Na Mwandishi Wetu, Ngorongoro.
Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya eneo la Ngorongoro (NCAA) Bw. Abdul-Razaq Badru ameongoza kikao cha kimkakati kilichojumuisha waheshimiwa Madiwani, Viongozi wa Mila, watendaji wa kata, wenyeviti wa Vijiji na watendaji wa vijiji kwa lengo la kudumisha mahusiano na uboreshaji wa huduma za kijamii na uboreshaji wa shughuli za Uhifadhi shirikishi.
Kamishna Abdul-Razaq Badru ameeleza kuwa kikao hicho ni sehemu ya mkakati wa Mamlaka hiyo kukutana na makundi mbalimbali kujadili uboreshaji wa shughuli za kijamii na huduma za wananchi kama Maji, shule, Malisho, barabara, mawasiliano, afya na mengineyo.
“Viongozi na Wananchi wa Tarafa ya Ngorongoro ni wadau muhimu katika hifadhi, tunakutana nao kama sehemu ya kuboresha uhusiano na kuwaeleza mikakati ya Serikali dhidi yao.
kwa sasa tunaboresha miundombinu ya huduma za maji, ujenzi wa Barabara kwa tabaka gumu kutoka Loduare hadi Golini, kujenga minara mipya ya mawasiliano 9 ndani ya hifadhi ili kufikisha huduma kwa wananchi na wadau mbalimbali” amefafanua Kamishna Badru.
Kwa upande wa Viongozi waheshimiwa Madiwani, viongozi wa Mila wameiomba Serikali kupitia Mamlaka hiyo kuendelea kuboresha mahusiano, huduma za kijamii kama miundombinu ya Maji, barabara, ukarabati wa vituo vya afya na shule, mahitaji ya baraza la wafugaji, chunvi za mifugo na mpango wa malisho ya mifugo hawa wakati wa kiangazi.










