KOCHA Mkuu wa Singida Black Stars, Mkenya David Ouma, amesema kwa sasa timu hiyo inaenda Afrika Kusini kusaka heshima tu, katika mechi ya mwisho ya hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya Stellenbosch FC.
Wawakilishi hao wa Tanzania katika Kombe la Shirikisho Afrika, watatupa karata yao ya mwisho keshokutwa Jumapili kuanzia saa 1:00 usiku kwa kucheza dhidi ya Stellenbosch ya Afrika Kusini, huku timu zote zikiwa hazina nafasi ya kusonga mbele.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ouma amesema baada ya mechi ya ushindi wa timu hiyo wa bao 1-0, dhidi ya Fountain Gate, hali ya wachezaji ni nzuri na hakuna majeruhi yeyote, hivyo wanaenda kukabiliana na wapinzani wao kwa heshima na nidhamu tu.
“Hatuna cha kupoteza tena baada ya kutokuwa na mwenendo usioridhisha, tulipofikia kwetu ni mafanikio makubwa kwa sababu ni mara ya kwanza, hivyo, tumejifunza vitu vingi ikiwemo pia namna ya kutumia vizuri uwanja wa nyumbani,” amesema Ouma.
Kocha huyo amesema haikuwa rahisi kwa timu hiyo kuonyesha ushindani na timu zenye uzoefu mkubwa zaidi ya kikosi hicho, ingawa maingizo ya nyota wapya katika dirisha dogo la Januari 2026, yameanza kuonyesha matumaini makubwa kwa msimu huu.
CR Belouizdad ya Algeria inayonolewa na aliyekuwa kocha wa Yanga, Sead Ramovic, inaongoza kundi C ikiwa na pointi 12, ikifuatiwa na AS Otoho D’Oyo ya Congo Brazzaville yenye pointi tisa, ambazo timu zote tayari zimefuzu hatua inayofuata.
Kwa upande wa Singida inashika nafasi ya tatu na pointi nne ambazo ni sawa na za Stellenbosch inayoburuza mkiani, hivyo, mechi kati ya timu hizo zote ni ya kusaka heshima, kwani matokeo ya aina yoyote hayawezi pia kuzinufaisha kusonga mbele.
Mechi ya kwanza iliyopigwa kwenye Uwanja wa New Amaan Zanzibar, Novemba 30, 2025, zilitoka sare ya bao 1-1, huku Singida ikichomoa dakika ya 90+1, kupitia kwa Marouf Tchakei, baada ya Langelihle Phili kuitanguliza Stellenbosch dakika ya 52.