Nyama choma ni miongoni mwa vyakula vinavyopendwa kwa kiwango kikubwa, hasa katika mikusanyiko ya kijamii na sherehe.
Hata hivyo, kazi za kitafiti za kisayansi zimeonyesha kuwa ulaji wa nyama iliyochomwa sana au iliyoungua unaweza kuhusishwa na ongezeko la hatari ya baadhi ya saratani, hususan kansa ya utumbo mpana.
Utafiti uliofanywa mwaka 2005 na Taasisi ya Taifa ya Saratani ya Marekani uliowahusisha zaidi ya watu 300,000 katika majimbo mbalimbali, ulibaini kuwa watu waliokuwa wakila nyama nyekundu iliyochomwa hadi kuungua, walikuwa na hatari kubwa ya kupata saratani ya utumbo mpana na kongosho.
Utafiti huo, uliochapishwa mwaka 2007, ulieleza kuwa chanzo kikuu cha hatari hiyo ni kemikali zinazotengenezwa wakati wa kuchoma nyama kwa joto kali, hususan heterocyclic amines (HCAs) na polycyclic aromatic hydrocarbons (PAHs).
Katika bara la Ulaya, utafiti wa EPIC (European Prospective Investigation into Cancer and Nutrition) uliohusisha zaidi ya washiriki 500,000 katika nchi 10, ulibaini kuwa ulaji mkubwa wa nyama nyekundu na nyama iliyopikwa kwa joto kali, ulihusishwa na ongezeko la kansa ya utumbo mpana.
Utafiti huo uliochapishwa mwaka 2011 ulisisitiza kuwa hatari ilikuwa kubwa zaidi kwa watu waliokuwa wakila nyama hiyo mara kwa mara bila kuzingatia mbinu salama za upishi.
Mwaka 2015, Shirika la Afya Duniani (WHO) kupitia Shirika la Kimataifa la Utafiti wa Saratani (IARC) lilichambua zaidi ya kazi za kitafiti 800 kutoka duniani kote, huku matokeo yake yakionesha kuwa nyama iliyosindikwa iliwekwa katika kundi lenye ushahidi wa kutosha kusababisha saratani kwa binadamu (Group 1 carcinogen ) huku, nyama nyekundu hususan inapopikwa kwa joto kali kama kwa kuchoma, iliwekwa katika kundi la Group 2A (inaweza kusababisha saratani kwa binadamu), lakini ushahidi huo haujakamilika.
IARC ilieleza kuwa ushahidi huo ulitokana na tafiti za watu, majaribio ya maabara, pamoja na ushahidi wa kibaiolojia unaoonesha kemikali za HCAs na PAHs zinaweza kuharibu vinasaba vya seli.
Mnamo 2021, uchambuzi wa pamoja wa tafiti 148 (meta-analysis) uliochapishwa katika jarida la kisayansi ulihitimisha kuwa ulaji wa nyama nyekundu, ulihusishwa na hatari ya saratani ya utumbo mpana, mapafu, ini na tumbo huku, ulaji wa nyama iliyosindikwa ukiongeza hatari ya saratani ya utumbo mpana kwa takribani asilimia 18 kwa kila gramu 50 zinazoliwa kwa siku.
Aidha, tafiti nyingine nchini Marekani na Australia zimeonyesha kuwa kemikali zinazotokana na nyama iliyochomwa sana, zinaongeza hatari ya hatua ya awali kabla ya saratani au hata kupata saratani ya figo pamoja na ile ya tezi dume.
Nyama choma ambayo inaelezwa ikichomwa sana au ikiungua inaweza kuhusishwa na ongezeko la hatari ya baadhi ya saratani, hususan kansa ya utumbo mpana. Picha na Mtandao
Wataalamu wanasema kuwa hatari haiko kwenye kula nyama mara moja moja, bali ni ulaji wa mara kwa mara nyama iliyochomwa hadi kuungua na kukosa mboga na matunda yenye virutubisho au kemikali zinazosaidia kuulinda mwili dhidi ya uharibifu wa seli.
