Mafaili ya Epstein na hekima ya usipoziba ufa utajenga ukuta – 4

Hekima za watumia Kiswahili walioishi dahari nyingi zilizopita waliacha methali ya ukumbusho wa kuchukua hatua haraka kabla mambo hayajaharibika zaidi.

Walisema, “usipoziba ufa utajenga ukuta.” Bibi yangu aliniambia, “bundi asipokabiliwa hugeuka zimwi.”

Kitendo cha msanii Maria Farmer kupuuzwa na malalamiko yake dhidi ya Jeffrey Epstein, hivi sasa dunia inapata habari kuhusu zimwi lililoharibu maisha ya watoto wa kike makumi kwa mamia.

Rushwa ni janga baya. Epstein asingekuwa na nguvu ya fedha na mtandao wa watu wazito waliomzunguka, hadithi ya Mafaili ya Epstein, isingekuwa nzito kwa kiwango cha sasa.

Mashitaka ya Maria dhidi ya Epstein na ushuhuda aliotoa, vilipaswa kuwazindua matajiri, wanasiasa na watu wengine mashuhuri kujitenga na mhalifu huyo wa makosa ya kingono kwa watoto wadogo. Pengine ni kutimia kwa ngano ya ‘sikio la kufa.’

Kwa mujibu wa Maria, mbali na kubakwa na Epstein mwaka 1996, vilevile aligundua jambo zito ndani ya kasri la bilionea huyo.

Maria alisema, aliajiriwa na Epstein kama mshauri wake wa masuala ya sanaa. Siku moja Epstein alimwonesha Maria chumba maalumu kwa ajili ya shughuli za habari. Hii ilikuwa kwenye kasri la Epstein, lililopo Manhattan, New York.

Maria alisema aligundua ndani ya chumba cha masuala ya habari kulikuwa na watu maalumu, waliokuwa wakifuatilia picha zinazochukuliwa kutoka kwenye kamera mbalimbali, nyingi zikiwa za siri.

Kamera hizo za siri zilichukua na kurekodi picha vyumbani mpaka chooni. Mlango wa kuingilia chumba hicho cha masuala ya habari ulikuwa wa siri.

Kamera za kunasa matukio vitandani, chooni na mlango kuwa wa siri, kwa pamoja vilimtisha Maria.

 Hata hivyo, alipotoa maelezo hayo hakuna ambaye alimwelewa. Walimpuuza. Matajiri waliendelea kuzuru makasri ya Epstein na kupata starehe walizohitaji, wasijue kwamba kila walichofanya kilirekodiwa kama Maria alivyotahadharisha.

Ava Cordero ni mwanamitindo wa zamani. Kibaiolojia Ava ni transgender woman, yaani alizaliwa mwanamume, kisha akabadili jinsi kuwa mwanamke. Oktoba 2007, Ava alifungua mashitaka ya kunyanyaswa kingono na Epstein. Hata hivyo, shauri hilo la Ava lilitupiliwa mbali, kisha vyombo vya habari vikajikita kumjadili mwanamitindo huyo wa zamani kwa uamuzi wake wa kubadili jinsi na historia yake ya changamoto ya afya ya akili.

Mijadala ilipuuza malalamiko yake ya kutendewa ukatili.

Sasa kwenye muktadha anaingia mwanamke mwenye uraia pacha wa Marekani na Australia. Jina lake ni Virginia Giuffre. Aprili 25, 2025, Virginia alifariki dunia. Ripoti ya uchunguzi wa mwili wake ilieleza kuwa Virginia alijiua.

Hata hivyo, familia yake haijawahi kukubaliana na mapendekezo hayo ya madaktari. Wanaamini Virginia aliuawa na mtu au watu ambao hawataki uhalifu wao ujulikane.

Kutoka Machi 2005 mpaka Aprili 2025, ni miongo miwili kamili na mwezi mmoja. Ni kipindi ambacho Virginia alijitoa kukabiliana na uhalifu wa Epstein na mtandao wake.

 Alijipambanua kama mtetezi wa waathirika wote wa unyama wa Epstein na wateja wake. Ndani ya kipindi hicho, Virginia alitaja orodha ya watu wengi.

Watajwa hao, wengi wao ni watu mashuhuri. Zaidi, Virginia alibainisha kila ambacho kilikuwa kikifanyika kwenye makasri ya Epstein.

Ushuhuda wa Virginia unaanzia mwaka 2000, wakati huo alikuwa na miaka 16, ikibaki miezi afikishe miaka 17.

Virginia alikuwa mhudumu kwenye ofisi ya utoaji huduma ya spa kwenye klabu ya Mar-a-Lago, Palm Beach, Florida. Kuweka sawa kumbukumbu, Mar-a-Lago inamilikiwa na Rais wa Marekani, Donald Trump.

