Zimbabwe kubadilisha katiba kuongeza muda wa Rais madarakani

Harare. Baraza la Mawaziri la Zimbabwe limepitisha rasimu ya mabadiliko ya Katiba ya nchi hiyo, yatakayomwezesha Rais Emmerson Mnangagwa (83) kuendelea kubaki madarakani hata baada ya muda wake kwisha mwaka 2028.

Rasimu hiyo inapendekeza kwamba marais watakuwa wanachaguliwa na wabunge na siyo kuchaguliwa moja kwa moja na wananchi, na atatumikia mihula miwili ya miaka saba kila mmoja, tofauti na miaka mitano mitano ya sasa.

Kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), Waziri wa Sheria, Ziyambi Ziyambi amesema watafanya mashauriano na wadau mbalimbali kabla muswada haujawasilishwa bungeni kujadiliwa, ikizingatiwa kwamba mabunge yote yametawaliwa na wabunge wengi wa chama tawala cha Zanu PF.

Changamoto za kisheria zinatarajiwa kuibuka huku wataalamu wa katiba wakisisitiza kuwa kura ya maoni ni lazima iwapo ukomo wa mihula ya urais utabadilishwa na wanakumbusha kuwa marekebisho hayo hayawezi kumnufaisha rais aliyeko madarakani.

Mnangagwa, aliyeingia madarakani mwaka 2017 kufuatia mapinduzi ya kijeshi yaliyomwondoa kiongozi wa muda mrefu, Robert Mugabe alishinda uchaguzi wa urais mwaka uliofuata na kisha kuchaguliwa tena kwa muhula wa pili mwaka 2023, ingawa matokeo hayo yalipingwa na wapinzani.

Mnangagwa maarufu kwa jina la utani mamba kutokana na ustadi wake wa kisiasa, muhula wake wa mwisho wa miaka mitano unatarajiwa kumalizika mwaka 2028.

Katika kura ya maoni iliyofanyika miaka 13 iliyopita, Wazimbabwe walipiga kura kwa wingi kuidhinisha katiba mpya iliyoanzisha ukomo wa mihula ya urais, wakati ambao Mugabe alionekana kuwa amejikita madarakani akiwa ameiongoza nchi hiyo tangu ipate uhuru mwaka 1980.

Dalili kuwa Mnangagwa, aliyewahi kuwa makamu wa rais wakati wa Mugabe kabla ya wawili hao kuhitilafiana kutokana na kuongezeka kwa ushawishi wa kisiasa wa aliyekuwa mke wa rais, alitaka kusalia madarakani zaidi ya mwaka 2028 zilianza kujitokeza miaka miwili iliyopita.

Kaulimbiu ya “2030 bado ni yeye” ilianza kusikika katika mikutano ya Zanu-PF huku wafuasi wake wakidai anapaswa kubaki madarakani ili kukamilisha mpango wake wa maendeleo wa Ajenda 2030, japokuwa Rais Mnangagwa mwenyewe alikanusha hadharani azma hiyo.

Ndani ya Zanu-PF, amekabiliwa na wakosoaji, lakini mkosoaji wake mkuu, Blessed Geza maarufu kama “Bombshell”, alifariki dunia wiki iliyopita.

Wakati kama huu mwaka uliopita, Geza, mpiganaji mkongwe wa vita vya ukombozi miaka ya 1970 na aliyekuwa mjumbe wa Kamati Kuu yenye ushawishi mkubwa ya Zanu-PF, alianzisha mashambulizi makali kwa kile alichokitaja kuwa ni azma ya Mnangagwa kubaki madarakani baada ya 2028.

Aliomba radhi kwa kusaidia kumuingiza madarakani na kumshutumu rais huyo kwa upendeleo wa kifamilia katika jitihada za kuendeleza utawala wake.

Zanu-PF ilimfukuza Geza kwa tuhuma za kukosa utii na alilazimika kujificha. Hata hivyo, aliendelea kupata uungwaji mkono mkubwa kwenye mitandao ya kijamii, ambako alikuwa akichapisha mara kwa mara video akihamasisha maandamano.

Saa chache kabla ya kifo chake, ujumbe uliowekwa kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii uliwahimiza Wazimbabwe kuendeleza “vita ya heshima” ya kumuondoa Rais Mnangagwa na “kukomesha uporaji wa nchi yetu.”

Geza alikuwa Afrika Kusini wakati familia yake ilipotangaza kifo chake Ijumaa.

“Katika wakati ambao kunyamaza kungekuwa rahisi zaidi, alichagua kuzungumza dhidi ya rushwa na upendeleo wa kifamilia vinavyoendelea kudhoofisha ahadi ya uhuru,” alisema Andrease Ethan Mathibela, mwenyekiti wa kitaifa wa chama chenye ushawishi cha Zimbabwe National Liberation War Veterans Association.

Serikali sasa inaendelea kusukuma mbele ajenda ya 2030 ya Mnangagwa na imesema lengo la muswada wa sheria uliopendekezwa ni kuimarisha utawala bora na kuleta uthabiti wa kisiasa.