Unguja. Mahakama Kuu ya Zanzibar imetupilia mbali maombi yaliyowasilishwa na waliokuwa wagombea Uwakilishi wa ACT- Wazalendo kutoka majimbo 19 ya Unguja baada ya kukubaliana na pingamizi la wajibu maombi kwamba wakili aliyesaini kiapo kwenye maombi hayo hana leseni ya viapo.
Wagombea hao walipeleka ombi la zuio kwa hati ya dharura kufuatia tangazo la Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kwa umma likielezea nia ya kuteketeza nyaraka zote za uchaguzi wa mwaka 2025.
Ombi la zuio lilipelekwa mahakamani tayari kukiwa pia kuna ombi jingine la kugundua uwepo wa nyaraka mbalimbali na kupatiwa nakala hizo.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya upande wa wajibu maombi (Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Tume ya Uchaguzi Zanzibar) kabla ya kuanza kusikilizwa kuweka pingamizi kwamba wakili aliyesaini hati hizo licha ya kwamba ana sifa ya uwakili lakini hana leseni ya viapo, kwa hiyo hana sifa na kuomba Mahakama iyatupilie mbali.
ACT-Wazalendo imeendelea kukumbwa na mapigo ya kisheria baada ya Mahakama Kuu ya Zanzibar kutupilia mbali kesi hiyo. Awali, kesi 14 zilizokuwa zimewasilishwa kupinga matokeo ya uchaguzi wa wabunge katika majimbo ya Pemba, zilitupiliwa mbali.
Januari 29, 2026, kesi nyingine 19 za waliokuwa wagombea ubunge wa ACT-Wazalendo zilizokuwa zikipinga matokeo ya ubunge katika majimbo 19, pia, zilitupiliwa mbali.
Akitoa uamuzi wake leo Februari 13, 2026 mahakamani hapo, Jaji Salma Hassan amekubaliana na hoja hiyo akisema, Mahakama imejiridhisha kwamba wakili huyo hana leseni ya viapo.
Akizungumzia uamuzi huo wa Mahakama, Katibu wa Habari, Uenezi, Mawasiliano na Umma, ACT-Wazalendo, Salim Bimani amesema baada ya kufutwa kwa shauri hilo, wamefungua upya maombi kwa hati ya dharura.
“Dakika chache baada ya maombi hayo kuondolewa, tayari tumeshafungua upya maombi hayo kwa Hati ya Dharura katika Mahakama Kuu yaZanzibar, yakisajiliwa kama Maombi Madogo namba 19 ya Mwaka 2026 tukiwa tumerekebisha kasoro zote zilizodaiwa,” amesema Bimani.
Amesisitiza kwamba wanawatoa hofu wanachama wao na Wazanzibar kwa kuwa wamejipanga kuvuka kila kizingiti cha kisheria kitakachowekwa mbele yao. Amesema hawataruhusu hata karatasi moja ya kura ipotee au kuchomwa moto mpaka haki
Mkuu wa Kurugenzi ya Huduma za Sheria wa ZEC, Maulid Ame Mohamed amesema Mahakama imebaini kasoro kwa kusimamia hoja yao kwani wakili huyo hakuwa na sifa.
“Sheria inamkataza wakili kufanya kazi za kisheria ikiwemo kuwawakilisha watu mahakamani na kutengeneza nyaraka mbalimbali za kisheria kama viapo. Mahakama leo imejiridhisha na imeyafuta, kwa sasa hakuna zuio lolote la kuteketeza nyaraka zile ambazo zilitumika wakati wa uchaguzi mkuu,” amesema.
Maombi madogo ya madai namba 18 ya mwaka 2026 yalifunguliwa Ijumaa Februari 6, 2026 chini ya hati ya dharura.
Februari 10, 2026 Mahakama Kuu Tunguu kabla haijaanza kusikiliza hoja za wajibu maombi, iliweka pingamizi kuhusu hati hiyo ikidai aliyeapa licha ya kuwa ni wakili, hana sifa kwa sababu hana leseni ya kamishna wa kiapo.
