Moshi. Serikali kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura) imeanza utekelezaji wa ujenzi wa barabara ya Spencon–Mabogini–Kahe Chekereni yenye urefu wa kilomita 31.25 kwa kiwango cha changarawe utakaogharimu zaidi ya Sh7 bilioni.
Ujenzi wa mradi huo unalenga kuboresha huduma za usafiri na usafirishaji, ikiwa ni kurahisisha mawasiliano ya barabara kati ya vijiji 12 na kata tatu na maeneo ya biashara, pamoja na kuchochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi na kijamii katika wilaya hiyo.
Leo, Februari 13, 2026, kamati ya siasa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Moshi Vijijini imepita kukagua mradi wa barabara hiyo kujionea ujenzi unavyoendelea na kumtaka mkandarasi kukamilisha ujenzi huo kwa wakati uliopangwa, ambapo inatarajiwa kukamilika mwaka huu.
Akizungumzia mradi huo, Meneja wa Tarura Wilaya ya Moshi, Godfrey Mbena, amesema kukamilika kwa ujenzi wa barabara hiyo, ambayo inapita katika kata za Kahe Magharibi, Kahe Mashariki na Mabogini, kutatoa fursa kwa wananchi wa maeneo hayo kufanya shughuli zao za kiuchumi na kijamii kwa urahisi.
“Barabara hii ina jumla ya kilomita 31.25 na inapita katika kata tatu katikati ya vijiji 12. Barabara hii ni muhimu kwa kuwa ina wakazi wengi, na wanajishughulisha na shughuli za kilimo, ikiwemo cha mpunga na mbogamboga, na pia hutumika kufika katika huduma mbalimbali za kijamii.
“Katika mwaka wa fedha 2024/25, Tarura Mkoa wa Kilimanjaro tulipata mradi wa Sh7 bilioni toka Mfuko wa Barabara kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii yenye kilomita 31.25 inayojengwa kwa kiwango cha changarawe katika Wilaya ya Moshi,” amesema.
Aidha, amesema kukamilika kwa ujenzi huo kutaondoa na kupunguza maeneo yenye vikwanzo na kufanya barabara kupitika katika kipindi chote cha mwaka bila changamoto kubwa.
Barabara ya Spencon-Mabogini-Kahe- Chekereni ambayo inajengwa kilomita 31.25 kwa kiwango cha changarawe pamoja na mitaro mikubwa , ambapo itatumia gharama ya Sh7 bilioni. Picha na Janeth Joseph
Akizungumza wakati wa ukaguzi huo wa barabara, mkuu wa wilaya hiyo, Godfrey Mnzava, amesema ujenzi wa barabara hiyo utakapokamilika utasaidia wakulima wa mpunga kusafirisha mazao yao kwa urahisi kutoka mashambani kwenda masokoni.
“Kukamilika kwa barabara hii kutatoa tiba ya changamoto ya mafuriko iliyodumu kwa muda mrefu katika huu ukanda wa chini, ambao umekuwa na mafuriko kwa kipindi kirefu, hivyo kwa kutengeneza barabara hii na mitaro hii mikubwa kutasaidia kupunguza changamoto hii ya mafuriko,” amesema Mnzava.
Aidha, Mnzava amemtaka mkandarasi anayetekeleza mradi huo kuongeza kasi katika kutekeleza mradi huo, ambao umefikia asilimia 19 ya utekelezaji wake.
“Tupo asilimia 19 ya utekelezaji, Serikali tutaendelea kuhakikisha tunakamilisha mradi huo kwa wakati kwa mujibu wa mkataba unavyosema,” amesema Mnzava.
Naye, Katibu wa CCM Wilaya ya Moshi Vijijini, Ramadhani Mahanyu, amesema chama hicho kimeridhishwa na ujenzi huo na kumtaka mkandarasi kukamilisha kwa wakati.
“Tunaishukuru Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutuletea fedha nyingi za miradi. Mradi umeanza, shughuli zinaendelea, tumeridhishwa na kazi hii inayofanyika katika barabara hii, ni jambo la fahari sana,” amesema.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa kata ya Mabogini, unapopita mradi huo, Diwani wa kata hiyo, Joshua Mmuru, ameishukuru Serikali kujenga barabara hiyo ambayo kwa muda mrefu wananchi wamekuwa wakipita kwa shida, hususani kipindi cha mafuriko.