SERIKALI KUBORESHA SHERIA YA ELIMU KUENDANA NA SERA YA 2014 TOLEO LA 2023

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe, Wanu Hafidhi Ameir amesema Serikali inaendelea na mchakato wa kufanyia maboresho ya Sheria ya elimu ili iende sambamba na mabadiliko ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 toleo la 2023 pamoja na maboresho ya mitaala.

 

Mhe. Wanu ameyasema hayo jijini Dar es salaam Februari 13, 2026 alipomuwakilisha Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda katika kikao cha Wadau wa Mtandao wa Elimu TEN/MET kutoa maoni ya mapitio ya sheria ya elimu, sura ya 353.

Amesema Utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo 2014, Toleo la 2023 unagusa ngazi zote za elimu na mafunzo hivyo, Wizara, pamoja na tathmini inayoendelea ya Sheria ya Elimu na sheria za Taasisi mbalimbali zilizo chini ya Wizara, inaendelea pia na mapitio ya miundo ya taasisi mbalimbali zilizo chini ya Wizara kwa lengo la kuleta tija na ufanisi katika utekelezaji wa Sera katika ngazi zote za elimu na mafunzo.

“Sote tutakubaliana kuwa uwepo wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya 2014, Toleo la 2023 ni jambo moja, lakini utekelezaji wake unahitaji nyenzo mbalimbali za kuiwezesha Sera yenyewe kutekelezeka. Nyenzo mojawapo ni kuwepo kwa Sheria ya Elimu iliyoboreshwa hvyo tunawashukuru kwa kuendelea kutoa maoni ya kuboresha sharia yetu ya elimu,” amesema Mhe. Wanu

Kwa upande wake Bi Martha Makala Mratibu Taifa Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET) amesema Mapitio ya Sheria ya elimu ya mwaka 1978   sura  ya 353 inatoa fursa ya kuijenga Tanzania yenye elimu jumuishi, haki, yenye ubora inayolinda watoto na wanafunzi katika kutatua changamoto ikiwemo ukosefu wa ajira

Ameipongeza Wizara kwa kutekeleza tamko la kisera la kushirikisha wadau  kwenye mchakato huo, hatua inayoongeza wigo wa kufanya kazi na wadau na kwamba wao kama Mtandao wamepata fursa ya kutoa maoni katika maeneo yanayohitaji maboresho  katika sheria ya Elimu ya Mwaka 1978.

Ameyataja maeneo hayo kuwa ni wanafunzi  kukatisha masomo, kuwepo kifungu cha sheria kinachoeleza bayana kuhusu wanafunzi waliokatisha masomo kuhakiksha wanamaliza mzunguko wao wa masomo ili kuwa na undelevu wa kuwarejesha walioacha masomo,

Elimu ya lazima miaka 10 iwekwe kisheria ili kuwa endelevu,elimu bila  ada iwekwe kisheria ili kuwa na uendelevu, lishe shuleni wazazi na walezi iwekwe kisheria  ili kuongeza uwajibikaji  kwa baadhi ya wazazi na walezi, kufanyika marekebisho ya sheria kwa ajili ya  kuondoa ukinzani uliopo kwenye sheria ya ndoa na sheria itakayohakikisha uendelevu wa Bodi ya kitaaluma ya walimu.

Nae Mwenyekiti wa Kamati ya Mapitio ya Sheria ya Elimu ya mwaka 1978 Prof. Saudin Mwakaje amesema mapitio ya sheria hayo yanalenga kuimarisha mifumo ya kijamii na kiuchumi na kukidhi  mahitaji ya mabadiliko mapya  hususani utekelezaji wa mikataba ya kimataifa na uhalisia wa soko la ajira.   

Wakichangia maoni yao kuhusu uboreshaji wa sheria ya elimu, wadau wameiomba Wizara kuangalia upya suala la muda wa masomo ya ziada (tuition) wakisema  baadhi ya walimu hutumia muda wa vipindi vya ziada kufundisha mada ambazo zingepaswa kufundishwa darasani, hali inayowaweka katika mazingira magumu wanafunzi wasioweza kuhudhuria vipindi hivyo. 

Pia  wamependekeza lugha ya alama ifundishwe kuanzia shule za msingi hadi vyuo vikuu, ili kurahisisha mawasiliano, hususan katika maeneo muhimu ya huduma za jamii kama hospitali na masoko.

Kadhalika, wadau wamependekeza shule mpya za sekondari zinazojengwa nchini ziwe na majengo ya mabweni, hatua itakayosaidia kulinda watoto wa kike dhidi ya vishawishi mbalimbali na kuongeza usalama pamoja na ufanisi wao katika masomo.