Imekuwa tamthiliya ya miongo. Vyama vya Democratic na Republican Marekani vimegeuza sakata kuwa turufu ya kisiasa. Mwanzo wake ilikuwa sawa na ngano ya machozi ya samaki. Waliolalamika waliishia kupuuzwa na kugeuzwa kejeli kwenye uso wa jamii. Ni kuhusu Mafaili ya Epstein!
Ni kashfa ya ulimwengu sasa. Inagusa uadilifu wa serikali kwa serikali mpaka koo zenye nguvu ulimwenguni.
Marekani, UK, Ufaransa, Norway, Urusi, Israel, India, Australia, Saudi Arabia, Sweden, na Slovakia, kwa kutaja nchi ambazo viongozi wake tayari majina yao yameshaonekana kwenye Mafaili ya Epstein.
Mwalimu aliyegeuka bilionea, Jeffrey Epstein ndiyo jina la mada. Utajiri ulipomlevya, alitopea kuwa mhalifu wa ngono kwa mabinti wadogo.
Mafaili ya Epstein ni mamilioni ya nyaraka, picha, video na barua pepe za ushahidi kuhusu uhalifu wa Epstein kwa mabinti wadogo, akishirikiana na wenzake, ambao wanatambuliwa kama wateja wake (wateja wa Epstein).
Neno ‘wenzake, ‘washirika wake,’ au ‘wateja wake,’ ndipo kwenye kizaazaa kinachofanya tamthiliya iwe maarufu.
Ni chemchemi ya msukumo wa presha ya umma kutaka kujua majina ya wahusika walioshirikiana na Epstein kutenda uhalifu wa kingono. Uzani wa majina ya washukiwa ndiyo kiini cha presha yenyewe.
Wafanyabiashara matajiri na wanasiasa mashuhuri ulimwenguni, watu kutoka koo zenye nguvu duniani, wanazuoni na jumuiya ya watu maarufu, hasa wasanii na wanamitindo, ni aina ya majina yanayotokea mara nyingi ndani ya Mafaili ya Epstein.
Swali ni je, nani na nani miongoni mwao alishirikiana na Epstein kutenda uhalifu wa kingono kwa watoto? Yupi na yupi hawajatajwa lakini wamo kwenye nyaraka ambazo hazijawekwa wazi?
Majina ya Donald Trump (Rais wa Marekani), Vladimir Putin (Rais wa Urusi), Ehud Barak (Waziri Mkuu wa zamani wa Israel), Gordon Brown (Waziri Mkuu wa zamani wa UK), Thorbjorn Jagland (Waziri Mkuu wa zamani wa Norway), Sergey Lavrov (Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi) na Jack Lang (Waziri wa zamani wa Utamaduni, Serikali ya Ufaransa).
Majina mengine ya viongozi ni Peter Mandelson (Waziri namba moja wa zamani wa UK), Miroslav Lajcak (Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Slovakia na Rais wa zamani wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa), Robert Mugabe (Rais wa zamani wa Zimbabwe), Penny Pritzker (Waziri wa zamani wa Biashara wa Marekani), na Hardeep Singh Puri (Waziri wa Petroli na Gesi Asilia wa India).
Waziri wa Mkuu wa zamani wa Hispania, Jose Maria Aznar, naye ametokeza kwenye Mafaili ya Epstein, sawa na Waziri wa Afya na Huduma za Watu wa Marekani, Robert F. Kennedy Jr, Waziri wa zamani wa Utawala na Mipango wa Norway, Terje Rod-Larsen, Naibu Waziri wa zamani wa Maendeleo ya Uchumi wa Urusi, Sergey Belyakov, na Gavana wa zamani wa Marekani, Visiwa vya Virgin, John de Jongh Jr.
Ndani ya Visiwa wa Virgin, mwanasiasa mwingine anayepatikana kwenye Mafaili ya Epstein ni mwanajopo kwenye Baraza la Wawakilishi Marekani, Stacey Plaskett, wamo pia mwanadiplomasia mashuhuri Marekani, George Mitchell, Mwanasheria wa zamani wa White House, Kathryn Ruemmler, na mke wa Rais Trump, Melania Knauss Trump.
