Dar es Salaam. Shahidi wa tano wa Jamhuri katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, ameieleza Mahakama kuwa aliposikiliza hotuba ya Lissu kuhusu kukinukisha kuzuia uchaguzi kwa kuuvuruga alishawishika kuwa miongoni mwa vijana watakaoshiriki mpango huo.
Shahidi huyo ambaye ni miongoni mwa mashahidi fiche wa Jamhuri ( waliopewa ulinzi, yaani wasiotakiwa kuonekana wala kutambulika), ametambulishwa kwa jina la P6 (24) na ametoa ushahidi wake akiwa ndani ya kizimba maalumu ambacho hakimuwezeshi kuonekana kwa wasikilizaji wala mshtakiwa isipokuwa kwa majaji tu.
Lissu anakabiliwa na shtaka moja la uhaini kinyume na kifungu cha 39(2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, linalotokana na maneno aliyoyatamka kuhusiana na kusudio la kuzuia kufanyika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Anadaiwa kuwa, Aprili 3, 2025, jijini Dar es Salaam, akiwa raia wa Tanzania, kwa nia ya uchochezi alishawishi umma kuzuia kufanyia kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, huku akitamka na kuandika maneno ya kumshinikiza kiongozi mkuu wa Serikali ya Tanzania kuwa:-
“Wakisema msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli…, kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi, hivyo ndivyo namna ya kupata mabadiliko…, kwa hiyo tunaenda kikinukisha…, sana sana huu uchaguzi tutaenda kuuvuruga kwelikweli…, tunaenda kukinukisha vibaya sana…”
Kesi hiyo inayosikilizwa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam na jopo la majaji watatu linaloongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Iringa, Dunstan Ndunguru akishirikiana na James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde, iko katika hatua ya usikilizwaji wa ushahidi wa upande wa mashtaka.
Katika mwendelezo wa ushahidi wa Jamhuri, shahidi huyo wa nne katika ushahidi wake leo Alhamis, Februari 13, 2026 akiongozwa na mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali, Cuthbert Mbilingi, ameeleza kuwa, yeye ni mkazi wa Songea na ni ofisa usafirishaji kwa kutumia bodaboda.
Amedai kuwa, mwaka 2024 alianza kushiriki siasa za Chadema kwa kuhudhuria mikutano mbalimbali ya hadhara na kuwafuatilia baadhi ya viongozi ili aweze kuwafahamu na kwa kipindi hicho alifanikiwa kuwafahamu viongozi akiwamo Lissu na baadhi wa Songea kama Katibu wa Vijana Songea aliyekuwa akiitwa Chiza maarufu kama Mwamba wa Kigoma.
Amedai kuwa, ilipofika Januari 2025 ndipo akavutiwa na kutaka kuwa mwanachama wa chama hicho, hivyo, alimfuata Chiza akamweleza nia yake hiyo ya kuwa mwanachama wa Chadema.
Amedai kuwa, Chiza alimuahidi kumshughulikia kufanikisha kupata kadi ya uanachama na akamuahidi kuwa atakuwa anamshirikisha katika shughuli mbalimbali za chama ikiwamo kuandaa mikutano na wao kama bodaboda ili waongoze misafara wakiwa na bendera.
Amedai kuwa, Aprili 4, 2025, akiwa sehemu yake kazi akiwa na simu yake aina ya Infinix Smart8, iliyokuwa na bando la intaneti, alikuwa anaangalia mtandao wa kijamii wa YouTube.
Amedai kuwa, aliingia kwenye chanel ya Jambo TV ambako aliona na kusikiliza hotuba aliyokuwa anaitoa Mwenyekiti wa Chadema akihutubia watu, katika mazingira ya ukumbini na nyuma ya ukuta kulikuwa na kitambaa ambacho kilikuwa na rangi ya bendera ya Tanzania na pembeni kulionekana bendera ya Chadema.
Amedai kuwa, Lissu ambaye anamfahamu kama mwanasiasa mkongwe na maarufu, siku hiyo alikuwa amevaa kombati ya rangi khaki.
Amedai kuwa, katika hotuba hiyo alimsikia Lissu akisema kwamba, “bila mabadiliko hakuna uchaguzi, hivyo tunaenda kukinukisha, tunakwenda kuvuruga uchaguzi.”
Amedai kuwa, alimsikia akisema kuwa, “tunakwenda kukinukisha na yeyote ambaye atataka kwenda na sisi tutakwenda naye ambaye hatataka tutamuacha…
“Kama kuna mtu ambaye anatarajia kugombea udiwani, ubunge, asahau, hata mimi mwenyekiti kuhusu kugombea uraisi hilo sahau. Bila mabadiliko hakuna uchaguzi. Watasema tunafanya uasi, ni kweli utakuwa ni uasi bila mabadiliko hakuna uchaguzi.”
Amedai kuwa, baada ya kuona na kusikiliza kwa makini hiyo video, maneno yake yalimwingia moyoni na yalimshawishi kutamani kuwa miongoni mwa watu ambao watashiriki ajenda ya kuzuia uchaguzi, bila mabadiliko, kwa kukinukisha, kwa maana ya kufanya vurugu au kuharibu uchaguzi.
Amedai kuwa, uchaguzi huo ulikuwa ni uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 wa madiwani, wabunge na Rais.
