Moshi. Shahidi wa kwanza wa upande wa Jamhuri katika kesi ya makosa ya kimtandao inayomkabili Mchungaji Godfrey Malisa, ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi jinsi alivyopokea vielelezo na kukabidhi kingine maabara ya kisayansi Dar es Salaam kwa ajili ya uchunguzi.
Shahidi huyo, askari polisi G 1671 Sajenti Chediel, ambaye ni mtunza vielelezo katika Kituo cha Polisi cha Kati Moshi, ameeleza mchakato huo wakati akitoa ushahidi wake katika kesi hiyo jana Alhamisi, Februari 12, 2026.
Katika kesi hiyo ya jinai namba 28411/ 2025, Malisa anatuhumiwa kuchapisha taarifa kwenye mtandao wake wa YouTube, akidai Rais Samia Suluhu Hassan anatakiwa kujiuzulu kwa kusimamia mauaji ya maelfu ya Watanzania.
Katika kosa la kwanza, upande wa mashitaka unadai kuwa, mchungaji Malisa alitenda kosa hilo Novemba 15,2025 huko Miembeni wilayani Moshi na alichapisha maneno hayo katika akaunti ya YouTube yenye jina Godfrey Malisa.
Hati ya mashitaka inanukuu maneno aliyoyachapisha kuwa: “Samia Suluhu Hassan anatakiwa kujiuzulu mara moja kwa kuwa amekuwa ni Rais aliyesimamia mauaji ya maelfu ya Watanzania.”
Upande wa Jamhuri unadai alichapisha maneno hayo akijua kuwa taarifa hizo hazikuwa sahihi na zilikuwa na lengo la kupotosha umma wa Watanzania.
Katika kosa la pili, anatuhumiwa kufanya uchochezi kinyume na Kifungu cha 35 cha Kanuni ya Adhabu sura ya 16 kama kilivyofanyiwa marejeo mwaka 2023.
Maelezo ya kosa ni kuwa Novemba 15, 2025 huko Miembeni Wilaya ya Moshi, anadaiwa kuchochea umma wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutenda kosa la jinai ambalo ni kufanya mkusanyiko usio halali kinyume cha sheria.
Jana, Jamhuri iliwakilishwa na Wakili Frank Wambura, huku Malisa akitetewa na jopo la mawakili watano wakiongozwa na Wakili Deogratias Matata.
Akitoa ushahidi wake wa msingi, shahidi huyo ameieleza Mahakama kuwa ana uzoefu wa miaka 19 kazini baada ya kupata mafunzo Chuo cha Polisi Moshi (CCP), mwaka 2008 hadi 2009.
Amedai kuwa, baadaye mwaka 2024/25 alipata mafunzo maalumu ya masuala ya utunzaji vielelezo katika Chuo cha Polisi Zanzibar na kutunukiwa cheti cha utunzaji wa vielelezo.
Amedai kuwa, akiwa kama mtunza vielelezo katika Kituo Kikuu cha Polisi Moshi, wajibu wake ni kupokea vielelezo, kuingiza kwenye kitabu cha vielelezo cha PF 16, kuweka alama vielelezo na kuvihifadhi katika chumba maalumu cha kuhifadhia vielelezo.
Amedai kuwa, usalama wa chumba cha kutunzia vielelezo ni imara kwa kuwa, kuna kamera za CCTV mbili, anayemiliki funguo za chumba hicho ni yeye mwenyewe na hakuna mtu anayeingia kwenye chumba hicho isipokuwa yeye au ukaguzi maalumu wa viongozi.
Amedai kuwa, Novemba 19,2025 saa tano na nusu usiku akiwa nyumbani (line polisi), alipata ujumbe kutoka kwa mwenzake PF 21242 Inspekta Nickson aliyemtaka afike kituoni hapo kwa kuwa, kulikuwa na vielelezo vya kuhifadhiwa.
Amedai kuwa, walienda hadi karibu na mlango wa chumba cha kuhifadhia vielelezo hivyo na baada ya kukabidhiwa bahasha za kaki alibaini zilikuwa na laptop mbili ikiwamo HP na chaja yake mashine pamoja na simu aina ya Infinix note 10.
Amedai kuwa, kwa nje ya bahasha hizo kulikuwa na karatasi yenye kesi namba Moshi IR/6544/2025, jina la askari aliyekusanya vielelezo hivyo ambaye ni Inspekta Nickson na jina la mtuhumiwa (Malisa).
Amedai kuwa, baada ya kupokea vielelezo hivyo aliviingiza katika kitabu cha vielelezo (PF 16) ambacho pia kilipokelwa mahakamani hapo kama kielelezo.