Ndani ya ofisi ya spa, Virginia alikuwa anasoma kitabu kuhusu huduma ya masaji. Ghislaine Maxwell ambaye alikuwa mpenzi wa Epstein na mshirika wake wa uhalifu wa kingono, alikuwa kwenye ofisi hiyo ya spa. Ghislane alivutiwa na Virginia.

Kwa kukumbusha, Ghislaine kwa sasa anatumikia kifungo cha miaka 20 jela baada ya kukutwa na hatia ya kuwaumiza na kuwatumikisha mabinti wadogo kingono kwa kushirikiana na Epstein.

Ghislaine baada ya kumwona Virginia anasoma kitabu kuhusu masaji, alimshawishi akubali kufanya kazi kama mtoa huduma ya masaji kwa Epstein na kwamba, angekuwa anasafiri sehemu tofauti duniani akihudumia. Ghislaine alimwambia Virginia asiwe na hofu, kwa sababu hakukuwa na umuhimu wa uzoefu wa kazi.

Siku ya kwanza Virginia kazini ilikuwa kwenye jumba la Epstein lililopo Palm Beach, Florida. Kwa mujibu wa maelezo yake, alimkuta Epstein mtupu kama alivyozaliwa. Ghislaine alimwambia Virginia asiogope, akamwambia amfanyie masaji Epstein.

Huo ukawa mwanzo wa maisha ya Virginia kutumikishwa kingono kwenye nyumba tofauti za Epstein.

Virginia alisimulia kuwa mwanzoni kabisa baada ya kuanza kazi, aliwaambia Epstein na Ghislane kuhusu maisha yake ya nyuma. Kwamba alipitia manyanyaso makubwa ya kingono, akawa mtu wa kukimbia huku na huko.

Aliwaambia kuwa, alifanya hivyo ili watu hao watambue historia yake na wajue alihitaji usalama mkubwa wa kisaikolojia.

“Mwanzoni niliwaona ni watu wazuri, nikawaamini,” alisimulia Virginia na kuongeza: “Nilidhani nilipowaambia nilinyanyaswa kingono, kimwili na kupigwa, wangenihurumia. Kumbe nilikosea sana kuwaeleza hivyo. Waliweza kuujua vizuri udhaifu wangu na kuona sikuwa na msaada wowote.”

Virginia anasimulia kuwa Epstein na Ghislane walimpa maelekezo ya kuwa anatoa huduma ya ngono wakati wa masaji, walimwambia kuwa hivyo ndivyo angeweza kufuzu kuwa mhudumu wa masaji kitaaluma.

Virginia alikuwa bado binti mdogo, Epstein na Ghislaine walimfundisha na kumkuza ili awe anatoa huduma ya ngono kwa ubora, anapofanya masaji.

Ripoti ya kiuchunguzi ya Gazeti la Miami Herald ilibainisha kati ya mwaka 2000 na 2002, Virginia alisafirishwa kwenye makasri mbalimbali ya Esptein alikotakiwa kutoa huduma ya masaji na ngono kwa Epstein mwenyewe na wateja wake.

Makasri ya Epstein yanayotajwa hapo ni jumba lake la Palm Beach, Florida na Manhattan, New York.

Ziara nyingine, Virginia alisafirishwa hadi kwenye ranchi ya Epstein, Zorro Ranch, iliyopo New Mexico, vilevile kwenye kisiwa cha Little Saint James, kilichokuwa kikimilikiwa na Epstein.

Little Saint James, ni moja ya visiwa vya Virgin, ambavyo ni mamlaka ndani ya Dola ya Marekani.

Virginia alisema yalikuwa maisha ya kutumikishwa bila kupenda na hakuwa na uwezo kukabiliana na watu waliomtumia.

“Nilikuwa natumiwa na kupelekwa kwa mwingine utadhani sahani kubwa la matunda, ukimaliza kujihudumia, sahani inakwenda kwa mwingine naye ajihudumie.

“Nilizungushwa sehemu nyingi duniani kwa ndege binafsi. Washirika wa Epstein ni watu wenye nguvu ya kifedha na mamlaka,” alisema Virginia.

Kumbukumbu mbaya zaidi ya Virginia alipokuwa hai ni mwaka 2001, akiwa na umri wa miaka 17, alipelekwa London, England, UK, alikobakwa mfululizo na mwanamfalme wa UK, Andrew Mountbatten-Windsor “Prince Andrew.”

Virginia alisema aliyofanyiwa na Andrew, ukisimuliwa huwezi kuamini kama yalitendwa na mwanachama wa koo yenye kuheshimika duniani, koo ya kifalme.