.

“Kampuni yetu tumeshirikiana naye katika miradi mingi, ikiwemo barabara ya njia nane. Alikuwa anachora na kushauri maeneo ya kuweka makutano,” amesema.

Akizungumzia fly over ya Mloganzila, Nyenga amesema awali walishindwa kuelewa maelekezo yake, lakini aliwasisitiza kuendelea na ujenzi kama alivyoshauri baada ya kukamilika, walithibitisha ubora na uhalisia wa maono yake.

Kwa mujibu wa Nyenga, hata ajali iliyosababisha kifo chake mkoani Lindi ilitokea akiwa katika harakati za kwenda kukagua kazi mpya, akionesha namna alivyokuwa amejitoa kwa kazi yake hadi dakika za mwisho wa maisha yake.

Meneja wa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura) mkoani Dar es Salaam, Godfrey Mkinga, amemuelezea kama mtaalamu aliyefanya usanifu barabara za mji wa Serikali na Dar es Salaam, ameshiriki usanifu barabara za mradi wa maendeleo ya jiji la Dar es Salaam (DMDP), kwa barabara za wilaya ya Ubungo na Kinondoni.

Humphrey Shoo mwenye jaketi rangi ya machungwa



“Kiukweli alikuwa kinara, kama tasnia tumepoteza mtu ambaye alikuwa bado na mchango wake ulikuwa unahitajika. Alikuwa wa kupenda maendeleo ya wengine na mtu anayesema Watanzania tunaweza,”amesema.

Amesema ameshiriki ujenzi wa barabara nane na ni mtu aliyekuwa nguli na kuifahamu kazi na maendeleo “Katika tasnia ya ujenzi tuna msiba mzito na tunasema tutamuenzi vizuri.”

Shoo, ambaye ameacha mke na watoto watatu wa kiume, anatarajiwa kuzikwa leo, katika makaburi ya Kondo Ununio, jijini Dar es Salaam ibada ya kuaga mwili itafanyika  katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Msasani, Jijini Dar es Salaam.