Tume ya maadili viongozi wa umma yapokea kesi 95 za uasharati, udhalilishaji kazini

Unguja. Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma imepokea kesi 95 kutoka kwa watumishi wa umma zikihusiana na uasherati, udhalilishaji wa kijinsia, rushwa na matumizi mabaya ya madaraka. 

Kesi nyingine zinazohusiana na tabia zisizofaa zilizopokewa kwa kipindi cha miaka mitano ni pamoja na upendeleo katika ajira, kushindwa kulipa madeni, uonevu, utapeli, lugha za matusi, kutelekeza familia, ucheleweshaji wa utoaji wa haki, unyanyasaji, mgongano wa kimaslahi na tuhuma za rushwa. 

Kati ya kesi hizo, 73 zimetolewa uamuzi, huku nyingine 22 zikiwa bado zinaendelea na uchunguzi.  

Hayo yamebanishwa leo Alhamisi, Februari 12, 2025 na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman wakati akijibu maswali ya wawakilishi katika mkutano wa baraza la wawakilishi unaoendelea Chukwani Zanzibar. 

Katika swali la msingi alilouliza Mwakilishi wa Ole, Seif Hamad Suleiman, ametaka kujua kesi ngapi zimeripotiwa na wananchi katika kipindi cha miaka mitano ya hivi karibuni na kesi ngapi kati ya hizo zimetolewa uamuzi. 

Pia amehoji ikiwa kuna kiongozi yeyote aliyetiwa hatiani na Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa kukiuka sheria au maadili ya umma.

“Ni kweli kwamba baadhi ya viongozi walionekana na Tume ya maadili kuwa wamevunja maadili kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma. 

“Kwa kipindi cha miaka mitano (2020/21 hadi 2024/25), jumla ya viongozi 50 walionekana kuvunja maadili. Uamuzi wa Tume kwa viongozi hao uliwasilishwa katika mamlaka husika za uteuzi na kinidhamu kwa ajili ya kuchukuliwa hatua,” amesema Waziri Haroun.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, viongozi hao walipewa adhabu ya onyo na tahadhari kutoka mamlaka zao za uteuzi na kinidhamu kwa mujibu wa kifungu cha 30 (a) cha sheria ya maadili ya viongozi wa umma. 

Kwa viongozi waliochelewa kurejesha fomu zao kwa wakati uliowekwa kisheria, kwa kipindi hichohicho, Waziri Haroun amesema jumla ya viongozi 144 walichelewa, kati ya hao 46 walionekana kuvunja maadili ya viongozi wa umma kwa kosa la kuchelewa kurejesha fomu. 

“Viongozi hao walipewa adhabu ya onyo na tahadhari kutoka mamlaka zao za uteuzi na kinidhamu kwa mujibu wa kifungu cha 30 (a) cha sheria ya maadili ya viongozi wa umma,” amesema.

Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma ni Taasisi iliyoanzishwa kwa mujibu wa sheria ya maadili ya viongozi wa umma, nambari 4 ya mwaka 2015 na imepewa mamlaka ya kusimamia maadili ya viongozi wa umma. 

Mamlaka hayo yanajumuisha kupokea, kuchunguza na kushughulikia malalamiko, tuhuma au madai kuhusu uvunjwaji wa sheria ya maadili ya viongozi wa umma pamoja na kusikiliza na kutoa uamuzi kuhusu madai yoyote ya uvunjwaji wa maadili.