Bill Clinton, Rais wa zamani wa Marekani, ni moja ya majina mazito yenye kushitua orodha ndani ya Mafaili ya Epstein, Balozi wa Marekani nchini Uturuki, Tom Barrack, Balozi wa zamani wa Marekani nchini Austria, Ronald Lauder, ambaye ni Rais wa Baraza la Wayahudi Ulimwenguni (WJC), amekuwa sehemu ya maudhui kwenye nyaraka za Epstein, kama alivyo mwanamkakati wa zamani wa Ikulu ya Marekani, White House, Steve Bannon.
Yumo Waziri wa Biashara wa Marekani, Howard Lutnick, Mkurugenzi wa Nane wa Idara ya Ujasusi Marekani (CIA), William Burns, halafu inagonga koo nzito Ulaya. Ndani ya familia ya Mfalme wa UK, imemtia kwenye aibu mwana-mfalme, Andrew Mountbatten-Windsor na mtalaka wake, Sarah Ferguson. Koo ya Kifalme ya Norway, imemvua nguo mwanamfalme Mette-Marit (crown princess) kuwa Malkia wa Norway.
Koo ya Kifalme ya Sweden imeguswa. Binti mfalme, Sofia, ametajwa, vilevile ukoo wa kitajiri wa Rothschild, unasomeka kwenye nyaraka za kwenye Mafaili ya Epstein, kupitia kwa binti mwana-ukoo, Ariane de Rothschild, ambaye ni Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO), wa taasisi kubwa ya kifedha ya Diamond de Rothschild Group.
Mafaili ya Esptein ni jakamoyo kwa wamiliki wa fedha za dunia, Bill Gates (tajiri aliyeshika nafasi ya kwanza mara nyingi ulimwenguni Karne ya 20 na 21), vilevile mtalaka wake, Melinda Gates.
Tajiri namba moja kwa sasa, Elon Musk, kisha ni mnyororo wa matajiri wengine, Anil Ambani (mdogo wa Mukesh Ambani), Leon Black, Richard Branson, Glenn Dubin, Andrew Farkas, Mark Zuckerberg, Peter Thiel, na Reid Hoffman.
Bilionea anayemiliki Klabu ya Chelsea ya England na timu ya kikapu NBA Marekani, Los Angeles Lakers, Todd Boehly, mmiliki wa timu ya NBA ya Philadelphia 76ers, na mpira wa American Football ya Washington Commanders, Joshua Harris, mwasisi wa Google, Sergey Brin, tajiri wa Kiitaliano, Flavio Briatore na bilionea kutoka familia ya Pritzker, Thomas Pritzker, taarifa zao zimo ndani ya nyaraka za kwenye Mafaili ya Epstein.
Sultan Ahmed bin Sulayem ni mwana wa familia ya Sulayem, yenye ukaribu na Ukoo wa Maktoum, ambao ndiyo watawala wa Falme ya Dubai, ikiwa ni moja ya koo sita zinazoongoza dola ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE). Sultan Ahmed ndiye Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa kampuni ya DP World, inayomilikiwa na Serikali ya Dubai.
DP World ina zabuni za kuendesha bandari mbalimbali ulimwengu, ikiwemo Bandari ya Dar es Salaam. Sultan Ahmed yumo kwenye Mafaili ya Epstein.
Wanazuoni wanaoheshimika kwenye vyuo vikuu ulimwenguni, wameonekana kwenye Mafaili ya Epstein. Mwanasayansi wa Ujerumani, Joscha Bach, Rais wa Chuo Kikuu cha Bard, kilichopo New York, Leon Botstein, Mwanasayansi wa Marekani, John Brockman, profesa wa Marekani, Noam Chomsky, Profesa wa Chuo Kikuu cha Harvard, George Church, mwalimu wa sheria Chuo Kikuu cha Harvard, Alan Dershowtz, mwalimu wa saikolojia ya jamii Chuo Kikuu cha New York, Jonathan Haidt, na mtafiti wa Kiingereza, Stephen Hawking, ni wanazuoni kwenye orodha.
Aliyekuwa Profesa wa Chuo Kikuu cha Montana, Jack Horner, Profesa Lawrence Krauss, ambaye ameshafundisha vyuo vikuu vya Arizona, Yale na Case Western Reserve, Profesa wa zamani wa Chuo Kikuu cha Harvard, Elisa New, bingwa wa Hisabati Chuo Kukuu cha Harvard, Martin Nowak, Rais wa zamani wa Chuo Kukuu cha Harvard, Lawrence Summers, ambaye amepata kuwa Waziri wa Fedha wa Marekani, anaunga orodha ya wanazuoni kwenye Mafaili ya Epstein.