Dar es Salaam/Dodoma. Wadau wa sekta za usafirishaji na uzalishaji wametoa wito wa kuboreshwa kwa mifumo ya usajili wa bajaji na pikipiki zinazotumia umeme (EVs), wakitaka Serikali kutumia uzoefu wa nchi zilizoendelea kiteknolojia ili kuiongoza nchi katika kipindi cha mpito kuelekea matumizi ya nishati safi.
Wadau hao walitaja mataifa yaliyopiga hatua katika matumizi ya vyombo hivyo vya usafiri vinavyotumia umeme, ikiwemo Uganda, Kenya, Rwanda, India na Ufilipino.
Ushauri wao unaonyesha kuwa Tanzania siyo nchi pekee inayokabiliana na changamoto zinazohusiana na vyombo vya usafiri vinavyotumia umeme, hususan katika kipindi hiki cha mpito kuelekea kwenye teknolojia mpya.
Hata hivyo, tofauti na baadhi ya nchi hizo, Tanzania inakabiliwa na ugumu wa kudhibiti vyombo hivyo vya usafiri, hususan bajaji na pikipiki, licha ya kuwepo kwa sheria na kanuni, pengo linalozua wasiwasi wa kiusalama.
Maoni ya wataalamu hao yanatokana na uchunguzi uliofanywa na gazeti la Mwananchi kati ya Oktoba na Desemba 2025 katika miji ya Dodoma na Dar es Salaam ili kubaini ukubwa wa tatizo hilo.
Uchunguzi huo umebaini kuongezeka kwa idadi ya vyombo vya magurudumu mawili na matatu vinavyotumia umeme vinavyoendesha shughuli zake katika miji hiyo, hali inayoongeza hofu ya ajali na uhalifu miongoni mwa watembea kwa miguu na watumiaji wengine wa barabara.
Hii ni kinyume na Kifungu cha 57(b)(I–IV) cha Sheria ya Marekebisho ya Kodi ya Usajili na Uhamisho wa Magari, Sura ya 124 ya mwaka 2023, ambacho kinatambua uwepo wa vyombo vya usafiri vinavyotumia nishati ya umeme, ikiwa ni pamoja na pikipiki na bajaji, katika mfumo wa kisheria wa Tanzania.
Pia, inakiuka Sheria ya Usalama Barabarani, Sura ya 168, hasa Kanuni za Marekebisho ya Usajili wa Magari za mwaka 2025, ambazo zilianzisha vifungu vidogo 1A (a)–(d).
Vifungu hivi vinaweka ada za leseni za magari zinazotozwa wakati wa utoaji wa cheti cha usajili kwa vyombo vinavyotumia umeme.
Ada hizo zimegawanywa katika makundi matatu: EVs za Nguvu Ndogo (chini ya 50kWh), EVs za Nguvu ya Kati (50.1–100kWh) na EVs za Nguvu Kubwa (100.1–200kWh).
Kanuni hizo, zilizotangazwa rasmi tarehe 26 Juni 2025 na kutiwa saini na aliyekuwa waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa, zinaweka ada za usajili za Sh50,000, Sh200,000 na Sh250,000 kwa madaraja ya 1, 2 na 3 mtawalia, huku Sh300,000 zikihusika kwa EVs za utendaji wa juu.
Kifungu kidogo cha 1B kinaeleza kuwa ada ya leseni ya pikipiki, iwe ya umeme au ya kawaida, ni Sh30,000, wakati ile ya bajaji inayobeba mizigo au abiria ni Sh50,000.
Hata hivyo, Kifungu cha 13(1) na (2) cha Sheria ya Usalama Barabarani, Sura ya 168, kinakataza matumizi ya gari au trela yoyote kwenye barabara za Tanzania pasipo kusajiliwa.
Kifungu cha 13(2) kinasema kwamba mmiliki au dereva yeyote anayeendesha gari lisilosajiliwa anafanya kosa, hivyo kustahili faini isiyozidi Sh50,000, kifungo cha hadi miaka mitano au vyote viwili, na chombo chake kinaweza kutaifishwa na Serikali.
Hali ya sasa pia inakiuka Mpango Mkakati wa Taifa wa Usalama Barabarani wa 2024/25–2026/27 na ahadi ya Tanzania katika Muongo wa Dunia wa Hatua za Usalama Barabarani 2021–2030.
Pia, Umoja wa Mataifa kupitia Shirika la Afya Duniani (WHO) umelenga kupunguza vifo na majeruhi wanaotokana na ajali za barabarani kwa angalau asilimia 50 ifikapo 2030.
Katika tangazo la Mei 2025, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilielekeza usajili wa lazima wa vyombo hivyo vinavyotumia nishati ya umeme, ikiweka ukomo wa Juni 2025, lakini utekelezaji wake chini ya Sheria ya Usalama Barabarani ya mwaka 1973 umeendelea kukumbwa na changamoto.
Kutokana na hali hiyo, magari mengi ya magurudumu mawili na matatu yanayotumia nishati ya umeme yanayofanya shughuli zake Dar es Salaam na Dodoma bado hayajasajiliwa, hali inayotia wasiwasi wa kuwepo kwa ajali na uhalifu barabarani.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazeti hili, wadau na wataalamu hao walisisitiza umuhimu wa watumiaji kuzingatia sheria, sambamba na kuanzishwa kwa sera mpya zitakazoongoza sekta ya EVs na kuhimiza kuzingatiwa kwa muda wa mpito kuelekea nishati safi.
