Kilombero Sugar Yaendelea Kukuza Mpango wa Uwezeshaji wa TEHAMA kwa Manufaa ya Zaidi ya Wanafunzi 2,500 Katika Bonde la Kilombero

Morogoro, 12 Februari 2026

KAMPUNI ya Sukari Kilombero imekamilisha kwa mafanikio Awamu ya Pili ya Mpango wa Uwezeshaji wa TEHAMA kwa Shule, mpango endelevu unaoendeshwa na dhamira ya kampuni katika kujenga jamii inayostawi na iliyo tayari kidijitali. Mpango huu unalenga kuipatia shule za sekondari zinazozunguka kampuni vifaa muhimu vya TEHAMA na ujuzi wa kiteknolojia unaowaandaa wanafunzi kwa fursa za baadaye.

Kupitia Awamu ya Pili, Kampuni ya Sukari Kilombero inatoa zaidi ya kompyuta za mezani (desktop) 50 zikiwa kamili kwa Shule za Sekondari za Kidodi, Iwemba na Malecela. Msaada huu unajumuisha usaidizi kamili wa kitaalamu kutoka Kitengo cha TEHAMA cha kampuni. Hii inafuatia Awamu ya Kwanza ambayo kampuni ilitoa kompyuta 35 pamoja na samani kwa Shule za Sekondari za Nyange na Lyahila.

Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano, Bw. Derick Stanley, Mkurugenzi wa Masuala ya Uhusiano wa Kampuni, alisema kuwa mpango huu unaendana na vipaumbele vya taifa, ikiwemo dira ya maendeleo ya taifa 2050 na Mkakati wa Taifa wa Elimu ya Kidijitali 2024/25–2029/30 na Mwongozo wa Taifa wa Utekelezaji wa Akili Bandia katika Elimu. Alisisitiza kuwa mpango huo utabadilisha mazingira ya elimu nchini kwa kuongeza upatikanaji wa fursa za kujifunza kwa njia ya kidijitali.

Kompyuta zilizotolewa zimeboreshwa kikamilifu kwa programu muhimu zinazofaa kwa mafunzo ya msingi ya matumizi ya kompyuta. Hatua hii inaunga mkono dira ya taifa ya 20250 na Mwongozo wa Taifa wa Shule na Vyuo vya Ualimu wa Kidijitali (2025) unaosisitiza umuhimu wa miundombinu salama, nafuu, na ya kuaminika ya TEHAMA kwa ufundishaji na ujifunzaji.

Bw. Victor Byemelwa, Meneja wa Mawasiliano na Uhusiano kwa wadau, alieleza vigezo vilivyotumika kuchagua shule zitakazonufaika:

“Tulipima utayari wa shule katika kujifunza kwa njia ya kidijitali, ikiwemo uwepo wa mwalimu wa TEHAMA, chumba maalum cha kompyuta, pamoja na uwezo wa shule kuunga mkono ajenda ya taifa ya elimu ya kidijitali.”

Aliongeza kuwa mpango huu uliozinduliwa Agosti 2025 utafanyika kwa awamu, na utakuwa na mfumo endelevu wa ufuatiliaji ili kuhakikisha matokeo na maboresho yatakayochochea kujifunza.

Mgeni rasmi, Mhe. Shaka Hamdu Shaka, Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, alisifu hatua hiyo:

“Serikali inaendelea kuimarisha uwezo wa walimu na watendaji wa elimu katika kuingiza matumizi ya TEHAMA kwenye ufundishaji na uendeshaji wa shule. Tunahamasisha wadau zaidi kuungana na Kilombero Sugar katika kuunga mkono mageuzi ya kidijitali nchini.”

Akizungumza kwa niaba ya shule walionufaika, Mwalimu. Yobu Joseph Mwalufyagila, Mkuu wa Shule ya Sekondari Kidodi, alitoa shukrani kwa msaada huo. Aidha, Bi. Restuta Ngaema, mwanafunzi wa Kidato cha Tatu kutoka Shule ya Sekondari Iwemba, alionyesha furaha yake akibainisha kuwa upatikanaji wa kompyuta utamwezesha kufuatilia ndoto yake ya kuendeleza masomo ya TEHAMA.

Kilombero Sugar imerejea dhamira yake ya kuendelea kupanua Mpango wa Uwezeshaji wa TEHAMA kwa Shule, kupitia upanuzi wa mradi huu ili kufikia shule zaidi katika Bonde la Kilombero kama sehemu ya mchango wake wa muda mrefu katika ajenda ya elimu ya kidijitali Tanzania.