Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema tatizo la wanafunzi kukosa madawati na kukaa chini si uhaba wa fedha bali ni ukosefu wa mipango madhubuti ya muda mrefu. Amesema viongozi wanapaswa kuwa na makadirio ya miaka 10 hadi 15 mbele ili kujua idadi ya wanafunzi na mahitaji yao.
Akizungumza leo Februari 12, 2026 katika ziara ya kukagua miradi wilayani Kinondoni, ikiwemo Shule ya Abbas Tarimba na Hospitali ya Shifaa, Chalamila amesema bado kuna mianya ya ukusanyaji mapato na ni lazima viongozi wakabane matumizi na kuongeza uwekezaji kwenye elimu. Amesisitiza pia ushiriki wa sekta binafsi kupitia uwajibikaji wa kijamii (CSI) kusaidia ujenzi wa miundombinu ya shule.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila akizungumza leo Februari 12, 2026 kwenye muendelezo wa ziara yake anayoifanya wilaya ya Kinondoni kukagua miradi ya ujenzi ambapo leo ametembelea shule ya Abbas Tarimba iliyopo Tandale.
Ameelekeza viongozi kujipanga kutokana na ongezeko la wanafunzi na changamoto ya ardhi, akipendekeza ujenzi wa shule za maghorofa na mabweni ili kupunguza msongamano na wanafunzi kuchelewa kurudi nyumbani.
Meya wa Kinondoni, Songoro Mnyonge amesema ujenzi wa shule ya ghorofa Tandale umetokana na uhaba wa ardhi, huku Mkurugenzi Hanifa Hamza akibainisha kuwa eneo hilo linaongezeka watu na linahitaji huduma zaidi za kijamii. Shule ya Abbas Tarimba inajengwa kwa gharama ya Sh3.3 bilioni, ambapo Sh1.8 bilioni tayari zimepokelewa.
Katika hatua nyingine, Chalamila amewataka viongozi kuimarisha ushirikiano na sekta binafsi ili kukuza uwekezaji, hususan katika huduma za afya kuelekea Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila akizungumza leo Februari 12, 2026 kwenye muendelezo wa ziara yake anayoifanya wilaya ya Kinondoni kukagua miradi ya ujenzi ambapo leo ametembelea shule ya Abbas Tarimba iliyopo Tandale.