Dk Sarah Elliyaphari kutoka Hospitali ya Rufaa mkoani Shinyanga, anaeleza kuwa nyama choma peke yake haiwezi kuchangia saratani, isipokuwa pale mtu anapoitumia mfululizo kwa muda mrefu bila uwiano wa mlo, jambo linaloweza kuongeza hatari ya kupata ugonjwa huo.
“Ulaji wa nyama choma hausababishi saratani moja kwa moja. Hata hivyo, ulaji wa nyama choma wa mara kwa mara na kwa muda mrefu bila kuupa mwili nafasi ya kutoa uchafu unaotokana na nyama ya kuchoma, unaweza kuchangia kwa asilimia fulani hatari ya mtu kupata saratani,”anasema.
Anasema ili mtu apate saratani, huchangiwa na mambo mengi kwa pamoja, si jambo moja pekee. Miongoni mwa mambo yanayochangia anasema ni ulaji wa vyakula kwa mtindo uleule kwa muda mrefu, hasa vyakula vya mafuta na wanga kama maandazi na chapati endapo vitatumika asubuhi, mchana na jioni kwa miaka mingi.
Anashauri kuwa kupunguza moto mkali, kuondoa sehemu zilizoungua, na kuongeza vyakula vya mimea, kunaweza kupunguza hatari hiyo.
Nyama choma ambayo inaelezwa ikichomwa sana au ikiungua inaweza kuhusishwa na ongezeko la hatari ya baadhi ya saratani, hususan kansa ya utumbo mpana. Picha na Mtandao
Njia nyingine za kujikinga kwa walaji nyama
Moja, ondoa mafuta au chagua nyama yenye mafuta kidogo: Tumia nyama isiyo na mafuta mengi, na kama yapo yaondoe kabla ya kuchoma.
Mafuta na majimaji yanapodondoka motoni husababisha moto mkali na moshi mwingi unaotengeneza kemikali hatarishi (PAHs) zinazoweza kushikamana na nyama.
Pili, epuka nyama zilizohifadhiwa: Nyama zilizohifadhiwa kwa kemikali kama sausage, bacon, nyama za makopo zimeainishwa na WHO kuwa huongeza hatari ya saratani ya utumbo mpana. Pendelea nyama mbichi isiyoongezwa vihifadhi
Tatu, choma kwa moto wa wastani:Joto la juu sana huzalisha kemikali zinazohusishwa na saratani. Hatari huongezeka nyama inapoungua.
Moto wa wastani hupunguza uzalishaji wa kemikali hizi. Hivyo epuka kuchoma nyama kwa moto mkali sana.
Nne, punguza muda wa kuchoma. Kuchoma kwa muda mrefu huongeza uwezekano wa nyama kuungua na kutengeneza carcinogens (kemikali zinazosababisha saratani.)
Lakini pia, kubadilisha upande wa nyama mara kwa mara hupunguza kuungua upande mmoja. Njia hii inapunguza uwepo wa kemikali hatari.
Tano, zingatia usafi wa vifaa. Masalio ya zamani kwenye waya au kikaangio yanaweza kuwa na kemikali hatarishi yakitumika tena. Kemikali hizo zinaweza kuingia kwenye chakula kipya. Hivyo, usafi hupunguza hatari ya kuhamisha sumu.
Sita, tumia mchanganyiko wa viungo. Ni muhimu sana kulainisha nyama kwa viungo kabla ya kuchoma kwakuwa husaidia kupunguza uzalishaji wa kemikali hatarishi, kwani huunda kinga kati ya nyama na moto. Viungo hivyo ni kama limao, vitunguu saumu, tangawizi, pilipili hoho, na mafuta kidogo.
Kwa mujibu wa wataalamu wa lishe, viungo hivyo vinaweza kupunguza uzalishaji wa kemikali hatarishi kwa asilimia 30 hadi 90.