Dodoma. Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii imesema utekelezaji madhubuti wa majukumu ya Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) utalipunguzia Taifa mzigo wa gharama za matibabu na fidia kwa wafanyakazi wanaoumia au kupata magonjwa yatokanayo na kazi.
Kauli hiyo imetolewa na mwenyekiti wa kamati hiyo, Hawa Chakoma, wakati akihitimisha mafunzo ya usalama na afya mahali pa kazi yaliyotolewa na OSHA kwa wajumbe wa kamati, leo, Februari 13, 2026, bungeni jijini Dodoma.
Mafunzo hayo ya siku moja yalifanyika kufuatia maelekezo yaliyotolewa na kamati katika kikao chake cha Januari 19, 2026, wakati OSHA ilipowasilisha taarifa kuhusu muundo na majukumu yake.
Lengo kuu lilikuwa ni kuiwezesha kamati kutekeleza kikamilifu jukumu lake la kuisimamia Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano) pamoja na taasisi zilizo chini yake, ikiwemo OSHA.
Akizungumza katika hafla ya kufunga mafunzo hayo, Chakoma ameipongeza OSHA kwa juhudi zake za kuimarisha usalama na afya mahali pa kazi kupitia utoaji wa mafunzo kwa waajiri na wafanyakazi, ukaguzi wa mifumo ya usalama, pamoja na uchunguzi wa afya za wafanyakazi katika hatua mbalimbali za ajira.
“Naendelea kuwapongeza na kuwashukuru kwa mafunzo haya, ambayo yamewafungua wabunge wengi. Ni mafunzo muhimu ambayo, kwa mtazamo wa haraka, unaweza kudhani yanahusu maeneo ya kazi pekee; lakini ukweli ni kwamba yanaweza kutumika hata katika mazingira ya nyumbani kukabiliana na hatari mbalimbali,” amesema Chakoma.
Amesisitiza kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za kuimarisha afya za wafanyakazi na wananchi kwa ujumla, akieleza kuwa OSHA ina nafasi muhimu katika kulinda rasilimali watu ya Taifa.
“Ikiitekeleza vyema majukumu yake kwa mujibu wa sheria na taratibu, hakika tutakuwa tunaliokoa Taifa dhidi ya mzigo mzito wa kutibu majeruhi na kulipa fidia kwa wafanyakazi wanaoumia kazini,” ameongeza.
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, wakifuatilia mada mbalimbali zilizowasilishwa katika mafunzo mafunzo ya usalama na afya mahali pa kazi yaliyotolewa na OSHA kwa Kamati hiyo Bungeni Jijini Dodoma.
Sambamba na pongezi hizo, kamati imeitaka OSHA kuishauri sekta binafsi na wamiliki wa maeneo ya kazi kuwekeza katika teknolojia na mitambo ya kisasa iliyosanifiwa ili kupunguza hatari za ajali na magonjwa kazini.
Mfano ulitolewa ni wa matumizi salama ya lifti katika majengo marefu yanayoendelea kuongezeka katika miji mbalimbali nchini.
Aidha, kamati imependekeza elimu ya masuala ya usalama na afya kazini itolewe kwa wabunge wote pamoja na makundi mbalimbali ya wananchi, ikiwemo wakulima wadogo, hususan wanaojishughulisha na kilimo cha tumbaku mkoani Tabora, ambao hukabiliwa na vihatarishi vya kiafya katika shughuli zao za kila siku.
Mjumbe wa kamati hiyo, Katani Ahmad Katani, amesema mafunzo hayo yameongeza uelewa mkubwa kwa wajumbe kuhusu majukumu ya OSHA na umuhimu wake katika jamii.
“Tangu niingie kwenye kamati hii na kufahamu kazi zinazofanywa na OSHA, natamani kuwaona kila mahali. Leo tumepata elimu kubwa, japokuwa muda haukuwa wa kutosha,” amesema.
Kwa upande wake, mjumbe mwingine wa kamati, Mariam Kisangi, ameipongeza OSHA kwa mafunzo hayo na kuomba yaendelezwe ili kuwajengea wabunge na wananchi uwezo zaidi wa kukabiliana na changamoto za usalama na afya.
“Ninaungana na wenzangu kusema kuwa mafunzo haya ni muhimu na yanaweza kutusaidia katika maisha yetu ya kila siku. Ni vyema yakawa endelevu,” amesema.