Wakieleza uzoefu wa Uganda, walisema nchi hiyo imejenga mazingira yanayounga mkono mfumo wa EVs kupitia motisha za kifedha na uwekezaji katika miundombinu, hatua iliyorahisisha matumizi ya pikipiki na bajaji zinazotumia nishati ya umeme.
Walisema Kenya imeainisha bajaji za umeme kama vyombo vya moto, hivyo kufanya usajili na utoaji wa leseni kuwa wa lazima.
Rwanda, waliongeza, imejumuisha EVs katika sera yake ya kitaifa ya usafirishaji, ikihakikisha pikipiki na bajaji zinazotumia umeme zinakidhi viwango vya usalama vya vipuri pamoja na betri.
Pia, walibainisha kuwa India imeunda kundi maalumu la riksha za umeme, hatua inayowezesha mamlaka kutekeleza kanuni kwa urahisi kwa kutumia namba za kijani, huku Ufilipino ikifuatilia waendeshaji kupitia vyama vya ushirika na mifumo ya ndani ya usajili.
Wadau hao waliongeza kuwa China ndilo soko kubwa zaidi la magari yanayotumia nishati ya umeme duniani, ikichangia zaidi ya asilimia 40 ya mauzo mapya ya magari hayo.
Walisema nchi hiyo imeanzisha namba za kijani kuashiria matumizi ya nishati safi, huku Ujerumani ikitoa namba kama hizo kwa EVs ili kukuza uendelevu.
“Kuhusu usajili, taasisi husika zinapaswa kuendelea na mchakato ili EVs zishughulikiwe kama vyombo vingine vya moto,” alisema mdau wa usafirishaji kutoka Kampuni ya Kainew Investment na Meneja Mkuu, Stanislaus Ndunguru.
Ndunguru, ambaye kiwanda chake kipo wilayani Mkuranga mkoani Pwani, alisema kimekuwa kikiunganisha magari ya umeme kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa, na kwamba kimeanza kuunda vyombo vya magurudumu matatu.
Aliiomba Serikali kupunguza Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa vyombo hivyo ili kupunguza gharama za uendeshaji, kuongeza uwezo wa kumudu na kusaidia uhamaji kuelekea kwenye nishati safi.
Ripoti ya Africa E-Mobility 2025: Trends, Policies and Investments in Electric Mobility inaonyesha Afrika Mashariki inaongoza soko la vyombo vya magurudumu mawili na matatu, huku Tanzania ikiibuka kinara.
Ripoti hiyo inasema pikipiki za umeme za kibiashara ndizo zinazoongoza kwa kutumiwa zaidi kutokana na upatikanaji wake sokoni, hali inayoiweka Afrika katika nafasi nzuri ya ukuaji na uhamaji wakati huu dunia ikihamia kwenye EVs.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kazimoto Mapikipiki Ltd yenye makao yake Dodoma, Gaudence Kazimoto, alisema Tanzania inaweza kuiga mifumo hiyo ili kuhimiza matumizi ya nishati safi.
“Katika safari zangu nje ya nchi, nimeona mataifa mengi yakitoa namba za kijani kwa magari yanayotumia nishati ya umeme. Hii inaashiria matumizi ya nishati safi na kuhimiza matumizi pamoja na uendelevu wake,” alisema mwagizaji na mwendeshaji huyo mzoefu.
Akiwa na uzoefu wa miaka mitatu katika teknolojia ya EVs, Kazimoto alisema: “Kadri muda unavyoenda, uelewa na kukubalika vinaongezeka kupitia watumiaji wanaoshirikishana uzoefu. Leo, mahitaji ya pikipiki na bajaji zinazotumia nishati ya umeme yameendelea kuongezeka.”
Mkurugenzi wa Masoko na Mauzo wa Kiira Motors Corporation, Jerome Ayazika, akitoa uzoefu wa Uganda, alisema nchi hiyo imeanzisha namba nyeupe kwa vyombo vya usafiri vinavyotumia nishati ya umeme na kwamba inajipanga kuanza kutumia namba za kijani katika bajeti ijayo ili kuhimiza matumizi ya nishati safi.
“Misamaha ya kodi na ruzuku huchochea uunganishaji wa vyombo hivi ndani ya nchi. Hivyo, misamaha ya ushuru wa kuagiza vipuri, VAT kwa vipengele muhimu na likizo ya kodi ya mapato kwa miaka mitano ni muhimu kwa maendeleo ya sekta hii,” alishauri.
Ayazika alisema uhamasishaji wa umma ni muhimu, akisisitiza elimu kwa wananchi kuhusu faida za EVs, kushughulikia dhana potofu na kuwekeza katika miundombinu ya kuchaji betri.
Alibainisha kuwa Uganda ina zaidi ya vituo vitano vya kuchaji betri za mabasi na vituo vingine 200 vya kuchaji betri za pikipiki, huku mipango ya upanuzi ikiendelea.
Aidha, aliishauri Tanzania kuandaa sera na mkakati jumuishi wa uhamaji kuelekea vyombo vya usafiri vinavyotumia nishati ya umeme ili kurahisisha kanuni na uendeshaji wa sekta hiyo.
“Mfumo wa pamoja wa udhibiti wa Uganda unahimiza uzalishaji wa ndani na kurahisisha utii wa sheria, masomo ambayo Tanzania inaweza kuyatumia katika kipindi cha mpito kuelekea nishati safi,” alisema.