Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba ameagiza baadhi ya watumishi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, kukatwa fedha kwenye mishahara yao ili kufidia uzembe uliosababisha mifuko ya saruji 1,262 kuganda.
Kwa mujibu wa Dk Mwigulu, watumishi hao ni wale waliopewa jukumu la kusimamia ujenzi wa Veta ambapo saruji ilitakiwa iwe malighafi katika ujenzi uliopangwa kutekelezwa wilayani Handeni mkoani Tanga.
Dk Mwigulu ameeleza hayo leo, Ijumaa Februari 13,2026 alipozungumza na wananchi wa Handeni ikiwa ni siku ya kwanza ya ziara yake ya kikazi mkoani humo.
“Wananchi wa Handeni wanasubiri Veta, waliotakiwa kujenga wameigandisha na kila siku wako ofisini, kila mwezi wanalipwa mishahara kwa kodi zenu mnaosubiri jengo.
“Huu uzembe ndio tunaosema hatuwezi kuuvumilia, nilipokuja nilijua watumishi wa halmashauri ningewafukuza leo leo, kumbe hili linasimamiwa kutoka wizarani,” amesema Dk Mwigulu.
Aidha Dk Mwigulu amemuagiza waziri wa wizara hiyo, kuwachukulia hatua watumishi waliofanya uzembe huo uliosababisha mifuko ya saruji 1,262 kuganda.
“Hii saruji iliyoganda wasimsumbue Rais (Samia Suluhu Hassan) kutafuta fedha, wakatwe kwenye mishahara yao ili saruji irudishwe hapa,” amesema Dk Mwigulu.
Dk Mwigulu amesema kamwe uzembe wa namna hiyo hauwezi kuvumiliwa na hata kwa mtu wa kawaida asingiweza kuigandisha mifuko ya saruji wakati akijenga nyumba yake.
“Watu wanajibana kulipa kodi, ili kujenga Veta na hospitali, lakini waliopewa dhamana waacha saruji inaganda. Nataka kuona hatua zikichukuliwa,” amesema.
Dk Mwigulu ameagiza kupatiwa kwa orodha ya watumishi waliohusika na uzembe wa namna hiyo.
Katika hatua nyingine, Dk Mwigulu ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuchunguza mwenendo wa ujenzi wa jengo la mama na mtoto katika kituo cha afya Sindeni wilayani Handeni lililojengwa chini ya viwango.
Kwa mujibu wa Dk Mwigulu, miongoni mwa kasoro hizo ni milango 34 iliyowekwa ipo chini ya viwango.
“Katika ujenzi ule milango 34 ipo chini ya viwango, ndio mazoea mazoea hayo watu wanabandika tu na kuondoka,” amesema Dk Mwigulu.
Chimbuko la agizo hilo, limetokana na taarifa alizonazo Dk Mwigulu zinaeleza Handeni kuna matatizo kwenye utekelezaji wa baadhi ya miradi.
Kutokana na hilo, Dk Mwigulu ameiagiza Takukuru kuchunguza na kuchukua hatua zinazostahili kwa wote watakaobainika.
“Kama mtagundua wameweka milango ya chini ya kiwango ili kuiba fedha hatua za kisheria zilichukuliwe. Mkuu wa Mkoa (Dk Batlida Burian-Tanga) wafuatilia hawa wote kama wamefanya makusudi hatua zichukuliwe,”
“Haiwezekani fedha Sh300milioni zikatoka halafu watu wanaweka milango ya ovyo ovyo ambayo baada ya miezi miwili au mitatu inadondoka. Nipate orodha ya waliohusika, uchunguzi ukikamilika nipate taarifa kitu gani kilichofanyika,” ameeleza Dk Mwigulu.