Kulala na soksi rafiki na adui kwako

Kuna watu duniani wanapolala wakiwa wamevaa soksi, hupata usingizi mwanana, huku wengine wakishindwa kabisa kulala.

Mtaalam wa masuala ya usingizi, Mwende Kimweli, anasema kuwa kwa watu wengi, kulala na soksi husaidia kupata usingizi.

Miguu yenye joto hutuma ujumbe kwa ubongo kwamba ‘unaweza kupumzika’ jambo linalosaidia mwili kulala haraka.

“Miguu baridi hufanya kinyume chake. Huifanya mishipa ya damu kujikaza na kuuweka mwili tayari kwa hivyo,’’ anasema.

Zaidi ya hayo, kadri muda wa kulala unavyokaribia, mwili hutulia. Joto la ndani ya mwili hushuka, huku mishipa ya damu kwenye mikono na miguu ikitanuka ili kutoa joto.

Kupoa huku, Kimweli anasema ni kichocheo muhimu kinachouambia ubongo, kuwa ni wakati wa kulala.  Miguu ikiwa baridi sana, mishipa hiyo hujikusanya na kuchelewesha mwili kutulia.

kuvaa soksi chafu zinaweza kusababisha ngozi kuwasha au kusambaza bakteria. Picha na Mtandao



Kwa mujibu wa Kimweli, wanaoweza kunufaika zaidi kwa kuvaa soksi wanapolala ni pamoja na watu wenye miguu baridi, wenye mzunguko hafifu wa damu, wanaotatizika kulala (insomnia), wazee ambao mzunguko wa damu hupungua kwa njia ya kawaida, na mtu yeyote anayeishi kwenye maeneo ya baridi au nyumba zenye sakafu baridi.

Kuvaa soksi kunaweza kusaidia kupunguza kuamka usiku au kutolala vizuri, kwa sababu miguu yenye joto husaidia kudumisha hali thabiti ya joto au baridi mwilini usiku kucha.

“Mabadiliko ya halijoto ni mojawapo ya sababu kubwa zinazowafanya watu waamke. Soksi husaidia kudhibiti halijoto na kupunguza kugeukageuka kitandani,”anaeleza.

Zaidi ya hayo, Kimweli anasema kuwa kuna hali ambazo kupasha miguu joto usiku kunapendekezwa. Hii ni pamoja na watu wanaougua ugonjwa wa vidole vya mikono au miguu kuwa baridi sana au kufa ganzi unaofahamika kama Raynaud’s, wenye matatizo ya mzunguko wa damu kwenye miguu, au wanaoukosa usingizi hali  inayochochewa na msongo wa mawazo  na kutolala vizuri sababu ya baridi.

Katika hali hizi, Kimweli anasema joto linaweza kuzuia usumbufu unaokatiza usingizi.

soksi zinazobana sana zinaweza kuzuia mtiririko wa damu hasa kwenye vifundo. Picha na Mtandao



Hata hivyo, si kila mtu anapaswa kuvaa soksi anapolala.  Kimweli anasema watu wanaopaswa kuwa waangalifu, ni pamoja na wenye matatizo sugu ya mzunguko wa damu, na wenye baadhi ya matatizo ya kisukari yanayoathiri miguu.

“Pia, watu wenye maambukizi ya ngozi, vidonda, au ukurutu kwenye miguu, na watu wanaotokwa jasho kupita kiasi usiku,”anasema na kueleza kuwa kuna madhara yanaoibuka kwa kulala ukiwa umevaa soksi.

Kwa mfano, soksi zinazobana sana zinaweza kuzuia mtiririko wa damu hasa kwenye vifundo. Hii ni kwa sababu baadhi ya nyuzi zilizotumika kuunda soksi hunasa unyevu na kutengeneza mazingira bora ya fangasi kama fangasi wa mguu. Au kuvaa soksi chafu zinazoweza kuwasha ngozi au kusambaza bakteria.

unapaswa kuwa na soksi maalum za wakati wa kulala zisizobana kifundo cha mguu, na zilizo nyepesi au nzito. Picha na Mtandao



Ni soksi gani bora za kulalia?

“Unaweza ukachagua soksi laini za pamba, za manyoya, za mianzi au zile zinazopitisha hewa,’’ anasema.

Pia, anasema soksi hizo zinapaswa kuwa huru, zisizobana kifundo cha mguu, na zilizo nyepesi au nzito kulingana na hali ya hewa.

Pia, unapaswa kuwa na soksi maalum za wakati wa kulala. Hii ni njia safi zaidi ya kuzuia jasho, uchafu na bakteria. Mbali na soksi, Kimweli anasema unaweza kupasha miguu joto au kudhibiti halijoto ya usiku kwa kuoga maji vuguvugu kabla ya kulala.

“Hii husaidia mwili hutulia baadaye, mtu akalala vizuri,” anaeleza.

Pia unaweza kuweka chupa ya maji ya moto kwenye miguu, kutumia matandiko mepesi, kuwasha kipasha-joto kwa kiwango cha chini au kutia miguu kwenye maji vuguvugu kwa dakika kumi kabla ya kulala.