Shahidi huyo amedai kuwa, baada ya kushawishika na hotuba hiyo alimfuata mwenyekiti wa vijana, wakati huo Chiza ambaye alikuwa Songea, akamweleza nia yake ya kuwa miongoni mwa vijana ambao watashiriki kukinusha kabla ya mabadiliko ya uchaguzi.
Amedai kuwa, Chiza alimsifia kwa uamuzi mzuri na wa kishujaa na akampongeza, akisema vijana kama yeye ndio vijana wanaotakiwa kulikomboa Taifa.
Amedai kuwa, Chiza alimuahidi kuwa chochote ambacho kitakuwa kinaendelea kuhusiana na harakati hizo za kukinukisha atamshirikisha na kumuunganisha makundi mbalimbali ambayo yanajadili mipango ya kudai mabadiliko kabla ya uchaguzi.
Amedai kuwa, Chiza alimuunganisha kwenye kundi lililoitwa Siasa Yetu Update.
Amedai kuwa, baada ya mazungumzo yao hayo kila mmoja aliendelea na shughuli zake.
Shahidi huyo, amedai kuwa, Aprili 6, 2025 alipata taarifa kutoka kwa Chiza, kuwa mwenyekiti wa Chadema, Lissu atakuwa na ziara mkoani Ruvuma na taarifa hiyo iliwataka kufanya maandalizi ya kumpokea mwenyekiti na ilipangwa angekuwa Songea Aprili 10, 2025 , uwanja wa Shule ya Msingi Matalawe, Songea.
Amedai kuwa, Aprili 9, 2024 alipata taarifa kuwa mwenyekiti alikamatwa wilayani Mbinga akiwa ziarani na alimuulizia Chiza kuhusu ukweli wa taarifa hiyo na Chiza akamthibitishia kuwa ni kweli mwenyekiti amekamatwa lakini ratiba ya mkutano wa Aprili 10, 2025 itakuwa palepale na akamtaka ajiandae kuwepo mkutanoni hapo.
Amedai kuwa, Aprili 10, 2025 walikusanyika uwanja wa Shule ya Msingi Matalawe kuwasubiri viongozi walioambatana na mwenyekiti ili wahutubie mkutano.
Amedai kuwa, viongozi hao walikuwa ni Godbless Lema, Dk Wilbroad Slaa na makamu mwenyekiti wa Chadema, John Heche.
Amedai kuwa, wakati wanawasubiria viongozi hao lilitokea gari la polisi likawatawanya kwa kuwa, siku hiyo hakutakuwa na mkutano hivyo walikuwa hawaruhusiwi kukaa eneo hilo.
Amedai kuwa, walitawanyika kuelekea ofisi za chama, zilizoko Faranyaki, Songea ili kujua nini kinachoendelea ambako waliwakuta waandishi wa habari wakijiandaa kuongea na viongozi, akiwemo Anely Mayala, aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kusini.
Amedai kuwa, ghafla lilifika gari la polisi na mabomu ya machozi na kuwatangazia watawanyike. Waliondoka kuelekea Shule ya Msingi Matalawe na alifika Heche aliwaeleza kuwa, amepokea barua kutoka polisi kwamba, hapatakiwi kufanyika mkutano eneo hilo na akawataka watawanyike
Amedai kuwa, Aprili 18, 2025 akiwa kwenye shughuli zake alipokea taarifa kuwa Aprili 20, 2025 iliyokuwa siku ya Pasaka, kutakuwa na matembezi ya hiyari yakiambatana na kugawiwa t-shirt zenye maandishi ‘no reforms, no election’ ili kuendelea kusisitiza msimamo wa chama.
Amedai kuwa, maandalizi ya t-shirt hizo yaliendelea na wakatakiwa kuchangia kwa ajili ya kusafirishwa kutoka Dar es Salaam.
Amedai kuwa, Aprili 20, 2025 asubuhi t-shirt zilizoagizwa kutoka Dar es Salaam zilifika na kila mmoja aligawiwa t-shirt yake, na wakaelezwa katika kundi lao la Siasa Yetu kuwa, jioni saa 10 ndio lingefanyika tukio la matembezi ya hiyari.
Walikubaliana wakutane Songea Mjini kwa Disi Kitimoto.
Amedai kuwa, saa 10 jioni ya siku hiyo baada ya kusogea eneo hilo kwa ajili ya kusubiria bodaboda wengine, akiwa amevaa t-shirt ya ‘no refoms, no election,’ ghafla lilifika gari la polisi na askari waliokuwepo wakajitambulisha kuwa ni askari kutoka Kituo cha Polisi Songea na wakawaeleza kuwa wanahitajika kituoni hapo kwa ajili ya mahojiano.
Amedai kuwa, waliwakamatwa na kuwekwa ndani ya gari kisha wakapelekwa katika kituo cha Polisi Songea ambako walijulishwa kuwa wana tuhuma za kupanga maandamano bila kibali.
Amedai kuwa, walielezwa kuwa watahojiwa na kisha watatoka kwa dhamana lakini wakatakiwa kuripoti kwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa (RCO) Ruvuma, Aprili 25, 2025.
Amedai kuwa, Aprili 25, 2025 waliripoti ofisi ya RCO Ruvuma na RCO akawataka waelezee namna ilivyokuwa hadi kufika mahali hapo.
Baada ya kuhitimisha ushahidi wake huo mkuu shahidi huyo amehojiwa na mshtakiwa Lissu maswali mbalimbali ya dodoso kuhusiana na ushahidi wake huo.