::::::::::
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania Dkt. Aneth Komba amesema, Serikali imetoa vitabu vya masomo ya Elimu ya Amali bure kwa shule zote za umma na binafsi ili kuongeza hamasa katika ufundishaji na ujifunzaji wa masomo hayo yatayosaidia kukabiliana na changamoto ya ajira kwa mwanafunzi pindi wanapohitimu.
Dkt. Komba amesema hayo leo Februari 12, 2026 katika zoezi la ugawaji wa vitabu vya Amali kwa wakuu wa shule zote Tanzania Bara ambazo zinatoa Elimu ya Sekondari katika mkondo huo.
Amesema, mwaka 2024 Serikali ilianza kutekeleza Mtaala uliobereshwa ambao umegawanyika katika mkondo wa Amali na mkondo wa jumla, huku akisisitiza mkondo wa Amali lengo lake ni kujenga Elimu ujuzi kwa mwanafunzi.
Sambamba na ugawaji wa vitabu vya Amali, Dkt. Komba amesema, TET imetoa mafunzo kwa wakuu wa shule wote kuhusu maboresho yaliyofanyika kwenye Mtaala hasa katika mkondo wa Amali, pamoja na namna kutumia Maktaba mtandao ambapo vitabu vyote hupatikana.
Aidha, Dkt Komba amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha zilizosaidia upatikanaji wa vitabu nchini, hasa vitabu vya Amali ambavyo vinagawiwa bure kwa shule zote nchini za Serikali na za binafsi.
Nae, Meneja uchapaji na usambazaji wa vitabu Taasisi ya Elimu Tanzania Bw. Emmanuel Stanslaus ametoa wito kwa walimu kuhakikisha wanatua vitabu hivyo kwa usahihi ili vilete tija kwa wanafunzi kulingana na fani wanazosoma.
Kwa upande wake Mkuu wa shule ya ufundi Nzega na Makamu Mwenyekiti wa wakuu wa shuke Tanzania Bara Mwl. Mwanakombo Juma Martin amesema vitabu hivyo vilivyotolewa bure kwa shule za Serikali na binafsi vitasaidia katika ufundishaji na ujifunzaji kwa wanafunzi hivyo kuleta tija katika utekelezaji wa Mtaala ulioboreshwa mkondo wa Amali.
Nae, Mkuu wa shule ya Ufundi ya wavulana Bwiru iliyopo Mkoani Mwanza Mwl. Thomas Werema amesema Elimu ya Amali inaenda kuwa Mkombozi kwa vijana wa Tanzania, kwani hutoa fursa kwa mw anafunzi kujiajiri, kuajiriwa au kuajiri wengine pindi amalizapo masomo yake, hivyo kusaidia kukabiliana na changamoto ya ajira nchini.