Akifafanua kuhusu hilo, Wakili wa Serikali Mkuu kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Said Salim Said alidai kuwa watawasilisha mapingamizi matano chini ya kifungu namba 129 sura ya nane ya sheria za Zanzibar. Hata hivyo, waliwasilisha hoja moja ikawekewa pingamizi na ikitosha kuyatupilia mbali maombi hayo.
Amesema katika kifungu cha 38 (1) kimeeleza wazi kwamba ni kosa mawakili kujitambulisha mtaalamu wa sheria bila kuwa na leseni.
“Kwa msingi huo, hati ya kiapo iliyowasilishwa mahakamani imeapiwa na wakili Ussi Khamis Haji Februari 5, 2026 kama yeye ni kamishna wa kiapo, akaweka tarehe na kusaini akijua hana leseni,” amedai.
“Unaweza kuwa wakili lakini usiwe kamishna wa viapo, tofauti na Tanzania Bara, mtu anaweza kuwa wakili, moja kwa moja anakuwa kamishna lakini sisi (Zanzibar) sheria ipo wazi sana.”
Katika kuthibitisha hilo, wakili Said alitaka kuwasilisha barua waliyoipata Februari 10, 2026 kutoka Ofisi ya Mrajisi wa Mahakama ikithibitisha wakili huyo kutokuwa na leseni.
Hata hivyo, aliwekewa pingamizi na wakili wa upande wa waleta maombi, Rajab Abdalla Rajab akidai barua hiyo inatakiwa itoke kwa ushahidi na aliyeiwasilisha anatakiwa aulizwe kuhusu barua hiyo, hoja ambayo ilikubaliwa na Jaji na akakataa kupokea barua hiyo.
Hatua hiyo ilitoa fursa ya wakili wa Serikali, Said kueleza zaidi kuhusu sababu za wakili huyo kukosa sifa za kusaini viapo hivyo.
Wakati akieleza, alisimama wakili wa waleta maombi, Rajab, akasema hakuna sababu ya kupoteza muda wa Mahakama akashauri Mahakama ikijiridhishe ikiwa kama ni kweli wakili huyo hana sifa au vinginevyo na itoe uamuzi leo.
Hata hivyo, licha ya Jaji kukubaliana na hoja hiyo ya kujiridhisha na kwamba ana uwezo wa kupata majibu siku hiyo, lakini alisema anatakiwa apate muda wa kuandika uamuzi huo, hivyo akaahirisha shauri hilo hadi leo Ijumaa Februari 13, 2026 ambapo ametoa uamuzi wake na kuyatupilia mbali maombi hayo.
Katika shauri hilo, upande wa waleta maombi uliwakilishwa na mawakili wawili, Rajab Abdalla Rajab na Suleiman Abdalla huku upande wa wajibu maombi ukiwakilishwa na mawakili Said Salim Said kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, Maulid Ame Mohamed kutoka ZEC, Mbarouk Suleiman Othman na Ali Issa Abdalla.
Waombaji ambao ni wadai katika mashauri ya uchaguzi namba mbili hadi 18 za mwaka 2025, waliwasilisha maombi hayo chini ya hati ya dharura.
Hatua hiyo ilikuja kufuatia tangazo la ZEC kwa umma likielezea nia ya kuteketeza nyaraka zote za uchaguzi wa mwaka 2025.
Nyaraka ambazo zilikuwa zimeombewa kuzuiwa ni fomu PS namba tisa, fomu ya makabidhiano ya orodha ya vifaa zilizojazwa na wasimamizi wa vituo vyote vya kupigia kura vya Jimbo la Pangawe, Malindi, Kiembe Samaki, Chumbuni, Chaani, Makunduchi, Mwera, Nungwi, Tumbatu, Mkwajuni, Bumbwini, Mpendae, Mtoni, Welezo, Amani, Mwanakwerekwe na Kijini kwenye uchaguzi mkuu wa 2025.
Nyingine ni fomu PS namba 13B, hesabu ya karatasi za kura, fomu namba 16, fomu ya kufunga kituo cha kupiga kura na fomu PS namba 17B ya matokeo, fomu MWJ namba 19B ya majumuisho ya kura na orodha ya wapigakura ya mapema katika majimbo hayo.