Uhamiaji yashtukia waoaji na waolewaji na wahamiaji nchini

Kishapu. Idara ya Uhamiaji wilayani Kishapu mkoani Shinyanga imetoa elimu kwa walimu na wanafunzi wa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) Kishapu kuhusu masuala ya uhamiaji, uraia, pasipoti na hati za safari, sambamba na kampeni ya ‘Mjue Jirani Yako,’ ikiwa ni sehemu ya kuimarisha usalama wa nchi na kuwajengea vijana uelewa wa sheria.

Akizungumza leo Alhamisi, Februari 12, 2026, chuoni hapo, Kaimu Ofisa wa Uhamiaji wilayani Kishapu, Robert Mahenge, amesema wapo baadhi ya wageni wasiokuwa raia wa Tanzania wanaoingia nchini kwa njia zisizo halali na kujihusisha na shughuli za kiuchumi kinyume cha sheria.

“Wapo wageni wasiokuwa raia wa Tanzania wanaingia nchini kwa njia zisizo halali kwa lengo la kuoa au kuolewa na kisha kushiriki shughuli za kiuchumi kama kilimo na ufugaji bila kufuata sheria. Wananchi wanaoingia kwenye mahusiano au kuajiri raia wa kigeni wanapaswa kupata mwongozo kutoka Ofisi za Uhamiaji ili kuepuka kuvunja sheria bila kujua,” amesema Mahenge.

Ameongeza kuwa uzalendo ni nguzo muhimu katika kulinda usalama wa taifa, akiwataka walimu na wanafunzi kuwa mabalozi wazuri kwa jamii kwa kutoa taarifa sahihi wanapobaini uwepo wa wageni wasiokuwa na vibali halali.

Katika picha ni wanafunzi wa Chuo cha ufundi Stadi (VETA) wakisoma nakala ya Uhamiaji. Picha na Hellen Mdinda



“Usalama wa nchi unaanzia kwa mwananchi mmoja mmoja. Tunaposhirikiana na mamlaka husika, tunalinda ajira zetu, rasilimali zetu na mustakabali wa taifa letu,” amesisitiza.

Katika elimu hiyo, wanafunzi pia wameelezwa umuhimu wa kuwa na pasipoti na hati za safari mapema kama maandalizi ya kutumia fursa za ajira, masomo au biashara nje ya nchi. Gharama ya pasipoti ni Sh150,000, huku hati ya safari ya dharura ikigharimu Sh20,000.

Kwa niaba ya wanafunzi, Gloria Justus Dominick, anayesomea fani ya umeme, amesema mafunzo hayo yamewapanua uelewa kuhusu wajibu wao katika kulinda taifa.

“Mbali na taaluma tunazosoma, tumeelewa kuwa hata kuoa au kuolewa na mhamiaji kunahitaji kufuata mwongozo wa kisheria. Sisi vijana ni kundi kubwa, hivyo tunapaswa kusaidia kuelimisha wengine kuhusu masuala ya uhamiaji na usalama,” amesema Dominick.

Ofisa Uhamiaji na Mkaguzi wa uhamiaji wilayani Kishapu mkoani Shinyanga Robert Mahenge (Katikati) pamoja na wanafunzi wa VETA Halmashuri ya wilaya ya Kishapu pamoja na wakufunzi. Picha na Hellen Mdinda



Kwa upande wake, mkufunzi Domician Mjuni, akizungumza kwa niaba ya uongozi wa chuo hicho, ameishukuru Idara ya Uhamiaji kwa kufika chuoni hapo na kutoa elimu, akisema imeongeza uelewa kwa walimu na wanafunzi kuhusu sheria na taratibu za uhamiaji.

Amesema chuo kitaendelea kushirikiana na Ofisi ya Uhamiaji kwa kutoa taarifa za wanafunzi raia wa kigeni na kuhakikisha taratibu zote zinafuatwa kwa mujibu wa sheria, hatua itakayosaidia kudhibiti wahamiaji haramu katika Wilaya ya Kishapu.