Baada ya kumaliza ushahidi wake wa msingi shahidi huyo aliwekwa katika kikaango cha maswali ya dodoso kutoka kwa mawakili wa utetezi, kutokana na mahojiano hayo shahidi huyo alieleza Mahakama kuwa, hana uthibitisho wowote kuwa simu aliyoitoa katika chumba cha kuhifadhia vielelezo iliyopelekwa maabara ya kisayansi Dar es Salaam, kama ndiyo iliyorudishwa.
Amedai kuwa, wakati anapokea vielelezo kumhusu Malisa hakukagua namba ya utambulisho wa simu (Imei) wala IP Adress ya kompyuta mpakato mbili alivyopokea kama vielelezo.
Mbele ya Hakimu Mkuu Mkazi, Ally Mkama, shahidi huyo ambaye ameieleza Mahakama kuwa yeye ndiye mtunza vielelezo, kuwa tangu apokee vielelezo hivyo Novemba 19,2025,hajawahi kujua vilivyomo ndani yake wala hajawahi kujua namba zake za utambuzi.
Akihojiwa na Wakili Matata ,shahidi huyo alidai kuwa, alipokabidhiwa vielelezo hivyo vilikuwa na kesi namba Moshi/IR/6544/2025, vikiwa na jina la askari aliyevikamata Inspekta Nickson, jina la mshtakiwa (Malisa) na yeye alivisajili katika chumba hicho maalumu na kuvipa namba 546/2025.
Amedai kuwa, Novemba 26, 2025 askari mwenye namba H 1281, Detective Zephania alimfuata akihitaji moja ya vielelezo hivyo (simu) kwa ajili ya kuipeleka maabara Dar es Salaam na kuwa alimkabidhi kufuatia barua aliyokuwa ameandikiwa na RCO kuhusu kielelezo hicho.
Amedai kuwa, Mahakama licha ya simu hiyo kurejeshwa kwake kutoka maabara hiyo, Desemba 6, 2025 akiwa kama mtunza vielelezo hakujua kilichotokea kwenye simu hiyo na kuwa hajui kama simu hiyo ndiyo aliyoitoa na ndiyo iliyorejeshwa kwake kwa kuwa, hakukagua IMEI namba yake.
Amedai kuwa, hata alipokabidhiwa hakukagua IMEI namba yake hivyo hana uthibitisho wowote kuwa simu hiyo ndiyo aliyoikabidhi kwenda maabara.
Kuhusu laptop hizo, shahidi huyo aliieleza Mahakama kuwa, hawezi kueleza iwapo vielelezo hivyo vina nini ndani yake kwa kuwa, hajawahi kuviwasha na wala hafahamu vimetoka wapi.
Alipoulizwa kuhusu mahali alipohifadhi vielelezo hivyo na usalama wake ulikuwaje, alieleza kuwa akihifadhi ndani ya chumba hicho na kuwa mfumo wa CCTV kamera hauko kwake.
Baada ya shahidi huyo kumaliza kutoa ushahidi wake, Hakimu Mkama aliahirisha kesi hiyo hadi Februari 20,2026 itakapoendelea kusikilizwa.
Mbali na kesi hiyo, mchungaji Malisa anakabiliwa na kesi ya uhaini chini ya kifungu 39(2)(d) cha Kanuni ya Adhabu sura ya 16 kama kilivyofanyiwa marejeo na Bunge mwaka 2023, akituhumiwa kuhamasisha mkusanyiko usio halali hapa Tanzania.
Februari 10,2025 mchungaji Malisa ambaye ni mwanazuoni mwenye shahada ya Uzamivu (PhD), alifukuzwa uanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM ) baada ya kupinga maamuzi ya mkutano mkuu wa CCM uliomteua Rais Samia kuwa mgombea urais.
Maamuzi ya kumfukuza uanachama yalitangazwa na Katibu wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Merce Mollel, akiegemea maamuzi ya Halmashauri Kuu ya CCM Kilimanjaro iliyomuondolea sifa ya kuendelea kuwa mwanachama.
“Malisa amefukuzwa kutokana na kukosa sifa za kuendelea kuwa mwanachama kwa sababu mara kwa mara amekuwa akibeza maamuzi halali yaliyofanywa na mkutano mkuu wa CCM taifa uliofanyika Januari 19,2025,”alieleza Mollel.
Katibu huyo alinukuliwa akidai Malisa amekuwa akitoa matamko ambayo hayaleti umoja na mshikamano ndani ya chama na nchi kutokana na kudai mkutano huo uliomteua Samia kuwa mgombea pekee ulivunja katiba jambo ambalo si la kweli.
Pamoja na kufukuzwa uanachama, bado aliendelea kupinga uteuzi huo kwa kujaribu kufungua kesi mahakamani ambazo hakufanikiwa.