BEKI wa zamani wa Simba SC, Emily Mugeta ambaye kwa sasa anapiga soka la kulipwa nchini Ujerumani akiwa na FC Waldkirch, amezungumzia kuvutiwa kwake na kiwango cha beki mpya wa Wekundu wa Msimbazi, Nickson Kibabage.
Mugeta ambaye kwa sasa yupo nchini kwa mapumziko mafupi, amesema tangu Kibabage ajiunge na Simba katika dirisha dogo la usajili la Januari, ameonekana kuendana haraka na mfumo wa kocha Steve Barker na kuleta utulivu katika eneo la beki wa kushoto.
“Kwa kweli nimefurahishwa na namna anavyocheza, ana kujiamini, anajua kupanda na kushuka kwa wakati na ana nidhamu ya uchezaji,” amesema Mugeta.
Kibabage ambaye ni nyota wa zamani wa Mtibwa Sugar, Yanga, Singida Black Stars na Difaa El Jadida ya Morocco, tayari amecheza mechi nne kati ya tano tangu atue Msimbazi, ikiwemo mbili za Ligi ya Mabingwa dhidi ya ES Tunis.
Mugeta anaamini uzoefu alioupata Kibabage katika klabu mbalimbali ndani na nje ya nchi unampa uzoefu, hasa katika mechi zenye presha kubwa.
“Kijana ameiva. Unaona kabisa ana uzoefu wa mashindano makubwa na anajua nini maana ya kucheza katika timu yenye malengo ya ubingwa,” aliongeza.
Zaidi ya yote, Mugeta anaona Kibabage anaweza kuwa mrithi sahihi wa Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, aliyedumu Simba kwa takribani miaka 15 kabla ya kuhamia Yanga.
Kwa Mugeta, si rahisi kuziba pengo la mchezaji aliyedumu kwa muda mrefu kiasi hicho lakini anaamini Kibabage ana uwezo wa kufanya hivyo. “Kuziba nafasi ya Tshabalala si jambo dogo lakini kwa ninavyoona, Kibabage ana kila sifa ya kuwa mrithi wake. Anahitaji tu kupewa muda na kuendelea kuaminiwa,” alieleza.
Awali kabla ya Kibabage, Anthony Mligo ndiye alikuwa akipewa nafasi ya kurithi mikoba ya Tshabalala kabla ya Simba kuongeza nguvu upande huo huku Naby Camara ambaye ni kiraka akitumika zaidi katika nafasi ya kiungo.